Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kilianzishwa kwa sheria ya Bunge namba 405 ya mwaka 1998. Miongoni mwa majukumu ya chuo ni kutoa mafunzo ya sheria ya ndani na ya kimataifa( local and international training) kama itakavyokuwa imeelekezwa na Baraza la Uongozi wa Chuo.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999, Chuo cha Mahakama kimekuwa kikitoa kozi ya cheti cha sheria na astashahada ya sheria. Kimeweza kutoa wahitimu wengi ambao wameajiriwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama wamekuwa kwa muda mrefu kimbilio la waajiri- wa umma au sekta binafsi.

Mchango wa Chuo cha Mahakama kwa mfano, katika kupunguza upungufu wa mahakimu uliokuwa ukizikabili Mahakama za Mwanzo nchi hauwezi kupuuzwa hata kidogo. Kwa sasa kutokana na mabadiliko ya muundo wa utumishi wa mahakimu wa mahakama za mwanzo, chuo sasa kinazalisha wahitimu ambao huajiriwa zaidi kama makarani katika ofisi mbalimbali na watendaji wa vijiji na maeneo mengine, lakini si mahakamani tena.

Chuo kinapaswa kujikita katika kutoa mafunzo endelevu ya kimahakama kwa watumishi wa mhimili huu wa dola. (si lengo la makala hii kujadili haya).

Chuo cha Uongozi wa Mahakama kama vilivyo vyuo vingine nchini vya kati (tertiary institutions) kiko chini ya mamlaka ya udhibiti (regulatory authority) ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Mamlaka hii hutoa miongozo ya namna ya kuendesha shughuli za kitaaluma na uendeshaji wa vyuo vilivyo chini yake. Ni lazima kwa taasisi zilizo chini yake kukidhi matakwa ya kisheria na kikanuni yanayotolewa na Baraza hilo. Kwa mfano, ili chuo kiweze kutoa mafunzo ni lazima kipate ithibati, ni lazima pia kwa chuo kitoe mafunzo kwa kujikita kwenye mitaala ya umahiri (Competence Based Training). Chuo cha Uongozi wa Mahakama kimepata ithibati na tayari kimeanza kutoa mafunzo yake kwa kufuata mitaala ya umahiri japo kwa kuchelewa.

Wakati hayo yakiwa yamefanyiwa kazi bado kuna suala moja kubwa ambalo Baraza limefumbia macho kwa muda mrefu na kuleta hisia kuwa Baraza huenda linakiogopa Chuo cha Mahakama. Hii inaweza kusababishwa na Chuo kuongozwa na watu wanaotoka Mahakama hasa majaji wa Mahakama Kuu watu ambao huogopwa- na kwa kweli wengine huishi kama miungu watu hapa duniani. Na kama chuo hakiogopwi, kigugumizi cha kutekeleza kanuni zake kinatokana na nini? Kisa cha kuibua maswali haya kunatokana na hili ninaloeleza hapa chini.

Tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Mahakama, kimekuwa chini ya wakuu watatu wa chuo kwa vipindi tofauti tofauti -kila kipindi kikiwa na changamoto zake. Mkuu wa chuo wa kwanza alikuwa Mheshimiwa Emilian Mushi- kipindi hicho alikuwa hakimu. Aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na kuhamishiwa Dar es Salaam. Baadaye akiwa tayari ni Jaji alirudishwa tena chuoni na kuendelea na ukuu wa chuo. Baadaye alihamishiwa Dar es Salaam na akaletwa Mheshimiwa Jaji Aloysius Mujulizi kuongoza Chuo cha Mahakama.

Baada ya miaka kadhaa ya utumishi alipewa majukumu mengine na Rais na nafasi yake ikachukuliwa na Mheshimiwa Jaji Ferdinand Wambali ambaye yupo hadi ninapoandika makala hii.

Kwa mujibu wa sheria inayoanzisha Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Mkuu wa Chuo huteuliwa na Rais baada ya kushauriana na Jaji Mkuu baada ya Jaji Mkuu kuwa amepokea mapendekezo kutoka Baraza la Uongozi wa Chuo. Sharti hilo linabainishwa katika kifungu cha 10(1) cha Sheria namba 405.

Wakati huo ndio ukiwa utaratibu wa kumpata mkuu wa chuo kwa mujibu wa sheria, sheria hiyo haijaweka kiwango cha elimu anachostahili kuwa nacho mtu huyo. Hivyo basi, ujaji umekuwa ni sifa kubwa japo haijabainishwa na sheria.

Ikiwa sheria inayoanzisha chuo haijaweka kigezo cha elimu, ni lazima anayependekeza na anayeteua kujiridhisha kama vigezo vilivyowekwa na NACTE anayepaswa kuteuliwa amevikidhi. Baraza katika mwongozo wake limeweka bayana kuwa mkuu wa chuo atakuwa mtu mwenye sifa ya elimu ya shahada ya uzamivu, aliye na uzoefu wa kutosha wa masuala ya utawala na taaluma.

Sifa hizi zimekuwa hazitoshi kwa wakuu wote wa chuo waliopita na aliyepo. Wakuu hawa wana sifa zao mbalimbali, lakini hawafikii vigezo vya kitaaluma vilivyowekwa na NACTE ambavyo vinapasika kufuatwa mara maelekezo hayo yanapotolewa.

Swali la kujiuliza ni je, Mahakama ya Tanzania haina majaji wenye fisa toshelezi kuweza kuongoza chuo? Ukweli ni kwamba wapo, tena wengi. Wapo majaji wenye u-profesa na wapo wenye shahada za uzamivu na ambao walikuwa walimu katika taasisi mbalimbali za elimu nchini. Na kama ni hivyo basi, kwanini ateuliwe mtu asiyefikia viwango kuwa mkuu wa chuo hali wenye sifa wapo? Ni wazi katika hili NACTE imeshindwa kutekeleza sehemu ya majukumu yake na haiwezi kukwepa lawama.

Na si kwa mkuu wa chuo tu, bali hata wasaidizi wake hawana sifa toshelezi na hii imesababisha wasaidizi hao kuwa kina ‘ndiyo mzee’ kwa mkuu wao ambaye ndiye kimsingi anayewapendekeza kwenye Baraza la Uongozi wa Chuo kushika hizo nyadhifa. Sababu ya kuwa hivyo ni moja tu kuwa wamepewa madaraka wasiyostahili kwa kukosa sifa. Hali hii si afya kwa ustawi wa taasisi na taifa.

Kigezo hiki kinazidi kuonekana muhimu ukizingatia hali ya Chuo cha Mahakama kwa sasa. Wadau wa chuo wanaona umuhimu wa kuwa na mkuu mwenye sifa toshelezi anayefahamu utamaduni wa kuendesha taasisi ya elimu tofauti na unavyoendesha mahakama (academic culture). Leo hii katika kipindi cha utawala ambao mtu hawezi kuuita uongozi wa Mheshimiwa Jaji Wambali, chuo kimepoteza mvuto ndani na nje ya Lushoto. Si chuo tena kilichokuwa kikikimbiliwa na wanafunzi na wazazi wengi kutaka watoto wao wasome hapo.

Ukizungumza na watumishi wa chuo unaona wamekatishwa tamaa, wahadhiri wamekatishwa tamaa zaidi. Hawana ari ya kufanya chochote. Wengi wanafundisha kutimiza wajibu.

Morali ya waalimu na watumishi ipo chini. Jaji Mkuu hajui wala Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Jaji Mstaafu Mrosso hajui. Leo ukiuliza menejimenti ya chuo imekaa lini na inakaa mara ngapi kwa mwaka tangu Mheshimiwa Jaji Wambali aje chuoni, utashangaa! Huitisha vikao anapotaka yeye na kwa muda anaotaka yeye kwa mambo anayoyataka yeye. Hii ni sawa na kuendesha taasisi kama kitu binafsi.

Lakini jingine kubwa ni kwa mheshimiwa kukaa ofisini kwa muda mfupi sana. Kila uchao ni safari, safari na yeye. Inawezekana Mahakama inamtumia sana. Kama ni hivyo ingekuwa busara kuleta mkuu mwingine wa chuo ili kimtumie vizuri zaidi. Kwa mtindo huu lazima kuwe na udhaifu katika uendeshaji wa chuo.

Ukiachilia mbali hayo, kuna mambo kadhaa ambayo yamekatisha watumishi tamaa ya kukitumikia chuo kama walivyokuwa wakifanya hapo awali. Watumishi wengi wanafikiria na wamejaribu kutaka kuhama, lakini wanadhibitiwa kwa barua zao kutopitishwa. Wengine wamehama kwa mbinde na wengine wameacha kazi na kwenda maeneo mengine kwa sababu mbalimbali.

Miongoni mwa vilivyowakatisha tamaa ni kuona mtu anakaa kwenye taassisi isiyokua, imedumaa, haileti changamoto ya ubongo na utendaji. Watu wanataka kubadili upepo kupata mawazo mapya.

Kwa mfano, jambo moja lililokatisha tamaa wengi ni kwa kufungwa kwa Tawi la Mwanza. Ufunguzi wa tawi hilo ulitoa picha ya chuo kukua. Tawi la Mwanza lilianzishwa kwa maelekezo ya Baraza la Uongozi wa Chuo. Na kwa bahati nzuri lilianzishwa wakati Mwenyekiti wa Baraza la Chuo akiwa ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Mohamed Chande.

Baraza la Uongozi wa Chuo lilifanya hayo kutekeleza sheria. Kifungu cha 5(2) cha Sheria inayoanzisha chuo kinalipa Baraza la Chuo uwezo wa kufungua matawi nchini. Ni wazi uanzishwaji wowote wa kitu kipya haukosi changamoto, lakini sishawishiki kuamini kuwa kufunga tawi ndilo suluhisho la kupambana na changamoto. Lakini swali jingine muhimu ni je, nani ana mamlaka ya kufunga tawi? Je, Baraza liliridhia ufungwaji wa tawi hilo? Na kama halikuridhia, limechukua hatua gani? Na kama halijachukua hatua, linastahili kuwapo? Kufungwa kwa Tawi la Mwanza ni sawa na kupiga hatua 10 mbele na mtu akurudishe hatua tisa au 10 kabisa nyuma. Haiwezekani kuwa ulikuwa uamuzi wa kukurupuka kama ambavyo watu wanavyotaka kuiaminisha dunia. Sijui hata Jaji Mkuu anajisikiaje kufungwa tawi alilosimamia uanzishwaji wake.

Jingine linalokatisha tamaa watumishi ni kwa Mkuu wa Chuo kuuweka kando mchakato wa kuanzisha digrii ya sheria na kozi nyingine zinazoweza kusaidia utendaji wa Mahakama na taifa. Mchakato huu ungemkuta mkuu wa chuo mwenye mtazamo wa kitaaluma na mwenye sifa toshelezi angeusukuma kwa nguvu zote. Yawezekana mchakato huu umewekwa pembeni kwa sababu chuo kinavyokuwa ndio hitaji la kuwa na mkuu wa taasisi mwenye sifa toshelezi linavyoongezeka.

Ikumbukwe wakati wa mahafali ya miaka 10 Rais Jakaya Kikwete (mstaafu) aliunga mkono uanzishwaji wa shahada ya sheria na nyinginezo, lakini akatoa angalizo la kutofuta mafunzo yaliyopo kwa kuwa ni muhimu mno kwa taifa. Tunapoelekea mwaka wa 15 tangu chuo kianzishwe hakuna cha kujivunia kwani kukua kwa chuo si uwepo wa majengo, bali mafunzo yanayokidhi vigezo.

Leo tawi limefungwa wadau wamekaa kimya hakuna anayehoji. Wanaogopa kumhoji Jaji, mchakato wa kuanzisha programu mbalimbali umegota au umesitishwa japo vyote vimetumia mamilioni ya fedha za walipa kodi achilia mbali kupunguzwa kwa wanachuo hali ambayo imewaacha wananchi wa Lushoto katika mazingira magumu.

Wananchi walikopa na kujenga nyumba kwa ajili ya makazi ya wanachuo kutokana na ongezeko lao mwaka hadi mwaka. Hili si jambo la kupuuza kwani linafanya uhusiano kati ya taasisi na wananchi kuwa mbaya.

Mwisho, mamlaka zinazohusika zifuatilie hali inavyoendelea Chuo cha Mahakama. Ni muhimu NACTE kuchukua hatua kwa kusimamia vigezo si kwa Chuo cha Mahakama pekee, bali vyuo vyote vilivyo chini yake.

Jaji Mkuu achukue hatua stahiki ili kukinusuru chuo na kufuata miongozo ya NACTE kabla ya kupeleka jina kwa rais ambaye ndiye mamlaka ya uteuzi wa mkuu wa chuo. Ikumbukwe kuwa Mahakama ni chombo cha kutafsiri sheria, hivyo ni lazima na chenyewe kifuate sheria, kanuni na miongozo. Ikifanya kinyume, watu au taasisi nyingine zitafanyaje?

Lakini zaidi ni muhimu kwa Kamati ya Bunge ya Sheria kukitembelea chuo kujionea hali halisi na kuhoji yaliyoibuliwa kwenye makala hii.

 

Mwandishi wa makala hii amejitambulishwa kuwa ni msomaji wa Gazeti la Jamhuri

3849 Total Views 2 Views Today
||||| 5 I Like It! |||||
Sambaza!