Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) inaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaojihusisha na unajangili wa mazao ya misitu kwa kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa Sheria.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (Mb) wakati akijibu Swali la Aleksia Asia Kamguna (Mb) ambaye alitaka kujua mikakati ya Serikali ya kupanda miti katika Mkoa wa Morogoro hususan Milima ya Uluguru na kandokando ya Mto Fulua, Mnyera na Kilombero.
Kitandula aliongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Halmashauri na Wadau mabalimbali imepanda jumla ya miti 9,026,605 (ikiwemo miti 1,000,000 ya mikarafuu kwa ajili ya viungo) katika mpaka wa msitu, vijiji vinavyopakana na msitu wa Uluguru mkoani wa Morogoro.
Aidha Kitandula aliongeza kuwa katika kuhakikisha uhifadhi unaendelezwa katika Milima ya Uluguru, zoezi la kupanda miti lilifanyika kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024.
Pia Kitandula alisema kuwa kwa upande wa maeneo ya Mto Fulua, Mnyera na Kilombero, Wizara inaendelea na jitihada za kutunza maeneo hayo kwa kupanda miti rafiki wa maji pamoja na kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa uhifadhi.
”Katika kuimarisha jitihada hizo Wizara inashirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kuelimisha jamii, kuwezesha jamii kubuni na kuanzisha vyanzo mbadala vya kujipatia kipato na kupanda miti stahili katika maeneo ya kingo za mito. Wadau hao ni pamoja na Mfuko wa Uhifadhi Misitu Tao La Mashariki, AGRIWEZESHA, WWF, AWF, SAGOT, TAF na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)”. Alisema Mhe. Kitandula