Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kufungua mtandao wa barabara mpya wa Km. 826 katika kipindi cha miaka mitatu kutokana na ongezeko la bajeti.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Kagera Mhandisi Avithi Theodory wakati akizungumzia mafanikio ya miaka mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Theodory amesema kwamba TARURA imefanikiwa kufungua barabara hizo mpya ambazo awali zilikuwa ni changamoto kwa wananchi wa mkoa huo kwani walikuwa wakitembea umbali mrefu kufika eneo la huduma za jamii.
“Tumeweza kuwafungulia njia ambapo awali ilikuwa ni vikwazo kwa wananchi kwani walikuwa wakitembea umbali mrefu hadi kufikia huduma za kijamii, mfano mtu alikuwa akitembea Km. 21 lakini kwa sasa ni Km. 9, wapo wengine walitembea Km.8 na sasa wanatembea Km. 1.6 , hivyo tumejenga barabara mpya na sasa wananchi hawapati tena shida ya kutumia muda mrefu kufikia huduma za kijamii katika mkoa wetu” amesema.
Aidha, amesema Mkoa wa Kagera umetengewa bajeti ya fedha shilingi Bilioni 31 mwaka wa fedha 2023/2024 kutoka Bilioni 9 kulinganisha na miaka ya nyuma, jambo ambalo limefanya barabara za mkoa wa Kagera za vijijini kufunguliwa kwa kasi na kurahisisha maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Kagera .
“Tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani bajeti yetu imeweza kupanda mara tatu hadi kufikia Bilioni 31 tofauti na bajeti ya awali na hivyo kufanya Barabara za mkoa wa Kagera hususani za vijijini kufunguliwa kwa Kasi na kurahisisha maendeleo ya wakazi wa mkoa huu” ameongeza.
Hata hivyo amesema kuongezeka kwa bajeti hiyo imeweza kuongeza barabara zenye kiwango cha lami Km. 125 kulinganisha na Km. 80 za awali, ujenzi wa makalavati 1,600 na kufanya maeneo mengi ya vijijini kupitika kwa urahisi na hivyo kuweza kusafirisha mazao yao kutoka kijiji kimoja hadi kijiji kingine na kujipatia kipato.
Pia Serikali kupitia TARURA itaendelea kuhakikisha wanakuza miji kwa kuboresha miundombinu ya barabara ili wananchi wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara waweze kusafirisha na kuuza bidhaa zao nyakati zote katika masoko na katika kutekeleza hilo wamefanikiwa kufunga taa za barabarani zipatazo 240 na nyingine 140 zinaendelea kuwekwa sehemu mbalimbali katikati ya mji.
Naye, Bi. Kudra Kagungu, mkazi wa Biharamulo amesema kuwa Serikali inapaswa kupongezwa kwa zawadi kubwa ya kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa na wananchi wanaondokana na kero katika matumizi ya Barabara mbaya hasa za vijijini.
Amesema uboreshaji wa barabara umeweza kuwasaidia wananchi kujikomboa na umaskini na kuimarika kwa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja kwani hivi sasa maeneo mengi hakuna tena adha ya usafiri na usafirishaji wa mazao kwani sehemu nyingi ambazo walitumia kiasi cha shilingi elfu 20,000 kufuata mzigo kwa Sasa wanatumia shilingi elfu 3,000 hadi 5,000 kwa sababu barabara zimeimarika.
Kabla ya ujenzi wa barabara ya Orthodox-Rwenkorongo-Chonyonyo wananchi walikuwa wakivuka kwa kutumia mitumbwi lakini hivi sasa kukamilika kwa barabara imeweza kuwarahisishia usafiri katika maeneo hayo.
Muonekano wa barabara ya Nyaruzumbura-Kishanda B inayounganisha kijiji cha Kishanda B na Nyaruzumbura wilaya ya Kyerwa, awali hapakuwepo na barabara katika vijiji hivyo ambapo wananchi walikuwa wakitumia mitumbwi kama njia ya usafiri.
Barabara ya Biharamulo Mtaa wa uswahilini yenye urefu wa Km. 1 ambapo barabara hiyo imeweza kuongeza thamani ya eneo hilo pamoja na kuwarahisishia usafiri wakazi wa mtaa huo.