Habari nyingi siku hizi zinahusu vitimbi vya mfanyabiashara tajiri Mmarekani Donald Trump, katika kampeni zake za kuwania kuteuliwa mgombea urais kupitia chama cha Republican katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kwenye kampeni hizo kwa upande wa chama cha Democrat, mwanasiasa Bernie Sanders naye anazungumzwa kwa kupendelea kwake sera zinazoonekana kuwa za kijamaa. Kwa desturi za siasa za Marekani, kuhusishwa na ujamaa siyo sifa, ni doa.  

Ujamaa hauhusishwi na neema hata kidogo, unahusishwa na maovu tu ambayo serikali inaweza kuwatendea wananchi wake. Katika maana hii, hoja inabeba uzito zaidi iwapo ujamaa na ukomunisti unaunganishwa na kuwa kitu kimoja, ingawa zipo tofauti za msingi kati ya itikadi hizo mbili. 

Pamoja na mambo mengine serikali za kijamaa zinahusishwa na kunyima wananchi haki za kiraia na za kibinadamu, na huongozwa na watu wasioamini yupo Muumba, kwamba binadamu ni matokeo ya mlipuko wa kemikali ulioyotokea miaka 13 bilioni iliyopita. Leo hii, wakati nchi ya Venezuela inakabiliwa na ukame wa muda mrefu unaosababisha mgao wa umeme ambao hata Tanzania hatujapata kushuhudia, ni sera za kijamaa za serikali ya Venezuela zinazotajwa kuwa chanzo cha mgao huo.

Kama ilivyo katika nyanja ya siasa kote duniani, wapiga kura wengi wa nchini Marekani huamini zaidi wanayosikia kutoka kwa wanasiasa, vyombo vya habari, na wachambuzi wa masuala ya siasa kuliko kutafiti ukweli wao wenyewe. Kwa sababu hii, inatosha tu kumuita mtu mjamaa na kumpa sifa ya kutowatakia mema wapiga kura wake na hilo peke yake likampunguzia ushawishi kwa wapiga kura.

Lakini pamoja na kuwa hawapo wanasiasa wengi wa Marekani ambao wako tayari kuitwa Wajamaa, wapo viongozi wa Marekani ambao wametekeleza sera au kuchukua uamuzi ambao unafananishwa na ule unaoongoza serikali za kijamaa. Rais Franklin Roosevelt, aliyeongoza Marekani kati ya 1933 hadi 1945 alianzisha mpango kamambe wa ujenzi wa miundombinu uliojulikana kama New Deal na kuidhinisha serikali yake matumizi makubwa ya pesa yaliyoinua uchumi wa Marekani.

Na miradi kama hii haikuwa tu kwa marais wa chama cha Democratic ambao ndiyo kwa kawaida huhusishwa na sera za aina hii, yalitekelezwa pia na marais waliotokana na chama cha Republican. 

Rais Dwight D. Eisenhower, aliyeongoza kati ya mwaka 1953 na 1961 naye, pamoja na uamuzi mwngine, aliendeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara. Tukumbuke kuwa zipo nchi za kipebari ambako barabara hujengwa na kumlikiwa na kampuni binafsi ambazo hutoza waendesha magari kutumia barabara hizo.

Serikali zinazofuata sera za kibepari zinayo sifa ya kuweka mazingira mazuri na rahisi kwa wafanyabiashara na wenye viwanda. Benki ya Dunia huorodhesha nchi ambazo zinaongoza kwa sifa hizo na wawekezaji wasiotaka ufuatiliaji wa karibu wa serikali huelekeza mitaji yao huko. Lakini ni utawala wa Richard Nixon, Rais kati ya mwaka 1969 na 1974 ambao ulizindua kitengo cha kusimamia uhifadhi wa mazingira, pamoja na idara ya kulinda masilahi ya wafanyakazi. Ni ujamaa na ukomunisti ndio huhusishwa zaidi na kulinda masilahi ya wafanyakazi dhidi ya masilahi ya wamiliki wa biashara na viwanda.

Mifano hii machache, ni sehemu tu ya mifano mingi ya utekelezaji wa uamuzi ambao kimtazamo usingetegetarajiwa kufanywa na nchi ambayo wanasiasa wake huonya mara kwa mara juu ya maovu sera za ujamaa.

Mwaka 2009 serikali ya Rais Barack Obama ilipitisha sheria iliyojulikana kama American Recovery and Investment Act. Sheria hii iliidhinisha Serikali ya Marekani kutumia dola bilioni 831 za Marekani kwenye sekta za elimu, afya, miundombinu, na nishati mbadala ili kusaidia kuhuisha hali mbaya ya uchumi. 

Jambo moja la msingi linalotofautisha sera za kijamaa na zile za kibepari ni ule mwiko unaofuatwa na serikali za kibepari wa kuwekeza kwenye sekta za jamii, kama afya na elimu. Dini ya wahafidhina ni kila mtu na lwake. Kwa sheria hii, Rais Obama angestahili tuzo kutoka kwa vinara wa kutekeleza sera za kijamaa.

Lakini ili kuficha uhalisia wa sera zenyewe, uamuzi kama huu hupachikwa majina yanayoficha hali halisi. Matumizi kama haya kwa serikali za kijamaa yangeitwa ruzuku. Matumizi haya yamepachikwa jina la “kichocheo” na serikali ya Rais Obama, ili kuleta maana kwamba kichocheo ni jambo lenye nia njema wakati ruzuku inaleta maana ya matumizi ya kihasara-hasara tu. Neno ruzuku linahusishwa zaidi na ufujaji, au uwekezaji ambao hautoi faida yoyote. Msingi mkuu wa ubepari ni faida.

Ni kwa sababu ya doa hili ujamaa, Bernie Sanders amekuwa anafanya jitihada ya kufafanua aina ya ujamaa ambayo anaunga mkono, na atatekeleza akichaguliwa kuwa rais. Ni ujamaa ambao utazingatia demokrasia, na utajali masilahi ya watu. Ni ujamaa wa nchi za Skandinavia; na siyo ukomunisti wa Urusi ya zamani. Hata Sanders ambaye anaandamwa na wasiomuunga mkono kuwa anakusudia kuitumbukiza Marekani kwenye ujamaa iwapo atakuwa rais anaweka jitihada kubwa ya kubainisha kuwa ujamaa anaoshabikia ni ujamaa wenye kujali demokrasia na kuheshimu uhuru wa watu.

Sanders hana hofu sana kuwa kujiita mjamaa katika kampeni za sasa kutamharibia mbio zake za urais. Ukweli ni kuwa kwa sasa, ndani ya chama cha Democrat, kushabikia ujamaa kunalipa. Kwenye kura za maoni zilizotolewa na YouGuv hivi karibuni matokeo yanaonesha kuwa mwaka 2015 wapiga kura wengi wanaounga mkono chama cha Democrat wanakubali sera za kijamaa.

Labda nitakuwa nimetia chumvi kidogo kusema kuwa kwa mwanasiasa Mmarekani kuitwa mjamaa ni sawa na kutukanwa tusi la nguoni. Lakini ni kweli kuwa kuitwa hivyo hupunguza badala ya kuongeza sifa za mwanasiasa.

By Jamhuri