Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Wadau wa uhifadhi nchini wametakiwa kuhakikisha kuwa mnyama Kakakuona analindwa na kutunzwa kwani yupo hatarini kutoweka.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Tanzania Research Conservation Organization (TRCO) kuanzia mwaka 2022 hadi 2024 umesema mnyama huyo anakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uwindaji haramu, biashara haramu, mila na desturi potofu pamoja na uharibifu wa mazingira.

Akizungumza na wadau wa uhifadhi kutoka katika shoroba ya Kwakuchinja, Mratibu wa Mradi wa kuhifadhi Kakakuona shoroba ya Kwakichinja ambaye pia ni Meneja rasilimali watu na utawala na mmoja wa waanzilishi wa shirika hilo, Elisante Kimambo amesema baadhi ya jamii imekuwa na imani potofu ya kutumia viungo vya mnyama huyo kwa ajili ya kukuza biashara, kuondoa nuksi, dawa pamoja na urembo.

Mafunzo ya kukuza uelewa kuhusu biolojia, ikolojia na uhifadhi wa kakakuona kwa wakazi wa kijiji cha Kwemtindi (Picha Kwa hisani ya TRCO)

Kimambo amesema malengo ya utafiti huo ni kutathmini matukio na maeneo anayookena kakakuona katika shoroba za kwakuchinja, Nyerere-Selous-Udzungwa na Amani-Nilo pamoja na kuwajengea na kuimarisha uwezo wa wadau katika kumlinda.

“Malengo mengine ya utafiti huu ni kubaini mtandao, njia na aina ya biashara kuhusiana na mnyama huyu kwa maana ya viungo na hata mwili mzima ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu faida za utunzaji wa ikolojia, bioanuai na uhifadhi.

“Aidha tumelenga kuiwezesha na kushirikisha jamii kuhusu utafiti wa ikolojia, usimamizi wa rasilimali zilizopo, lakini pia kuishirikisha jamii kuhusu tabianchi na athari zake kwa uhifadhi wa bionuai na kuongeza kipato kwa jamii zinazozunguka shoroba hizo tatu” amesema.

Amesema ushoroba ni sehemu muhimu ya makazi, mazalia na mapitio ya wanyamapori na utafiti huo umeelezea umuhimu wa shoroba hizo kuwa zinasaidia kutunza bionuai na kuunganisha maeneo ya wanyamapori yaliyotengana, kupunguza migogoro kati ya binadamu wanyamapori pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji.

Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu huo, mnyama Kakakuona ambaye hana madhara kwa binadamu hupendelea kuishi maeneo tulivu, yenye maji ya kutosha hivyo ni muhimu kwa jamii kulinda ikolojia yake ili aweze kutafuta chakula, maji na mazalia kwa ajili ya uendelevu wake.

Mkurugenzi Msaidizi wa TRCO Nyemo Chilagane aliyembeba Kakakuona wakati wa kukusanya data za msingi kutoka kwa jamii baada ya kumuokoa mnyama huyo katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, iliyoko katika kijiji cha Mahuninga. (Picha kwa hisani ya Simon Chidodo)

Kwa upande wake Mtafiti Msaidizi kutoka shirika hilo Leon Hermenegild amesema lengo mahsusi la utafiti huo ni kuweka mazingira mazuri ya kumuokoa mnyama kakakuona ili kuendelea kuishi na kuzaliana na kuitaka jamii kutoa taarifa kwa mamlaka husika iwapo watamuona kakakuona eneo ambalo siyo makazi yake ya asili.

“Iwapo kakakuona akionekana sehemu ambayo siyo makazi yake, kwanza mamlaka ipewe taarifa kwa maana ya viongozi wa kijiji au halmshauri, lakini pia awekwe sehemu tulivu kwani hapendi kelele, lakini muda wa kumuachia inatakiwa iwe usiku kwani hutafuta malisho yake nyakati za usiku” amesema Hermenegild na kuongeza

“Lakini eneo la kumwachia lazima lifanane na mazingira yake ya asili lenye mashimo na vichuguu kwa ajili ya kupata malisho yake ya wadudu, lisiwe eneo lenye vihatarishi vya ujangili lakini baada ya kumuachia kuwe na ufuatiliaji” amesisitiza Hermenegild.

Wadau wa uhifadhi wakifuatilia uwasilishaji wa utafiti juu ya kakakuona uliofanywa na Shirika la Tanzania Research and Conservation Organizations (TRCO)

Akichangia katika uwasilishaji huo, mwanaikolojia kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara Halima Kiwango amelishauri shirika hilo kutoa elimu kwa jamii inayoishi jirani ya hifadhi kubadili changamoto zinazosababishwa na wananchi dhidi ya Kakakuona kuwa fursa.

Ameshauri itumie njia rafiki katika kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii na siyo kutumia ubabe au kuwabugudhi kwa kuwa wananchi ni waelewa iwapo watasikilizwa na kushirikishwa kikamilifu.

“Kwa mfano hao waganga wa kienyeji ambao wanatumia mazao ya kakakuona kama tiba nao washirikishwe, waulizwe ni kwa namna gani kakakuona anatibu, mwisho muwape elimu yenye majibu kwa maana ya mbadala wa dawa hizo, nina uhakika wakielewa wataacha kutumia mazao ya kakakuona na watatumia tiba sahihi” amesema Kiwango.

By Jamhuri