Picha ya Waziri MagembeNaanza kuona nuru ya uhuru wetu na heshima vikirejea kupitia Serikali hii ya Awamu ya Tano. Ni dhahiri kuwa nchi imerudi mikononi mwa viongozi wazalendo ambao hawatishiwi nyau wala kupokea amri kutoka Marekani.

Ile kinga waliyopewa wageni kuvunja sheria za nchi wapendavyo imekwisha. Ni wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inajijengea heshima kwa kukwepa aibu waliyokuwa wameikumbatia viongozi wetu waliopita ambao waliwasaliti Watanzania wenzao huku wakiwalamba miguu na kuwaabudu wageni ili kutibu njaa na tamaa zao.

Agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, lililotaka kupitiwa mikataba yote inayohusu uanzishwaji wa Ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba na onyo lake dhidi ya tabia ya wawekezaji kunyanyasa wananchi kwa kisingizio cha uwekezaji; vinaleta faraja kubwa na kurejesha matumaini kwa Watanzania. Hii ni baada ya hisia za muda mrefu kuwa ukoloni umerejea nchini au nchi imeuzwa kupitia uwekezaji.

Kampuni ya Mwiba Holdings na kampuni dada zake- Tanzania Game Trackers and Safaris na Wengert Windrose Safaris-zimekuwa kero kwa muda mrefu, si katika eneo la Makao tu, bali Tanzania nzima huku zikifumbiwa macho na kutetewa na wakubwa.

 

Friedkin Conservation 

Fund ni nani?

 Friedikin Conservation Fund (FCF) ni Kampuni tanzu ya kampuni za uwindaji zinazomilikiwa na bilionea Mmarekani, Friedkin. Kampuni hizi zimekuwa mstari wa mbele kuvuruga tasnia ya uwindaji wa kitalii nchini. Zimekuwa zikikiuka sheria za nchi kwa makusudi huku zikionekana dhahiri kuwa ziliiweka Serikali iliyopita mfukoni. Zimekuwa zikijivisha joho la kusaidia juhudi za uhifadhi ingawa zimekuwa zikitajwa kujihusisha na ujangili na uhalifu mwingine. Zimekuwa zikiyafanya haya kwa kutumia vibaraka wao ambao ni viongozi wa Serikali na baadhi ya wabunge.

Kampuni hizi zimekuwa na ujasiri wa kudai hadharani kuwa zina uwezo wa kuamua nani awe Waziri wa Maliasili, nani awe Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira; na nani awe Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori! Kampuni hizi zimekuwa zinamwagiza waziri nini cha kufanya huku zikikiuka sheria za nchi kwa makusudi bila kufanywa lolote.

Kampuni za Friedkin zimekuwa zikiendesha shughuli zake kihuni na kwa ubabe na hata zimefikia kutishia amani kwa wananchi, wawekezaji wenzao na hata wageni watalii kiasi cha kuharibu jina zuri la Tanzania na kuifanya ionekane kuwa si mahali salama kwa utalii.

Kwa mfano, kule Lake Natron na Makao WMA (eneo jirani na Mwiba Ranchi) kampuni hizi zimewahi kuharibu miundombinu katika vitalu walivyovitaka wao, lakini wakavikosa. Wamewahi kufunga barabara na kuchimba mashimo katika viwanja vidogo vya ndege (airstrips) ili kuzuia wawekezaji wenzao wasifanye biashara. Wamewahi kutishia wageni kwa helikopta na magari, na hivyo wageni wengine kuamua kukatisha safari na kurejea makwao.

Pamoja na uhuni huo, Lazaro Nyalandu kwa kutumia nafasi yake ya uwaziri alinyang’anya vitalu kutoka kwa kampuni zilizokuwa zimemilikishwa kihalali na kuvigawa kwa rafiki zake hao Wamarekani huku akikiuka kabisa Sheria na Kanuni za uwindaji wa kitalii.

Sheria inaweka ukomo wa idadi ya vitalu kwa kampuni; inataka mchakato wa kugawa vitalu ufanywe na Kamati ya Ugawaji Vitalu; inataka mchakato huo uanze kwa kutangazwa kwanza kwenye vyombo vya habari na waombaji washindanishwe kwa kuzingatia vigezo; inataka kampuni inayoomba kitalu iwe imeandikishwa kama Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii.

Kampuni hizi zimewahi kutajwa kuhusika kwenye ujangili na magari yao yamewahi kukamatwa na bangi. Kampuni hizi zilitajwa kuwarubuni aliyekuwa Waziri wa Maliasili, Nyalandu, Mkuu wa Wilaya – Rosemary Kirigini, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, – James Lembeli, pamoja na Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii – Peter Msigwa (Chadema), ili kuwatumia kufanikisha mambo yao. Na bila woga naamini watu hawa walijitahidi sana kuwatumikia ‘waajiri’ wao hawa.

Kampuni hizi zimewahi kumkabidhi Nyalandu hundi hewa ili kuuhadaa umma kuwa wako mstari wa mbele kusaidia juhudi za uhifadhi. Hadi leo hundi hiyo ya mamilioni ya dola za Marekani haijawahi kuonekana na Nyalandu hakuwahi kutoa maelezo yoyote.

Aidha, kampuni hizi zilimpa Nyalandu ndege ya kutumia wakati wa kampeni zake za ubunge. Katika Awamu hii ya Tano kampuni hizi zilihaha kuhakikisha kuwa Nyalandu anapata Uwaziri wa Maliasili na Utalii; na alipokosa zikaelekeza nguvu zao kuhakikisha kuwa anapata uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira- ambapo nako aliangukia pua.

Nyalandu alizizawadia kampuni hizi Leseni ya Rais ya kuua wanyamapori 704 bure wakati kisheria zilikuwa hazistahili. Aidha, Nyalandu aliamua kukiuka kwa makusudi Sheria za Ugawaji wa Vitalu na kuzipa vitalu vinane; zaidi ya idadi inayoelekezwa na sheria ya vitalu vitano, achilia mbali kwamba vitalu hivi alinyang’anya kutoka kwa kampuni nyingi zilizogawiwa kihalali na moja ya alichokiita kitalu (Mwiba Ranchi) hakikuwa kimekidhi sifa ya kuitwa kitalu kutokana na kuwa chini ya kilometa za mraba 200.

Katika Leseni ya Rais iliyotolewa kwa watu ambao hawana hadhi ya kupewa leseni hiyo, Nyalandu aliruhusu watoto wadogo chini ya miaka 15 kuwinda, kinyume cha Sheria za nchi. Hili alilifanya siku chache tu baada ya kuifungia kampuni ya mzawa kwa madai ya kutenda kosa hilo hilo.

Uanzishwaji wa Ranchi ya Mwiba wilayani Meatu ni moja ya vitendo vya dhahiri vya ufisadi na uchafu ambavyo vilitekelezwa kibabe na Nyalandu, akiwa na washirika wake kina Lembeli na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, Rose Kirigini. Ufuatao ndio ukweli kuhusu Mwiba Ranchi.

 

Mwiba Holdings

Mwiba Holdings Ltd ni Kampuni dada ya kampuni nyingine za Friedkin Conservation Fund (FCF) ambazo ni Wengert Windrose Safaris (WWS) na Tanzania Game Trackers and Safaris (TGTS).

Hata hivyo, tofauti na WWS na TGTS, Mwiba Holdings Ltd haikuwahi kuandikishwa kama Kampuni ya uwindaji wa Kitalii. Pamoja na kutambua hilo,  Julai 24, 2013 kampuni hiyo iliomba kupatiwa haki ya matumizi  ya eneo hilo kwa ajili ya utalii wa picha (photographic tourism) na uwindaji wa kitalii (tourist hunting).

Maombi haya yalitumwa moja kwa moja kwa Waziri wa wakati huo (Balozi Kagasheki). Hata hivyo, Waziri Khamis Kagasheki aliwataka wasubiri taratibu za kisheria (kanuni) zikamilike. Baada ya ombi lao kukwaa kisiki kwa Waziri, waliamua kuelekeza maombi hayo kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori huku wakitaja Kanuni ambazo hazikuwahi kuwapo (lengo likiwa kudanganya ili waonekane kuwa wanafuata sheria!) Mkurugenzi wa Wanyamapori aliwaeleza kuwa hizo kanuni walizotaja hazipo na kuwashauri wasubiri kanuni zikamilike.

Baada ya kukwama tena waliamua kwenda kwa aliyekuwa Naibu Waziri (Nyalandu) ambaye alimuita Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alex Songorwa na Msaidizi wake aliyekuwa anasimamia Matumizi Endelevu ya Wanyamapori (Profesa Jafari Kidengesho).

Nyalandu aliwaeleza wakurugenzi hao kuwa amepokea malalamiko kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwiba Holdings kuwa Idara imeinyima Kampuni hiyo haki ya matumizi (user right) katika Ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba iliyoko Meatu. Matumizi yaliyoombwa yalikuwa uwindaji wa kitalii (tourist hunting) na utalii wa picha (photographic tourism).

 

>>ITAENDELEA

By Jamhuri