Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Tanga

KITUO cha Uwekezaji nchini (TIC), kimesema kampeni ya nchi nzima ya kuhamasisha uwekezaji imeamsha ari ya watanzania wengi kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Afisa Uwekezaji wa kituo hicho, Valentine Kagombora, wakati akizunguza na wananchi waliotembelea banda la kituo hicho katika Maonesho ya Biashara na Utalii yanayoendelea Mkoa wa Tanga.

Maonyesho hayo yaliyoanza tarehe 28 yanatarajiwa kumalizika tarehe 6 Juni yenye kauli mbiu ya Kufungua Fursa za Kiuchumi kupitia ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi, yameshirikisha taasisi mbalimbali za serikali lengo ikiwa ni kuonyesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hizo.

Kagombora alisema Tanzania inafursa nyingi za uwekezaji na kuwataka watanzania kuunganisha nguvu ya mitaji na kusajili miradi ya ubia kwenye kituo hicho kama ambavyo wamekuwa wakifanya baadhi ya kampuni za kigeni.

Mwanzoni mwa mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizindua kampeni ya TIC kuzunguka mikoa mbalimbali kuhamasisha uwekezaji wa ndani ambayo inatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.

Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha watanzania kutumia fursa za uwekezaji zilizopo nchini na waache fikra kuwa uwekezaji ni kwaajili ya wageni pekee.

Kagombora aliwaeleza wananchi hao kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na fursa nyingi ambazo watanzania wanapaswa kuchangamkia na iwapo wataunganisha mitaji yao wanaweza kufanya mambo makubwa.

“TIC inaendelea na kampeni kwenye mikoa mbalimbali nchini ambako maofisa wa kituo wamekuwa wakikutana na wananchi kuwaeleza fursa zilizopo na namna ambaavyo serikali inatoa kipaumbele kwa wawekezaji watanzania,” alisema

Aliwaeleza wananchi hao kuwa serikali imepunguza kiwango cha mtaji kwa mwekezaji mtanzania kutoka dola za Marekani 100,000 hadi dola 50,000 tu ili kuwezesha watanzania wengi nao kuwekeza.

“Na tukisema dola 50,000 si kwamba ni fedha hapana hii inajumlisha mtaji wake wote kuanzia mashine mitambo kama ni eneo la uwekezaji vyenye thamani kama hiyo na siyo fedha taslim,” alisema

Alisema TIC imekuwa ikifanyia kazi vikwazo vyote vya biashara kimoja baada ya kingine na lengo ni kuendelea kuwavutia wawekezaji wa nje na wa ndani ya nchi waweze kuchangamkia fursa za uwekezaji.

Aliwataka watanzania kusajili miradi yao kwenye kituo hicho kama unafuu wa kodi kwenye uingizaji wa mitambo na rasilimali mbalimbali za mtaji.

Amri Mohamed ambaye alihudhuria maonyesho hayo alisema ni vyema serikali ikaweka utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara wa ndani mara kwa mara kuwapa elimu kuhusu uwekezaji kwani baadhi wanaamini kuwa uwekezaji ni kwaajili ya wageni.

“Nimefurahi kuambiwa kwamba hata mimi naweza kuwa mwekezaji sasa ni vyema elimu kama hii ikaendelea kutolewa nchi nzima ili watanzania wengi wajue kwamba fursa za uwekezaji zilizopo ni kwaajili yao pia siyo wageni pekee,” alisema