Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeshinda tuzo mbili ikiwemo mshindi wa jumla katika uandaaji bora wa taarifa za hesabu mwaka 2021 kwa kufuata viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu katika Taasisi za Umma yaani mfumo wa IPSASs.

Katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha NBAA Bunju jijini Dar es Salaam, TRA imeibuka mshindi wa kwanza katika uandaaji wa hesabu kwa mwaka 2021 katika kundi la Taasisi za Umma, na Mshindi wa jumla kwa Taasisi zote 2021.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Naibu Kamishna Upelelezi wa Kodi, TRA, Bw. Robert Manyama amesema tuzo hizo zimetokana na weledi katika kutekeleza miongozo ya uandaaji wa mahesabu iliyowekwa na kuhakikisha kuwa inafuatwa na waandaaji wa mahesabu yetu ndani ya TRA.

“Ni weledi tu katika kutekeleza miongozo iliyowekwa ya uandaaji wa mahesabu inayofuata na taasisi yetu ya TRA. Hali hii tunaifurahia, inatuongezea ari ya kuaminika kama chombo cha umma tunapoonyesha kwamba tunatoa hesabu zetu sawasawa basi umma unatuamini kuwa tunafanya kazi sawasawa” amesema Manyama na kutoa rai kwa taasisi nyingine za umma.

“Ni vizuri kwa taasisi nyingine za Serikali kushiriki ili kujiongezea kuaminika katika utendaji wa shughuli zao hasa sisi ambao tunatenda kwa niaba ya wananchi, ni vema sana kutumia chombo hiki chenye wataalamu wanaoweza kuonyesha utendaji wetu uko namna gani na hivi wanaonyesha tupo vizuri basi tunaaminika na wananchi” amesema Naibu Kamishna Manyama.

Aidha, Naibu Kamishna Manyama, ametoa rai walipakodi kuwa ni vizuri wakatambua kwamba kazi inayofanywa na mamlaka ya mapato ina thamani kubwa na ndio maana hata TRA imeweza kutoa taarifa zake kwa bodi ya wahasibu na wakaguzi wa mahesabu (NBAA).

“Ni muhimu na walipakodi wasimame katika nafasi yao, walipe kodi inayostahili na sisi tukiwa kama chombo kinachosimamia ukusanyaji wa kodi basi tunawaahidi kutoa huduma inayostahili waweze kulipa kodi sawasawa.” amesema Naibu Kamishna Manyama

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Mheshimiwa Jamali Kassim Ali ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema.

“Kwa mujibu wa Sheria, vigezo vyetu vya ndani na vile vya Kimataifa ili kufanya hesabu zetu ziwe na ubora na watumiaji wake waweze kuzitumia na kufanya maamuzi yaliyosahihi, hilo ndio jambo kubwa ambalo ningependa kuwaasa viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali na zile za binafsi”

“Kusema ukweli na hata ukiangalia kwa mujibu wa idadi ya washiriki wa kila kipengele ni kubwa kwaiyo hata mchujo uliofanyika kumpata wa kwanza wa pili na watatu inaonyesha kwamba haw a wote itakuwa ni tofauti ndogo ndogo, jambo kubwa kama alivyoeleza Mkurugenzi wa NBAA kwamba watatoa repoti kwa washiriki wote kuonesha namna gani walitahiniwa kwa wale wa kwanza walipata alama gani, wapi zilionekana ni dosari.” Hata hivyo amebainisha kuwa.

Mheshimiwa Jamali Kassim Ali ameongeza kuwa, anaamini hii itakuwa ni chachu kwa wao kuhakikisha wanakaa katika maeneo yale hesabu zao zinaonekana zina dosari kuona namna gani kwa mwaka unaofuatia kuhakikisha zile dosari zote wanazirekebisha na kuwa na hesabu bora zaidi.

Pamoja na kutoa tuzo kwa washindi, Bodi ya Taifa ya wahasibu na wakaguzi wa hesabu imeadhimishamiaka 50 tangu kuundwa kwa bodi hiyo ambapo shughuli mbalimbali kama vile makongamano na maonesho yalifanyika katika ukumbi wa APC Bunju jijini Dar es Saalaam.