Uboreshaji bandari unahitaji uwekezaji

Na Stella Aron,JamhuriMedia

NI lini Tanzania itaandika historia yake kwa kujiweka imara na kukuza uchumi kupitia biashara iliyoongezeka, kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni na kutengeneza ajira kupitia bandari ya Dar es Salaaam.

Kuna maswali mengi ambayo hukosa majibu kwa kuwa Tanzania ina fursa nyingi zitokazo na bandari lakini fursa hizo huishia sakafuni kwa kuwa hakuna mbinu wala juhudi zinazofanyika ili kupatikana kwa fursa hizo ambazo zingechangia kupaisha uchumi.

Pamoja na Tanzania kuzungukwa na nchi nane lakini bado hakuna mikakati ya kuhakikisha kuwa hakuna bidhaa inayopitishwa katika bendari kuelekea nchini nyingine na kukosa mapato.

Makontena ya nchi nyingine sasa yanapitia Bandari ya Dar es Salaam yanakwenda nchi nyingine
kwa mtazamo huo unachangia kushindwa kuchangia bajeti ya taifa ambapo kama kungekuwa na usimamizi dhabiti taifa lingepata faida kubwa kutokana na bandari.

Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika kupitia banadari ya Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan, Julai 4, 2022, alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Plasduce Mbossa ambaye alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo.

Rais Samia aliagiza TPA iwe na ufanisi zaidi na jitihada za uongozi mpya wa TPA chini ya Plasduce Mbossa kwa kuongeza ufanisi kwenye bandari zetu.

Rais Samia alisema wazi kuwa haridhidhwi na kasi ya utendaji wa bandari na kuwataka watendaji wa mamlaka hiyo kuchapa kazi kwani bado tuna suasua wawekezaji wanakuja na kuzungushwa mwanzo mwisho.

“Siasa zilizopo, longolongo zilizopo, watu huko nje mabandari yanaendeshwa kwa kasi kubwa, yanaendeshwa kwa operation na biashara zinakua kwa kasi kubwa kupitia bandari.. sisi bado tunasuasua.

Moja ya eneo la makontena katika bandari zinazoendeshwa na DP World, Falme za Kiarabu (UAE)

“Tunasuasua. Wawekezaji wanakuja ni kuzungushwa mwanzo mwisho, tutizame siasa, tutizame uchumi .. sijui tutizame maendeleo ya kitu gani.. nasema bandari watu wafanye kazi.. tutatupia jicho vizuri. Wale waliokabidhiwa bandari nataka tuelewane vizuri.

“Bandari ya bandari ndio jicho letu. Bandari hii ikifanya vizuri, nusu ya bajeti tunayoipanga kila mwaka itatolewa ndani ya bandari ya Dar.. lakini kama tutajipanga kufanya kazi… lakini kama tunakwenda na longolongo lengo hatutalifikia kwa hiyo wale wa bandari niwaombe twende tukafanye kazi kwa kasi kubwa,” anasema Rais Samia.

Wakati Tanzania ikiendelea kujipanga,tayari wenzetu katika baadhi ya nchi mfano ni bandari ya Rwanda, Senegal, Somalilanda zinanufaika kiuchumi baada ya kuingia ubia Kampuni ya DP World.

Kampuni hii inaendesha Bandari tatu ambazo ni Jebel Ali, Mina Rashid na Al Hamriyah ambazo ziko kati ya umbali wa kilomita nane (8) na 46 kutoka Bandari moja hadi nyingine na kuleta manufaa makubwa hivyi hata Tanzania inaweza ikanufaika kwa uwekezaji kupitia Kampuni ya DP World kutoka Falme za Kiarabu.

Mradi wa Bandari ya Ndayane nchini Senegal ndio uwekezaji mkubwa zaidi wa bandari wa DP World katika bara la Afrika hadi sasa, na uwekezaji mkubwa zaidi wa kibinafsi katika historia ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mradi wa Bandari ya Ndayane utatekelezwa kwa awamu mbili, ya kwanza ambayo unagharimu Dola za Marekani milioni 837 ikichangiwa na DP World Dakar SA, ubia kati ya DP World na Bandari ya Dakar (PAD), inajumuisha uundaji wa kituo cha kontena chenye ukubwa wa hekta 300, chaneli ya bahari ya kilomita 5, na ujenzi wa gati yenye urefu wa m 840 kina cha mita 18 yenye ukubwa wa kuchukua meli za baada ya Panamax na 366m.

Rais wa Somaliland Muse Bihi Abdi, alikaririwa akisema kuwa ubia wa DP World na Somaliland ni wakati wa kujivunia na wa kihistoria kwa Somaliland na watu wake, kwani kukamilika kwa awamu ya kwanza kumefanya maono yetu ya kuanzisha Berbera na eneo lake la kimkakati kuwa kitovu kikuu cha biashara katika mkoa huo kuwa ukweli.

“Pamoja na kituo kipya, pamoja na awamu ya pili ya upanuzi na ukanda wa uchumi kando ya ukanda wa Berbera, sasa tumejiweka imara kukuza na kukuza uchumi wetu kupitia biashara iliyoongezeka, kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni na kutengeneza ajira, “anasema Muse Bihi Abdi.

Kampuni binafsi ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzani (TICTS),imefanyakazi zaidi ya miaka 22 ambapo kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa madereva kuhusiana na utendajikazi ambao wanadai ulikuwa chini ya kiwango na kuchangia kuwepo kwa mrundikano wa makontena bandarini.

TICTS imefanyakazi kwa miaka 22 hivyo kuisha kwa mkataba TICTS kunaweza kukawa fursa ya kuleta mageuzi chanya katika bandari Dar es Salaam kwani ilichangia baadhi ya wateja kukimbilia kwenye bandari nyingine za Afrika.

Hata hivyo TPA kumalizana na TICTS iliyohudumu bandarini kwa miaka 22 imetokana na kufikia ukomo wa mkataba wa miaka mitano waliosaini Julai, 2017, pia ni kutoafikiana katika majadiliano ya kuongeza muda wa huduma.

Mkataba kati ya TPA na TICTS ulikoma Septemba 30, mwaka huu na kabla ya hatua hiyo, vilifanyika vikao kadhaa kuuhuisha bila mafanikio.

Ili kuleta ufanisi zaidi katika kitengo hicho kama Tanzania ikipata mwekezaji mpya kama Dubai World anaweza kuleta mageuzi makubwa kwenye uchumi nchini.

Mfano mzuri nchi ya Singapore kwa miaka 50 iliyopita, hali ya mji wa Singapore ilikuwa nchi isiyo na maendeleo na Pato la Taifa kwa kila mtu chini ya dola 320. Leo, ni moja ya uchumi wa kasi zaidi duniani. Pato la Taifa kwa kila mtu limeongezeka kwa dola za Kimarekani 60,000 za Marekani, na kuifanya kuwa ya juu zaidi ya sita duniani kwa takwimu za Shirikisho la Intelligence Agency. Kwa nchi ambayo haina eneo na rasilimali za asili, kupaa kwa uchumi wa Singapore ni kitu cha ajabu sana.

Makamu wa Rais Philip Mpango akiwa nchini humo wakati akihudhuria mkutano wa kimataiga wa Jukwaa la Majadiliano ya Kiuchumi ‘The Bloomberg New Economy Forum’ alitumia fursa hiyo kukutana na Naibu Waziri Mkuu wa Singapore Heng Swee Keat.

Katika mazungumzo hayo Waziri Mkuu wa Singapore alimuelezea jinsi nchi hiyo ilivyofaidika kiuchumi kupitia shughuli za bandari kubwa ya Singapore ambayo ndiyo imechangia kwa sehemu kubwa kuifanya nchi hiyo kuwa tajiri.

Bandari ya Singapore inapokea na kuhudumia meli 400 kwa mpigo katika siku moja na hivyo ni mojawapo ya bandari kubwa kibiashara duniani .Asilimia 90 ya biashara ya kimataifa mizigo yake yote inatumia huduma za meli na bandari.

Ni wakati sasa kwa Tanzania kuingia ubia na kampuni ya Kampuni ya DP World ili kupata mafanikio hivyo kama Tanzania inahitaji kujipanua zaidi na kuwa mshirika mkubwa wa huduma ya meli na bandari kwa ukanda wa Afrika ya Mashariki na nchi za maziwa makuu huku pia ujenzi wa bandari kubwa Bagamoyo, utaifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya huduma za bandari duniani.

Bandari ya Dar es Salaam

Tanzania ikipata mwekezaji mpya kama Dubai World anaweza kuleta mageuzi makubwa kwenye uchumi nchini na bandari ya Dar es Salaam kitovu cha biashara na usafirishaji cha Afrika.

Ni vizuri tukajifunza kwa wenzetu kwani Dubai ina bandari tatu zilizo karibu ambazo ni Jebel Ali, Mina Rashid na Al Hamriyah zote zikiwa chini ya DP World ambazo zote zinafanya kazi kwa kushirikiana (complementing each other) .

Kutokana na ujenzi huo kumekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi na kwa kampuni pia itasaidia kuondoa hofu ya kutojenga bandari mpya Bagamoyo kwa imani kuwa itakua karibu na bandari ya Dar na kuleta ushindani jambo ambalo haliusiani.

Hata hivyo katika bandari hizo tatu, kuna mitambo mikubwa ya kushusha na kupakia kontena milioni 22, hivyo kupitia DP World kwa sasa wanaendelea na mradi wanaotaraji kuukamilisha mwakani.

Kwamba mteja akiwa na kontena lake, hatalazimika kusubiri ‘winch’ ipangue makontena matano kufikia kontena lake la chini.

Uzoefu wa utendajikazi kwa kampuni ya DP World umezidi kuchochea teknolojia ambapo katika bandari hizo zilizojaa makontena hakuna foleni ya upakiaji kama ilivyo katika bandari ya Dar es Salaam ambapo mteja anaweza akasubiri kwa zaidi saa 12 kwa kazi ya kupakiliwa mzigo.

Katika bandari za DP World kontena zitakuwa zinapangwa kwenye chanja (shelves) ambazo ukibonyeza kifungo (button) na kuweka namba ya kontena husika, hata kama litakuwa katikati ya kontena 30,000 litajichomoa na kutoka nje.

Teknolojia hiyo kama ifika Tanzania si kusaidia kupunguza makontena tu bali hata kuchochea uchumi kwani wateja wamekuwa wakiilalamikia TICTS kwa kushindwa kufanyakazi ipasavyo na kutokuwepo kwa jitihada za kupunguza msongamano wa foleni.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),Plasduce Mbossa, alifichua siri kuwa mamlaka hiyo ina mpango wa kuongeza uwezo wa bandari za Dar es Salaam, Tanga, na Mtwara ili kuweza kuhudumia tani 27.5 za mizigo ifikapo mwaka wa fedha 2024/2025.

Mbossa anasema kuwa Serikali inatekeleza miradi tofauti kwenye bandari zilizopo na mpya ili kuongeza uwezo kabla ya mahitaji. Miongoni mwao ni kuboresha utunzaji wa mizigo katika bandari hizo tatu. Miradi mingine ni ujenzi wa bandari za Bagamoyo mkoani Pwani, Chongoleani mkoani Tanga, na Kisiwa-Mgao mkoani Mtwara.

“Wazo ni kuongeza uwezo wa bandari zetu na kuwa na ushindani katika ukanda wa Afrika mashariki na kati,” Mbossa anasema.

Mipango ya TPA ni ya kupongezwa lakini inaweza tu kutekelezwa kwa kuleta washughulikiaji wabunifu na wabunifu wa makontena ya mizigo wenye uzoefu na utaalam kama ule wa DP World, ambao utendakazi wake hauna shaka kote ulimwengu.