Kwa muda mrefu nchini Tanzania tumekuwa na Wizara ya Elimu ambayo haikusimamia elimu kwa ufanisi. Badala yake tumekuwa na viongozi watendaji wa wizara hiyo ambao wamekuwa wakiweka mbele maslahi yao binafsi. Wakajipatia asilimia kumi kutoka kwa wachapishaji wa vitabu kwa kuruhusu vitabu vibovu kuingia mashuleni.

Juu ya yote, viongozi na watendaji wa Wizara ya Elimu hawakujali maoni ya wadau wa elimu. Waligeuza elimu kuwa suala lao binafsi. Wakaendesha masuala ya elimu kwa ujeuri na ukaidi usio wa kawaida. Matokeo yake yakawa kuporomoka kwa elimu nchini kunakoendelea kushuhudiwa.

Hali hiyo mbaya haikuwapo wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Mwalimu Nyerere. Mwalimu Nyerere aliweka mbele masuala ya elimu tofauti na kiongozi wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah, aliyeweka mbele masuala ya uchumi.

Serikali ya Mwalimu Nyerere ilishughulikia masuala ya elimu kikamilifu na kwa ufanisi mkubwa. Vikao vya chama cha TANU kisha CCM wakati wa Mwalimu Nyerere, havikuishia kuzungumzia tu masuala ya siasa, vilizungumzia pia masuala muhimu ya Taifa kama elimu, maji, ajira na kadhalika.

Kwa upande wa elimu, ilikuwa Serikali ya Madaraka iliyoongozwa na Mwalimu Nyerere iliyoamua mwaka 1960 kujenga chuo kikuu Tanganyika – Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikafunguliwa Oktoba 25, 1961.

Mwaka 1967 chama cha TANU kilipitisha Azimio la Arusha. Pamoja na Azimio la Arusha kuleta sera ya elimu ya kujitegemea, pia elimu ilitolewa bure.

Mwaka 1970 ulitangazwa kuwa Mwaka wa Elimu ya Watu Wazima Tanzania, watu wazima wakajua kusoma na kuandika. Mwaka 1974 chama cha TANU kilipitisha Azimio la Musoma lililohusisha mpango wa elimu kwa watu wote, ulioanza kutekelezwa mwaka 1977.

Mwaka 1975 ilianzishwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. Elimu ya watu wazima ikaimarishwa.

Mwaka 1980 Serikali ya Mwalimu Nyerere ilisikia malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba elimu ilikuwa imeshuka. Mwalimu Nyerere hakupuuza malalamiko hayo, akaunda tume iliyochunguza mwenendo wa elimu nchini. Tume hiyo iliyoongozwa na Jackson Makwetta ikathibitisha kwamba elimu ilikuwa imeshuka, hatua zikachukuliwa kurekebisha mambo.

Miaka hii mambo ni tofauti kabisa, mfano mzuri ni somo la hisabati ambalo limeendelea kufanywa vibaya. Kadhalika, mtihani wa maarifa ya jamii. Nani ameunda tume kuchunguza changamoto hizo? Hakuna. Na hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukweli kwamba watoto wa wakubwa hawasomi shule za umma ambazo ni shule za watoto wa maskini.

Leo tuna Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk. John Magufuli. Serikali hii imeleta matumaini makubwa kwa wananchi, inaonesha kwamba inajali mambo. Ni mazingira hayo yanayotusukuma wananchi kutoa maoni yetu kuhusu hali ya elimu Tanzania ili elimu tunayotoa isiwe ya bure tu bali iwe pia bora.

Katika kuitazama upya elimu tunayotoa, nitataja baadhi ya kasoro zilizopo katika jitihada zetu za kutoa elimu.

Kwanza, kwa muda mrefu hatukuwajali walimu inavyostahili. Tumewasumbua kuhusu haki zao na maslahi yao. Kuna walimu wanapokea mshahara wa Sh. 300,000 kwa mwezi, kiasi ambacho ni posho ya mbunge ya siku moja. Kuna walimu wamepandishwa madaraja lakini hawapewi mishahara inayoendana na madaraja yao. Kisha kuna walimu ambao hawajahudhuria semina yoyote tangu walipoanza kufundisha.

Serikali ya Awamu ya Tano izitake halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya semina za walimu. Vile vile, wakaguzi wa shule wasikague masomo ambayo hawakuyafanyia semina.

Pili, elimu tunayotoa ni utitiri wa vitabu vilivyopo mashuleni kwa somo moja, kwa darasa moja. Kila mwandishi ameandika kivyake, na mara nyingi upotofu. Utitiri huu wa vitabu umevuruga sana elimu na umewachanganya sana walimu na wanafunzi wao. Hivi hao wanaotunga mtihani wanatumia kitabu kipi kwa somo moja?

Tutazame upya pia masomo ya uraia, historia na jiografia kadhalika na mitihani ya masomo hayo. Masomo haya yanategemewa kuwajengea uzalendo vijana wetu, lakini mtihani wa maarifa ya jamii unaochanganya masomo hayo ni mtihani unaofanywa vibaya kila mwaka. Sababu kubwa ni kwamba Serikali haijaona umuhimu wa masomo hayo.

Wakati masomo mengine yametengewa vipindi vitano mpaka sita kwa juma, masomo ya uraia na historia yametengewa vipindi viwili viwili na kwa kuwa ukubwa wa vitabu kwa masomo yote unafanana, walimu wa historia na uraia wamelazimika kufundisha mambo juu juu ili kumaliza kitabu.

Halafu, katika mtihani wa Taifa masomo mengine mwanafunzi hupimwa kwa kuulizwa maswali hamsini kila somo, lakini katika masomo ya uraia, historia huulizwa maswali hamsini kwa pamoja katika mtihani wa maarifa ya jamii.

Kwa nini masomo hayo yasijitegemee kwenye mtihani kama masomo mengine? Wabunge walitaka somo la maarifa ya jamii lifutwe, likafutwa! Kwa nini Serikali inaendeleza mtihani wa somo lililofutwa? Huko si kuendeleza somo lenyewe.

Mwisho, kuna somo la stadi za kazi lililoanzishwa siku nyingi kwa lengo la kuwasaidia kujiajiri wanafunzi wanaorudi majumbani baada ya kumaliza shule ya msingi. Somo hili halijamsaidia mwanafunzi yeyote kujiajiri kwa sababu linafundishwa bila vifaa na linafundishwa na walimu ambao hawakupewa mafunzo yoyote.

Nitazungumzia somo hili kikamilifu katika toleo lijalo la gazeti hili.

1763 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!