Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi karibu na Visiwa vya Ushelisheli, katika umbali wa takribani kilomita 1,600 kutoka pwani ya Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA iliyotolewa leo Oktoba 20,2026 kuwa uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa mgandamizo huo unatarajiwa kuimarika na kuwa Kimbunga katika eneo hilo la Bahari ndani ya kipindi cha siku nne zijazo, huku ukielekea pwani ya nchi yetu.
Mamlaka imesema uwepo wa mgandamizo huo Bahari ya Hindi unatarajiwa kuimarisha kwa kiasi mifumo inayosababisha mvua katika maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo jirani, hususani kuanzia tarehe 24 Oktoba, 2026.
Kutokana na hali hiyo, watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla wameshauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka TMA pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.
TMA imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mgandamizo huo na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini, na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

