Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Magharibi kilichopo Kigoma ambacho ni miongoni mwa vituo vitano vya TAWIRI, Dr. Angela Mwakatobe ametoa wito kwa watafiti na wadau kuendeleza mashirikiano ya tafiti za wanyamapori hususani spishi muhimu ya sokwe pamoja na kusambaza matokeo ya tafiti hizo kwa umma ili kuwa na uhifadhi endelevu wa sokwe hapa nchini.

Dkt. Mwakatobe amesema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Mei Mosi 2025 kutoka TAWIRI Makao Makuu iliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa Gombe, ikiwa ni safari ya pongezi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu TAWIRI baada ya kamati hiyo kufanya maandalizi na mikakati iliyopelekea TAWIRI kushinda Kombe la Mshindi wa Pili katika maadhimisho ya sherehe ya MeiMosi 2025 mkoa wa Arusha.

Aidha, Dkt. Mwakatobe amebainisha kuwa tafiti endelevu za Sokwe ni muhimu kwani wapo hatarini kutoweka (endangered) kufuatia idadi yao kupungua kwa kasi hali ikisababishwa na uharibifu mkubwa wa makazi yao ya asili.

“Sokwe wana umuhimu mkubwa katika uwiano wa mifumo Ikolojia wanayopatikana hivyo kuna sababu muhimu za kuhakikisha spishi hii inalindwa na kuhifadhiwa” amebainisha Dkt.Mwakatobe

Vilevile Dkt. Mwakatobe ameeleza mbali na Utafiti wa Sokwe, kituo kinafanya, kusimamia na kuratibu tafiti za wanyamapori katika maeneo ya kanda ya Magharibi nchini.