Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Bagamoyo
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kushughulikia kapu la hoja za ardhi wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, huku ikiwataka wananchi kuheshimu haki za umiliki na kufanya uhakiki wa kina wa nyaraka kabla ya kununua viwanja ama mashamba ili kuepuka migogoro.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, Oktoba 19, 2026, wakati wa Kliniki Maalumu ya Ardhi iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo, Bagamoyo, kufuatia agizo la Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, la kushughulikia changamoto za ardhi katika eneo hilo.
Dkt. Akwilapo alisema miongoni mwa changamoto kubwa za ardhi wilayani Bagamoyo ni uvamizi wa maeneo yenye wamiliki halali, hali inayochangia kuibuka kwa migogoro kati ya wananchi.
Alisisitiza kuwa maeneo yenye hukumu za mahakama yanapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia maamuzi yaliyotolewa, akieleza kuwa wananchi wanapaswa kufuata taratibu za kisheria katika kutatua migogoro yao.
“Wizara inatekeleza agizo la Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, la kushughulikia changamoto za ardhi katika Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo pamoja na kuanzisha Kliniki Maalumu ya Ardhi ili kusikiliza wananchi wenye kero za ardhi,” alisema Akwilapo.
Alieleza kliniki hiyo iliyoanza Oktoba 19, 2026, imepangwa kudumu kwa wiki moja, huku muda huo ukiweza kuongezwa kulingana na ukubwa na wingi wa changamoto zitakazojitokeza.
Akiongoza klinik hiyo Kamishna wa Ardhi, Nathaniel Nhonge, anasisitiza umuhimu wa kutoa huduma kwa wakati na kuzingatia mahitaji ya wananchi hasa wazee,watu wenye mahitaji maalum ili kuhakikisha kuzingatia mazingira yao.
Naibu Kamishna wa Ardhi, Hussein Sadick, anahimiza umuhimu wa ushirikiano baina ya wananchi na wataalamu wa ardhi katika kufanikisha zoezi la klinik hiyo.
KAULI YA MBUNGE NA MKUU WA WILAYA
Akizungumzia kliniki hiyo, Mbunge wa Bagamoyo, Subira Mgalu, alisema itakuwa na manufaa kwa wananchi, akifafanua kuwa ombi lake lililenga kuwasaidia wananchi wenye kero za ardhi, si kuingilia mashauri yaliyokwishaamuliwa na mahakama.
“Serikali yetu chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu, Kwa hatua hii, naipongeza Wizara ya Ardhi, Waziri wa Ardhi na wataalamu wake kwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu,” alisema Mgalu.
Aliwataka wananchi kuheshimu maamuzi ya mahakama na kuepuka kuendeleza migogoro isiyoisha, akionya kuwa kutofuata taratibu za kisheria kunaweza kusababisha madhara zaidi, ikiwemo kuvunjiwa majengo yaliyojengwa katika maeneo yenye migogoro.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, aliwataka wananchi kuwa wazi wanapowasilisha kero zao za ardhi ikiwemo muda wa kero hizo na hatua zilizochukuliwa ili kurahisisha utambuzi na hatua za kuzitatua.
Ndemanga alisema baadhi ya mashauri bado yako mahakamani, huku akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuingilia maamuzi ambayo tayari yametolewa na mahakama.
Aliwashauri wananchi wasiouridhishwa na hukumu kufuata taratibu za kisheria zilizowekwa.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, alitoa agizo hilo Oktoba 16, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kongani ya viwanda ya Kampuni ya Hongwang Tanzania (HWTZ SEZ Limited) na kuzungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo, wilayani Bagamoyo.






