Wiki iliyopita nilizungumza na wabunge wawili-Martha Mlata na Wiliam Ngeleja, kwa nyakati tofauti. Hawa ni miongoni mwa wabunge waliokuwa ziarani China.

Nilimwuliza, Mlata ni mambo gani yamemvutia baada ya kuiona China . Kabla ya kujibu, uso wake ulionesha namna alivyopata shida ya “aanze kuzungumza lipi”. Aanze kuzungumzia flyovers  alizoona, azungumzie kilimo au anieleze kuhusu uzalendo wa Wachina kwa Taifa lao.

Anasema aliwauliza siri ya mafanikio yao. Wakamjibu kwamba maendeleo yote yanayoonekana, ni matunda ya ujenzi wa uzalendo kwa wananchi wa China. Kwa maneno mengine ni kwamba kuithamini na kuitumikia China ndiyo dira ya maendeleo ya Taifa hilo. Maswali niliyomwuliza Mlata, ndiyo hayo hayo niliyomwuliza Ngeleja. Majibu niliyoyapata kwa Mlata, ndiyo hayo niliyoyapata kwa Ngeleja.

 

Nimejaribu kuyasema haya ili kuonesha athari tunazoweza kuzipata endapo hatutathamini na kuujenga uzalendo. Wanasiasa wetu ni nadra mno kuwasikia wakilizungumza suala la uzalendo kwa nguvu kubwa. Uzalendo unaozungumzwa sasa ni wa kurejeshwa kwa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Sawa, sibezi mafunzo haya. Waswahili walisema samaki mkunje akingali mbichi!

 

Kusubiri kijana aliyehitimu kidato cha sita au chuo kikuu ilikumfundisha uzalendo, ni kujaribu kumkunja samaki aliyekwishakauka. China wana Chipukizi. Huko ndiko watoto wanakopikwa na kuwafanya waamini kuwa wana wajibu kwa Taifa lao. Korea zote zina Chipukizi, ndiyo maana Korea Kaskazini, pamoja na kutengwa na ulimwengu, mapenzi kwa nchi yao yanazidi kuongezeka kila uchao.

 

Ujio wa siasa ya vyama vingi umekuwa na faida na hasara zake. Moja ya hasara kubwa kabisa ni kufutwa kwa mafunzo ya Chipukizi. Chipukizi ilikuwa ni zaidi ya gwaride na halaiki. Kupitia Chipukizi tulijifunza ukakamavu, lakini tulijengwa kwenye misingi ya uzalendo kwa kuimba nyimbo na kula viapo kwa utiifu kwa Taifa letu. Tuliimba nyimbo za kulisifu Taifa letu, kiasi cha kutufanya tuamini kuwa ni Tanzania pekee ambayo ilikuwa nchi nzuri miongoni mwa mataifa yote katika sayari hii. Tuliimba nyimbo za kuzisifu mbuga zetu za wanyamapori, Mlima Kilimanjaro, tuliimba nyimbo za kulaani ukandamizaji, tuliimba nyimbo zilizotujenga hata tukajiona tu ndugu wa tumbo moja!

 

Baadhi ya waliotoka kwenye Chipukizi waliendelea kukolezwa uzalendo kwa kuingia JKT. Chipukizi na JKT zikawafanya vijana wa Tanzania wasitambuane kwa dini, kabila wala kanda. Walitambuana kwa kuulizana makambi ya JKT walimokuwa, au magwaride na halaiki walizoshiriki! Wengine walitambuana kwa kutajiana shule walizosoma.

 

Baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa siasa ya vyama vingi, Chipukizi ikafa sawia na mfumo wa chama kimoja cha siasa. Vijana wote wenye umri wa miaka 20 na zaidi kidogo ya hapo (ambao ni wengi kweli kweli), hawana vionjo vya kizalendo kama tulivyofaidi sisi.

 

Juzi wakati wa maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar , na baadaye sherehe za uwashaji Mwenge wa Uhuru nilitokwa machozi ya furaha yaliyochanganyika na simanzi.

 

Nilifurahi kwa sababu niliwaona watoto walivyoshiriki halaiki. Walivyoweza kukusanywa pamoja na kuwa kitu kimoja. Niliingizwa simanzi kwa sababu niliona kile walichokuwa wakikifanya hakikuwa endelevu! Walipotengeneza maumbo yenye maandishi AMANI, nilijiuliza kama kweli viongozi wetu wa sasa wana dhamira ya kujenga umbo la neno hilo katika mioyo ya watoto wetu.

 

Uzalendo ndiyo dira ya maendeleo ya Taifa lolote. Wamarekani wanalinga na kutamba duniani kwa sababu ya uzalendo uliowazalishia umoja wao. Wachina wanasonga mbele kwa sababu wametambua kuwa dhima yao ni kufanya lolote liwalo ili wawe juu ya mataifa yote. Kama Wachina ambao ni zaidi ya bilioni 1.3 wameweza kujenga uzalendo, seuze Watanzania ambao ni milioni 45?

 

Tukiwa wazalendo hata haya matatizo ya kipuuzi ya ugomvi wa kiimani yatatoweka. Ugomvi wa vyama vya siasa utapungua au kutoweka kabisa. Uzalendo ni kujitambua. Kujitambua ndiyo chachu ya maendeleo ya jamii yoyote. Sioni namna nzuri ya kujenga uzalendo zaidi ya kuanza na watoto wadogo kupitia Chipukizi na mitaala katika shule na vyuo vyetu.

 

Please follow and like us:
Pin Share