Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) Gilead Teri amesema Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), imefanikiwa kusajili jumla ya miradi 2,020 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 177.47 katika kipindi cha mwezi Machi 2021 hadi Februari 2025 ikilinganishwa na miradi 728 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho, Machi 2018 hadi Machi 2021 iliyokuwa asilimia 63.19.
Ameeleza hayo leo Februari 27, 2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa kituo hicho ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipa kipaumbele sekta binafsi na uwekezaji .

Amesema Serikali imeiwezesha Tanzania kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kupitia ziara alizofanya Marekani, China, Korea ya Kusini, Jumuiya ya Ulaya, Afrika ya Kusini, Uturuki na Misri ambazo zimewezesha kuongezeka kwa wawekezaji wa ndani na kutoka nje ikiwemo Watanzania asilimia 34, wageni asilimia 42.6 na ubia asilimia 23.1.
Licha ya hayo amefafanua kuwa uwekezaji huo wa kipindi cha awamu ya sita, umezalisha ajira 523,891 ikilinganishwa na ajira 104,172 za kati ya mwaka 2018 hadi 2021, pia umeongeza makusanyo ya kituo hicho kutoka wastani wa milioni 400 hadi bilioni 1 kwa mwezi”, amesema Bw. Teri.
“Thamani ya mitaji ya miradi hiyo inakadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 23.67, ikiongezeka kwa asilimia 188 kutoka Dola za Marekani bilioni 8.2. Aidha, miradi iliyosajiliwa inatarajiwa kutoa ajira 523,891 sawa na ongezeko la asilimia 284.6 ikilinganishwa na ajira 136,232 za kipindi cha miaka mitatu yaani 2017- 2020,”amesema.

Amefafanua kuwa, Kituo hicho kimeboresha huduma kwa kuzingatia weledi na matumizi ya TEHAMA pia, uwepo wa Sheria Mpya ya Uwekezaji Na. 10 ya 2022 ambayo imeboresha kwa kiwango kikubwa mazingira ya uwekezaji huku mikoa inayoongoza kwa kusajili miradi ya uwekezaji nchini kwa mwaka 2024 ikiwa ni Dar es Salaam yenye miradi 356, Pwani 166, Arusha 64, Dodoma 47 na Mwanza 37.
Amezitaja sekta tano zilizoongoza kwa kusajili miradi mingi ikiwemo; sekta ya uzalishaji viwandani miradi 917, usafirishaji 348, majengo ya biashara 304, utalii 191 na kilimo yenye miradi 180 na kwamba moja ya malengo ya mwaka 2025 ya kituo hicho ni, kuvutia miradi mipya ya uwekezaji 1,500 na mitaji ya Dola za Marekani bilioni 15 ifikapo mwezi Desemba 2025 .

