Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Babati
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) imebainisha kuwa, wadudu hususani nyuki ni wanyamapori wenye mchango mkubwa katika uhifadhi wakiwa na jukumu kubwa la uchavushaji mimea ambayo hutumiwa kama chakula na wanyamapori wakubwa na wadogo.
Akitoa elimu ya wadudu kwa wanafunzi walio tembelea banda la TAWIRI wakati wa maonesho ya siku ya wanyamapori Duniani, yaliyofanyika Mjini Babati tarehe 3 Machi 2024, Mtafiti Kezia Oola alisema, mbali na jukumu la uchavushaji, wadudu wana mchango mkubwa katika uhifadhi mfumo Ikolojia.
Kezia alibainisha kuwa mdudu (Dung beetle) anasaidia utawanyaji na uoteshaji mbegu mwituni, umeng’enyaji virutubisho vya udongo hasa vinyesi vya wanyama, (decomposition) na uongezaji mbolea kwenye udongo (soil fertilization). Kwa kufanya hivi husaidia kuwezesha makazi ya wanyama wengine.
Pia, alieleza kuwa uwepo wa wadudu katika uhifadhi inasaida mzunguko wa chakula (food chain) ambapo kuna wanyama wadogo na ndege wanaotegemea wadudu kwa asilimia kubwa kama chakula chao akiwemo mnyama Mhanga (Aardvark) na wanyama hawa huliwa na wanyama wengine .
Kwa upande wake Mtafiti Kipemba Ntiniwa amebainisha kuwa katika uhifadhi nyuki anachukua nafasi kubwa katika uchavushaji tofauti na wadudu wengine kwa kuwa Nyuki wanakaa kwa makundi makubwa ambapo mzinga mmoja unakuwa na nyuki zaidi ya elfu ishirini.
“Nyuki ni mchavushaji mkuu wa kuendeleza uwepo wa mimea mbalimbali katika uhifadhi” alieleza Kipemba.
Ameongeza kuwa, nyuki wanatumika kupunguza migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori hususani tembo (Mitigation of Human-Wildlife Conflicts) ambapo uzio wa mizinga ya nyuki unaweza kuwazuia tembo kuingia maeneo/mashamba ya wananchi na kufanya uharibifu.
Vilevile, Kipemba amebainisha faida nyingine za nyuki kiuchumi na kijamii ni pamoja na kuongeza kipato kupitia utalii wa nyuki (Apitourism), uuzaji mazao ya nyuki ambayo ni asali, nta, chavua, sumu ya nyuki na maziwa ya nyuki pamoja na kusaidia uwepo na usalama wa chakula kupitia uchavushaji.
Ikumbukwe, katika Maonesho hayo yalifanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 28 February hadi tarehe Mosi Machi ,2024 Watafiti wa TAWIRI mbali na kutoa elimu katika banda la maonesho, waliitembelea Shule ya Sekondari Babati Day na Kutoa elimu juu ya umuhimu wa wadudu, tafiti za wanyamapori na uhifadhi endelevu katika kukuza utalii nchini.