Sasa hapo mnaona jibu la lile swali kwa nini Wakil alijiondoa? Ndiyo sababu hakusimama mhula wa pili, aliona heri astaafu kwa heshima na ampishe Mzanzibari mwingine kuongoza chombo hiki huko Visiwani.
Baada ya Uchaguzi ule 1985-1990 huko Pemba kulitokea vitimbwi vingi tu. Waziri Kiongozi akiwa Maalim Seif hakuonesha ule moyo wa kusaidiana na Rais.
Kuna matukio huko Pemba sina shaka yameonesha viashiria vya uvunjifu wa amani kabisa. Tumesikia kituko cha wananchi kuchana Bendera ya CCM na kuichoma moto. Hilo halikukemewa na uongozi wa Serikali. Lilitokea lile tendo la kuchanwa picha ya Mwenyekiti wa CCM mbele ya viongozi wa chama na Serikali katika mkutano, halikukemewa na yeyote yule. Ukaja mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na uongozi wote wa chama na Serikali, na Mwenyekiti wa Chama, Mwalimu Julius Nyerere, alihutubia na hapo inasemekana Wapemba walidiriki kutamka haya, “wasikudanganye hao bwana, hapa (Pemba) chama kimekufa!”
Si hayo tu, bali vitendo vya uhasama baina ya Wapemba wa CUF na wa CCM vilijitokeza waziwazi. Kulipata kujitokeza watu wasiojulikana waliochukua kinyesi cha binadamu wakapakaza kwenye kuta na mbao kwenye ofisi wanamofanyia uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ule wa 1990. Hakuna wa kulikemea hata hili.
Hapo matukio namna hayo yanaashiria amani ya kweli au chokochoko za mapambano? Ni viashiria vya mawimbi yaliyotikisa sana chombo (ngalawa) cha nahodha Wakil. Hapa ndipo Mzee Wakil alipopata lile wazo la kuuacha unahodha wa SMZ kwa kupumzika kutoka mambo ya siasa (Tazama hayo katika RADI toleo la Septemba 8, 1990 kurasa zile 20-21).
Kadhalika, ilifikia mahali mwaka 1988, Mzee alidiriki kutamka kwa madai kwamba kulikuwamo baadhi ya mawaziri wa SMZ wakipanga kupindua Serikali.
Hapa alisema wazi kwamba anawajua watu hao na kwamba walikuwa wakikutana kwa faragha katika majumba ya ibada na kwamba alikuwa na taarifa pia za misaada watu hao wanayopata kutoka nje ya nchi. Basi ni katika hali ya mawimbi namna hiyo ndipo akaja na hilo wazo la kupumzika kwa heshima na kuachia ngazi, ili chombo anachokiongoza kipate nahodha mpya akivushe kwenye mawimbi makali namna ile.
Kwa udukuzi wangu huo je, hapo swali langu ni nani wa kukemea mawimbi namna hiyo Zanzibar? Kama mawimbi hayakemeki nani basi angefaa kupiga makasia kwa kasi kuondoa chombo SMZ katika hayo mawimbi makali?
Inatosha mpaka hapo kwa msomaji kuona utata wa hali ya kisiasa huko Visiwani. Lipo tatizo kubwa la Upemba na Uunguja. Lipo tatizo la usongo wa matabaka ya Waafrika na Waarabu. Lipo tatizo na kujua nani huko Zanzibar ni Mzanzibari mzalendo na nani ni mamluki anayetumikia nguvu za nje ya nchi.
Hapo ndipo Balozi Amina Salum Ali anaposema kwa mshangao iweje Maalim Seif alalamike wakati yuko serikalini kama Makamu wa Kwanza, anakula halua na mwenzake Dr. Shein? Wanafurahi pamoja lakini akitoka nje anageuka? Tutafika wapi kwa tabia za siasa za namna hii? Balozi anauliza kwa mshangao.
Turudie kwenye hali halisi ya mitazamo ya Wazanzibari. Yuko mwanaharakati msomi na mwanasheria huko Visiwani ametoa mawazo ya uwazi na ukweli. Kwanza anasema “maana ya Mapinduzi imepotea Zanzibar katika siku ya kilele cha Sherehe ya Mapinduzi Jan, 12, 2016.Ametamka kuwa huu ni wakati sahihi kwa Serikali na Wazanzibari kujitathmini kama kweli tumeienzi mbegu ya Mapinduzi. Mwanaharakati huyu anakiri kuwa kabla ya Mapinduzi kulikuwa na makundi mchanganyiko ya Waafrika, Waarabu, Wahindi, Washirazi na kadhalika kwa sababu Zanzibar kilikuwa ni kituo kikuu cha biashara.
Mchanganyiko huo ulisababisha kuwapo kwa ubaguzi na ilikuwa vigumu kuwapo kwa ndoa za mwingiliano katika jamii. Kulitolewa Amri No. 6 ya Baraza la Mapinduzi mapema mwaka 1964, na kutokana na amri ile kuliwekwa wazi madhumuni ya yale Mapinduzi ni kwamba kila Mzanzibari kupata haki sawa, Mswahili, Mwarabu, Mhadimu na Mshirazi. Pia Mapinduzi yale yalikuwa kuhimiza umoja na mshikamano na kuweka utawala wa Visiwani mikononi mwa wananchi.
Anashangaa kuona Zanzibar hawatimizi yale malengo ya Mapinduzi. Kwa sasa Zanzibar kuna ubaguzi. Na kwa maoni yake ubaguzi wa aina yoyote ile ni dhambi. Ubaguzi wenyewe unapaliliwa baina ya watu wa Unguja Waarabu na Waafrika. Ubaguzi wa aina yoyote ile ni mbaya na hiki ni kitu kibaya (soma hayo katika Mwananchi Toleo Na. 5647 la Januari 12, 2016).
FATMA KARUME: “MAANA YA MAPINDUZI IMEPOTEA ZANZIBAR”
>>ITAENDELEA