Unapojipangakuomba udhamini ughaibuni kuna gharama lazima uingie. Gharama hizi haziepukiki.

Gharama hizi zimekuwa kikwazo kikubwa kwa watu wengi mno. Na ndiyo maana napenda kutoa ushauri huu kuwa kama unataka udhamini ughaibuni kuna gharama haziepukiki kamwe; kuziepuka maana yake ni kukubali kushindwa. Je, unataka kuingia kwenye mchakato ukiwa mshindi au mshindwa?

Kuna kitu kinaitwa English Proficiency Language Test. Huu ni mtihani wa kupima uwezo wako wa kujua lugha ya Kiingereza. Kwa kuwa lugha mama na ya taifa ya Tanzania si Kiingereza, basi ili kukidhi haja ya kuomba na kupata udhamini unatakiwa kufanya mtihani wa kuonesha unajua Kiingereza.

Napenda kutoa angalizo kuwa kuna vyuo vichache sana, kuna baadhi ya fursa za udhamini ambazo huwa wanatoa ruhusa (exemption) kwa mtu ambaye amesoma kwa lugha ya Kiingereza sekondari ya juu hadi Chuo Kikuu elimu yake- kwa Kiingereza hana haja ya kufanya mtihani huu. Onyo ni kwamba usiache kufanya mtihani huo ukisubiria vyuo au fursa hizo, ni fursa moja kati ya hamsini.

Hivyo, usifanye mambo kusubiria bahati nasibu. Kuwa umejiandaa kila wakati, na kuwa na mtazamo wa ushindani kila wakati.

Kuna aina mbili za mitihani ya Kiingereza. Unatakiwa kufanya mtihani mmoja kati ya hiyo, na si yote miwili.

Kuna mtihani wa TOEFL (Test of English as Foreign Language); na mtihani wa IELTS (International English Language Testing System).

Mtihani wa TOEFL ni wa Wamarekani. Unatungwa na kuongozwa na Wamarekani. Mtihani huu unafanyikia Chuo Cha Mwalimu Nyerere kule Kigamboni. Gharama ya mtihani huu ni karibia dola 185. Na ukienda kwenye tovuti yao www.ets.org/toefl unaweza kupata mfumo wa mtihani upoje na sampuli ya maswali yake na mazoezi.

Lakini pia ukienda ubalozi wa Marekani kuna maktaba ambayo ni kwa watu wote bure kuingia na kujiandaa kwa mtihani huu. Lakini pia unaweza kwenda YouTube na kupata video za kukupa mwanga na mbinu za kujiandaa.

Mtihani wa TOEFL iBT (Internet Based Test) ndio unatakiwa kufanya, kwani kuna aina mbalimbali za TOEFL. Huu TOEFL iBT una maksi hadi 120, na ni vyema upate kuanzia 75 na kuendelea ili kuwa mshindani.

Mtihani wa IELTS ni wa Waingereza. Huu hufanyikia pale British Council, Dar es Salaam. Ukiingia kwenye tovuti https://ielts.britishcouncil.org/tanzania unaweza kuangalia tarehe, gharama na mambo muhimu kuhusu mtihani huu. Ukijiandikisha na kulipia utapewa na vitabu vya kujiandaa na mtihani huu. Mtihani huu gharama yake ni kama Sh 400,000 hivi.

Sharti moja kujiandikisha kufanya IELTS ni lazima uwe na hati ya kusafiria (passport), hivyo kama huna inabidi uombe Uhamiaji. Maksi za mtihani huu ni kuanzia 0-10, ni vyema upate kuanzia 6.5.

Watu wengi hupambana na kikwazo hiki. Wengi hufanya kosa kubwa la kuanza kuomba chuo na udhamini kisha wanaambiwa watoe cheti kuonesha wameshafanya mtihani huu ndipo huanza kuhangaika kufanya mtihani.

Ukitumia njia hii lazima uchelewe maana mtihani huu haupo kila siku. Unaweza kukuta unafanyika mara moja au mbili ndani ya mwezi. Hivyo kuna kujiandaa, kulipia, kwenda kufanya na kusubiri matokeo. Huchukua muda na unajikuta upo nje ya deadline. Hapo ki-mjini tunasema 3-0 na umepata technical knockout bila kujitetea.

Nini ufanye sasa? Kwa kuwa muda wa kutuma maombi kwa vyuo vingi huwa ni kati ya Agosti na Desemba, ni vyema mtihani huu uufanye kabla ya Juni. Ukifanya mapema utakuwa umejiandaa na silaha moja nzito.

Vitu vingine unaweza kuvikusanya ndani ya siku mbili tu. Ila bila mtihani huu utaishia kusema una mkosi, kuna upendeleo au kusema kupata udhamini ughaibuni ni ‘zali’ wakati umeshindwa kufuata masharti.

Watu wengine hawapendi kufanya mtihani huu kwa sababu ni gharama kubwa. Ila fahamu kuwa huwezi kupata udhamini bila kupitia njia hii. Huwezi kwenda peponi bila kufa kwanza, huo ndiyo ukweli.

Pia izingatiwe kuwa unapopata udhamini ughaibuni unapewa shilingi zaidi ya milioni 100 hivi.

Kulipiwa ada, fedha ya matumizi na kadhalika ni hela kubwa mno. Sasa nani wa kukupa hela zaidi ya Sh milioni 100 bila ya kuzingatia masharti? Nani wa kukupa Sh milioni 100 bila kujiridhisha kuwa unakuja kusoma wakati hujui Kiingereza unaweza kufeli na kufukuzwa chuo hivyo wao kupoteza hela zao kupitia wewe?

Kuna watu wengi huwa wakinifuata kwa ushauri nawapa mbinu zote, ila kitu cha kwanza lazima wafanye mtihani huu, wanakimbia. Ili kupata hasira na motisha ya kufanya mtihani huu, lipia kwanza. Ukitoa hela yako Sh 400,000 lazima utapata uchungu wa kujiandaa, kusoma kwa bidii ili upate maksi nzuri.

Mitihani hii TOEFL au IELTS haijalishi unaenda kusoma wapi- iwe Ulaya au Marekani. Kila chuo unapewa fursa ya kuchagua uwasilishe matokeo ya mtihani upi kati ya hiyo.

Unaweza kufanya TOEFL wa Wamarekani na kwenda kusoma Uingereza au kufanya IELTS na kwenda kusoma USA. Chaguo la mtihani ni juu yako.

Kwa makala zijazo, nitapenda kujibu baadhi ya maswali ya wasomaji wetu. Unaweza kutuma swali lako kupitia e-mail ebmakulilo@yahoo.com au tumia Whatsapp namba +16192284381. Tafadhali namba hiyo ni kwa Whatsapp pekee. Ukinipigia nita-block namba yako sababu unakuwa umevunja masharti ya namba niliyotoa.

Katika kuuliza swali, (a) jina lako (b) upo wapi, yaani mkoa gani, nchi gani kama upo nje ya Tanzania (c) swali lako.

Katika majibu yangu, sintoweka namba yako ya simu au e-mail yako. Nitaweka jina lako la kwanza na mahali ulipo na swali lako na majibu yangu kuheshimu faragha yako.

 

Asante sana, tuendelee kuwa pamoja

2504 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!