Na Albano Midelo,JamhuriMedia, Ruvuma

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Ruvuma imefanikiwa kujenga madaraja mawili yenye thamani ya shilingi bilioni 1.3.

Meneja TARURA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Wahabu Nyamzungu amesema serikali imetoa shilingi milioni 900 kujenga daraja la Libango wilaya ya Namtumbo ambalo linaunganisha vijiji vya Libangu na Mianzini.

Amesema daraja hilo lenye urefu wa meta 30 lipo umbali wa kilometa 12 kutoka Namtumbo mjini na kwamba daraja limejengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza zilitumika milioni 600 na awamu ya pili shilingi milioni 300.

Meneja TARURA Mkoa amesema katika wilaya ya Namtumbo pekee TARURA pia inatekeleza mradi wa kivuko chenye kalvati mbili kinachojengwa mjini Namtumbo ambacho kinagharimu shilingi milioni 80.

Ameongeza kuwa serikali pia imetoa shilingi milioni 90 za kukarabati barabara yenye urefu wa kilometa 30 mjini Namtumbo na kujenga barabara ya lami mjini Namtumbo yenye urefu wa kilometa moja na nusu kwa shilingi milioni 800.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Libango na Mianzini wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi wa daraja hivyo kumaliza kero kubwa ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi hao.

Mwenye kofia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akikagua ujenzi wa darala la Libango wilayani Namtumbo lililogharimu shilingi milioni 900 linalounganisha vijiji vya Libango na Mianzini

Mohamed Rajabu Mkazi wa Libango amesema kwa miaka mingi walikuwa wanapata adha kubwa ya usafiri hasa kusafirisha mazao kutoka katika Kijiji cha Libango ambacho kinazalisha mazao mengi ya chakula.

Ashura Zuberi Mkazi wa Libango amesema daraja hili sasa limekuwa mkombozi hasa kwa akinamama wajawazito ambao walikuwa wanapata shida ya kuvuka wanapokwenda kujifungua katika hospitali ya wilaya ya Namtumbo.

“Walikuwa wakifika hapa darajani ,mama anashuka pikipiki inabebwa hadi ng’ambo ya pili,kwa daraja hili tumekombolewa tunamshukuru sana mama yetu,Rais wetu Samia Suluhu Hassan’’,alisema.

Naye Hassan Moyo Mkazi wa Kijiji cha Mianzini amesema kabla ya daraja hili wananchi wa vijiji vya Libango na Mianzini walikuwa wanavuka kwenye kivuko cha miti na kwamba mawasiliano yalikuwa hafifu sana kati ya vijiji hivyo na Namtumbo.

Daraja la Libango wilayani Namtumbo ambalo tayari limeanza kutumika kwa shughuli za usafiri na usafirishaji hivyo kumaliza adha ya usafirishaji kwa wananchi

TARURA Mkoa wa Ruvuma pia inatekeleza mradi wa ujenzi wa daraja lenye urefu wa meta 25 katika Mto Msinjewe linalounganisha barabara ya vijiji vya Tuwemacho,Nasya na Mtina wilayani Tunduru.

Mwakilishi wa Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Meneja TARURA Wilaya ya Tunduru Mhandisi Silivanus Ngonyani amesema serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 326 kutekeleza mradi wa ujenzi wa daraja hilo ulioanza Aprili 2022 na unatarajia kukamilika Desemba 2022.

Salehe Ally Mohamed Mkazi wa Kijiji cha Tumewacho wilayani Tunduru amesema wanaishukuru serikali kwa kuwajengea daraja hilo kwa sababu wakati wa masika baadhi ya watu walikuwa wanapoteza Maisha wakati wanavuka ambapo kwa mwaka jana pekee watu wawili wamekufa.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akikagua mradi wa ujenzi wa daraja katika Mto Msinjewe wilayani Tunduru linalounganisha vijiji vya Tuwemacho,Nasya na Mtina,mradi unagharimu shilingi milioni 326 na unatarajia kukamilika Desemba 2022

Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameipongeza TARURA kwa kusimamia kikamilifu miradi hiyo ambayo inakwenda kumaliza kero ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Namtumbo na Tunduru.

Amesema daraja hilo lenye uwezo wa kuvusha magari yenye uzito wa tani 25 litawezesha kusafirisha mazao ya wakulima hasa zao la korosho kutoka tarafa za Namasakata,Lukumbule na Nalasi zenye uzalishaji mkubwa wa zao la korosho.

Kanali Thomas amemshukuru Rais kwa kutoa fedha nyingi zinazotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Ruvuma ikiwemo ujenzi wa madaraja,vivuko na barabara.

By Jamhuri