Na Tatu Saad,JAMHURI MEDIA

Baada ya kelele nyingi kutoka kwa baadhi ya wapenzi wa soka nchini baada ya mabeki wawili wa klabu ya Simba SC Mohammed Hussein na Shomari Kapombe kutoitwa katika kikosi cha timu ya Taifa, shirikisho la soka nchini Tanzania limetoa ufafanuzi katika hilo.
Ameeleza katibu mkuu wa TFF, Wilfred Kidao kuwa shirikisho halina mamlaka yoyote ya kutengua au kupingana na maamuzi ya benchi la ufundi la Taifa Stars, hivyo wanayaheshimu maamuzi yoyote yanayotolewa na kocha Adel Amrouche.

“Mwalimu ndiye aliyepewa mamlaka ya kuchagua kikosi cha Taifa Stars kwa Asilimia Mia. Hili ni jambo lake.Niliona mitandaoni watu wakilalamika na kuhoji. Mwalimu alikuwa anafanya kazi yake muda tu, ndiyo maana mliona tukachelewa kumtangaza. Hii ni timu ya watu wote” amesema Kidao.

Vilevile Kidao ameeleza TFF itamsaidia mwalimu kwenye mambo ya kiutawala lakini sio kumuingilia kwenye majukumu yake kwani kila mtu ana majukumu yake, hata hivyo kocha hawezi kumuacha mchezaji moja kwa moja.

“Mwalimu hawezi kumuacha mchezaji moja kwa moja. Kazi yetu TFF kumsaidia mwalimu katika mambo ya kiutawala. TFF hatuwezi kumuingilia mwalimu. Kila mmoja anafanya katika majukumu yake ya kila siku. Mimi ni kocha pia, siwezi kukubali kuingiliwa na watu, hivyo hata mimi siwezi kuona mwalimu anaingiliwa.” Amesema Katibu Mkuu wa TFF.

Tanzania inatafuta tiketi ya kucheza AFCON 2023 baada ya kushiriki Fainali hizo mara mbili mwaka 980 ilipata nafasi kwa mara ya kwanza katika fainali zilizofanyika nchini Nigeria huku 2019 ikicheza mashindano hayo nchini Misri.

Taifa Stars itacheza mchezo wa mzunguuko watatu wa Kundi F dhidi ya Uganda kesho Ijumaa (Machi 24) katika Uwanja wa Suez Canal mjini Ismailia-Misri, kabla ya timu hizo kucheza mchezo wa Mzunguuko wanne Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Machi 28.

By Jamhuri