Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kwa kipindi cha miaka mitano, sekta ya bima imekuwa kwa wastani wa asilimia 12.8 kwa mwaka huku mauzi mauzo ghafi ya bima yameongezeka kutoka Sh bilioni 691.9 mwaka 2018 hadi kufikia trilion 1.2 mwaka 2022.

Pia, kutokana na mafanikio hayo ulipaji wa mafao ya bima umeimarika na kufikia asilimia 95.

Hayo yalielezwa leo Septemba 18, 2023 na Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk Baghayo Saqware wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Dar es Salaam.

Amesema mchango wa Sekta ya Bima kwenye pato la Taifa unazidi kuongezeka kutoka asilimia 0.56 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 1.68 kwa mwaka 2021.

Aidha,amesema TIRA imeendelea kuongeza gawio serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 imeweza kulipa gawio kwa serikali la Sh bilioni 2.9.

Dk.Saqware amesema sekta ya bima imechangia kwenye ajira kwa vijana ambapo hadi Septemba 2022 imetoa ajira za kudumu kwa Watanzania 4, 173.

Katika eneo la kulinda haki ya mteja wa bima, alisema Mamlaka imeendelea kuzisimamia kampuni za bima kuhakikisha zinalipa madai na fidia stahiki kwa wakati na kwa haki.

“Hadi sasa ulipaji wa madai na fidia stahiki kwa wateja wa bima umefikia asilimia 95 hivyo kupungua kwa malalamiko. Hata hivyo asilimia tano ya madai na fidia yana changamoto ambazo TIRA inafuatilia na kutoa suluhisho,” alifafanua.

Dk Saqware ametolea mfano, ulipaji wa madai ya bima za kawaida na kueleza kuwa uliongezeka kwa asilimia 10.1 kutoka Sh bilioni 301.9 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 332.09 mwaka 2022.

Aidha, amesema malipo ya madai na mafao ya bima za maisha yaliongezeka kwa asilimia 29.3 kutoka Sh bilioni 95.7 mwaka 2021 hadi bilioni 123.71 mwaka 2022. Jumla ya kiasi cha madai kilicholipwa mwaka 2022 ni Sh bilioni 455.80 hivyo, kupunguza umaskini kwa wanufaika na kufanya biashara kuwa
endelevu.

Amesema mamlaka inaendelea na uendeshaji wa mikutano ya kupokea na kusikiliza malalamiko ya bima kwa wananchi ambapo hivi karibun imefanikiwa kuandaa mikutano mitano katika kanda zote za Mamlaka.

Akizungumzia mafanikio ya TIRA kamishna Saqware amesema katika kipindi cha mwaka wa Fedha wa 2022/2023 Mamlaka imeanzisha Konsotia (Umoja) ya Bima ya Kilimo ili kutekeleza skimu ya bima ya Kilimo Tanzania kwa ufanisi.

Pia, ilianzisha Konsotia ya Bima ya Mafuta na Gesi ili kuhakikisha miradi yote ya gesi na mafuta inabakiza sio chini ya asilimia 45 ya ada zitokanazo na gesi na mafuta.

“Kufuatia kutokuwa na uwezo wa soko la ndani, vihatarishi vya nishati, vilielekezwa nje ya Nchi kwa asilimia 100. Jambo ambalo sio na lisilo na tija kwenye uchumi wa nchi,” ameeleza.

Aidha, amesema kuanzishwa kwa miradi mikubwa ya nishati kama vile bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ni fursa kwenye sekta ya bima kujipanga kwa ajili ya kuongeza tija, uchumi na ajira nchini.

Ameeleza kuwa malengo ya kuanzisha konsotia hiyo ni kutoa fursa kwa kampuni za bima za ndani kushiriki na kuandika vihatarishi vya nishati ya Gesi na Mafuta ndani ya nchi.

Pia, amesema sekta ya bima imepanga kushiriki katika bima ya mradi wa LNG, unaokadiriwa kuwa na gharama ya uwekezaji wa Dola za Kimarekani Sh Bilioni 40.

Amesema mpaka sasa kampuni 22 za Bima zimesaini Mkataba wa Muungano huo wa Bima ya Nishati ya Mafuta na Gesi Tanzania zenye jumla ya laini (hisa) 238 ambapo kila laini (hisa) ina thamani ya Dola za Kimarekani (USD) 25,000 ambayo ni jumla ya uwezo wa muungano wa kiasi cha mtaji cha dola za Marekani milioni sita.

Mafanikio mengine aliyoyataja ni katika mwaka huu wa fedha 2023/24 TIRA imeanzisha mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi ili kuifanyia marekebisho sheria ya Bima na Kanuni zake.

Amesema mchakato huo umeanzishwa kufuatia maboresho ya mifumo ya usimamizi wa Bima na maendeleo ya soko la bima nchini na kueleza kuwa wamelenga kukusanya maoni angalau ya wadau 500.

Kuhusu mikakati na mipango ijayo Saqware alisema mamlaka hiyo imepanga kuanzisha na kutekeleza Mpango wa kitaifa wa Bima ya Kilimo na kuanzisha bodi ya wataalamu wa Bima, Hifadhi ya Jamii na Takwimu Bima.

Pia, amesema imepanga kuunganisha mifumo ya kidigitali na Taasisi za umma ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, LATRA, NIDA, TASAC, TRA, PTA, ZRA lengo likiwa ni kuongeza usimamizi na maendeleo ya soko la Bima.

TIRA pia itaendelea na utoaji wa elimu ya bima kwa umma na wadau mbalimbali. “Kwa mfano Mamlaka imeandaa Semina ya Pili ya Makatibu Wakuu wote Nchini kwa lengo la kutoa elimu ya umuhimu wa ukataji bima. Semina imepangwa kufanyika Oktoba 27, 2023,”

Pamoja na hayo, alisema mamlaka hiyo itafungua ofisi za Bima Mtawanyo za Kikanda ambazo Serikali ya Tanzania inamiliki hisa za moja kwa moja au kupitia Taasisi zake ili kampuni hizo ziweze kufungua ofisi nchini kwa utaratibu wa Mikataba ya Uenyeji.

Kamishna huyo wanl bima alisisitiza kuwa Mamlaka kwa kushirikiana na Bodi ya Taifa ya Bima itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye Sekta ya Bima kwa ajili ya kuendeleza na kusimamia soko la Bima kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

“Mamlaka inapenda kuona soko la Bima lisilokuwa na udanganyifu, lenye ushindani, soko linalofuata uweledi na soko lenye kuleta faida,” amesisitiza Dk Saqware.