Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Tume ya Madini imefanikiwa kutoa jumla ya leseni za uchimbaji madini 9,642 kati ya leseni 9,174 zilizopangwa kutolewa na tume hiyo kwa mwaka wa fedha uliopita.

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo katika kipindi cha mwaka 2022/2023 na mikakati ya mwaka 2023/2024 ambapo amesema kuwa, ukuaji wa sekta hiyo umesaidia kuongeza mapato ya Serikali na kukua kwa mchango wa Sekta ya Madini nchini.

Mhandisi Lwamo ameeleza kuwa, Sekta ya Madini ni miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya kijamii na Taifa kwa ujumla ambapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta hiyo yametokana na uongozi imara wa Serikali chini ya uongozi makini wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Katika kuendelea kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini, Tume imefanikiwa kutoa jumla ya leseni za uchimbaji madini 9,642 ambazo zinajumuisha leseni za uchimbaji mkubwa, uchimbaji wa kati, uchimbaji mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini, na kati ya leseni zilizotolewa, leseni 6,511 sawa na asilimia 70.97 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo”, alisema Mhandisi Lwamo.

Ameongeza kuwa, kuongezeka kwa utoaji wa leseni hizo unadhihirisha azma ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wao katika sekta ya Madini.

Kwa upande mwingine, Tume ya Madini katika kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali madini, imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini pamoja na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23, jumla ya mipango 656 ya Ushirikishwaji wa Watanzania ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi na kati ya mipango iliyowasilishwa, 652 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa.” Alimalizia Mhandisi Lwamo.

By Jamhuri