Wanaowania urais wa Awamu ya Tano Tanzania, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), walianza kuchukua fomu mjini Dodoma Jumatano Juni 3, 2015. Inaonekana wengine waliokuwa wanatajwatajwa, wanasita, hawajajitokeza kugombea, hawajachukua fomu! Labda watajitokeza baadaye, au wanaona hawana nafasi nzuri.
Lakini jambo la kusikitisha ni ile hali ya kupakana matope iliyojitokeza wakati baadhi wagombea hao watarajiwa, walipokuwa wanatangaza nia. Badala ya kueleza sera zao, walitufanyia nini na watatufanyia nini, wanashambulia na kuwasema wenzao.Lowassaa

Kwani fisadi ni nani?
Kuna watu wanaowaita wenzao mafisadi, wala rushwa, wana kashfa mbalimbali n.k. Lakini, ukiwauliza watu hao, hawana ushahidi wowote! Hivi tujiulize fisadi ni nani? Fisadi huyo kwa nini hakamatwi, akafikishwa Takukuru na kwenye vyombo vya sheria na kazi ikaisha? Kuna madai pia kwamba baadhi ya wagombea wanamwaga pesa, n.k. Hivi hao wanaodai hivyo, wamewaona wagombea wakimwaga pesa? Na kama kweli wanamwaga pesa, mnawaona, halafu mnawaacha, maana yake nini?


Mtu akimwaga pesa na anaonekana au uthibitisho wa jinai hiyo unapatikana, si ndiyo ushahidi wa kutosha wa kumkamata na kumpelekea kwenye vyombo vya sheria ili achukuliwe hatua! Watu wanalalamika tu fisadi, fisadi, fisadi…! Ushahidi wala ukweli hakuna. Kwa vile mnamuona huyo fisadi, anafanya dhambi, mnamuacha, basi ni uthibitisho dhahiri kuwa ninyi mnaotoa madai hayo ni walalamishi tu, waongo na wazandiki! Lazima mtakuwa na lenu jambo! Uongo wa Richmond, kwa mfano, ulithibitishwa mahakamani na ndiyo maana waliofikishwa mahakamani, waliachiwa huru na hakuna mtu aliyetiwa hatiani! Waongo waliowazuga Watanzania kuwa mashine za kufua umeme za Dowans, zilizoletwa baada ya Kampuni ya Richmond kuchelewa kufua umeme wa dharura, kuwa ni mbovu, chuma-chakavu, hazifai, waliumbuka baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, kuzikagua na kusema ni mashine za kisasa na nzuri. Na ndiyo zinafua umeme chini ya kampuni ya Kimarekani! Hata Rais Barack Obama alizitembelea na kuthibitisha ubora wake!


Kulalamika na kunung’unika, uzushi, chuki, fitina, unafiki, kupakana matope, gere na kupiga porojo, ni tabia mbaya ambayo kwa bahati mbaya, imewakumba Watazania wengi. Na ndiyo maana hata utendaji wa baadhi ya viongozi hauonekani, bali ni kulalamika tu. Matatizo ya nchi yetu ni uzembe, kutofuata sheria na ukosefu wa uzalendo, siyo ufisadi.
Kwanza, ni dhahiri kwamba tatizo la Tanzania, kamwe si ufisadi wala rushwa! Tatizo kubwa la Tanzania la kwanza ni watendaji kutowajibika kikamilifu katika kazi zao na kutenda mambo yanayoonekana. Mtu akipewa kazi ya utendaji, haifanyi kwa ufanisi na matokeo yake, kunazuka matatizo. Kwa mfano, Mkurugenzi wa Halmashauri hasimamii usafi wala mipango miji, anaacha ujenzi holela, hahimizi utunzaji wa mazingira, n.k.


Matokeo yake, taka zinazagaa, afya za watu zinaathirika, watu wanajenga mabondeni na inashindikana kuwahamisha kiasi kwamba wakati wa mvua, mafuriko yanatokea na yanazoa na kuua watu. Na hii siyo tu kwenye Halmashauri, hata kwenye Serikali Kuu pia kuna watendaji wengi wizarani, hawatimizi wajibu wao na ndiyo maana matatizo hayaishi, watu wanakatishwa tamaa na watendaji. Hakuna mtu yeyote anayechukua hatua kwa utendaji mbovu wa aina hii. Si hata waziri wa kawaida au Waziri Mkuu! Huu ni ugonjwa mkubwa.
 Tatizo la pili, ni kutofuata na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu. Sheria zinavunjwa kila siku, kila mahali, kila eneo na hakuna mtu yeyote anayekemea hili. Si waziri, si hata Waziri Mkuu! Na ndiyo maana matatizo kama kuchinjwa kwa albino kama kuku hayaishi; mapigano ya wakulima na wafugaji yanashidikana kuzuiwa na sijui hadi wafe watu wangapi! Kwa jumla mambo mengi yanakwama! Kama kinyume cha ufisadi ni kile kinachoitwa uadilifu, basi Serikali hii inayoongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye ndiye anaonekana na kutajwa kuwa mwadilifu, basi utekelezaji wa mambo mbalimbali ungekwenda vizuri.
Kwa mfano, wakati wa kipindi cha miaka miwili tu cha Uwaziri Mkuu wa Edward Lowassa, utekelezaji wa Sera ya CCM ya Shule ya Sekondari kila Kata, ulitekelezwa vizuri. Kwa takriban miaka miwili tu, shule za sekondari za kata zipatazo 3,000 zilijengwa! Na shule maana yake ni vyumba visivyopungua 10 hivi, kila shule! Baada ya kuondoka Lowassa, Rais akaagiza mwaka 2012 kuwa zijengwe maabara kwa ajili ya shule hizo, kwa miaka miwili.


Maabara ni vyumba vitatu tu vya maabara ya Fizikia, Kemia na cha Bailojia. Miaka milwili ilitimia Novemba 30, 2014, lakini utekelezaji ni chini ya asilimia 50. Rais ikabidi aongeze muda wa miezi sita, hadi Juni 30, mwaka huu. Lakini hakuna uhakika, kama hata ifikapo wakati huo mradi huu utakuwa umekamilika.
Lowassa, alisimamia kikamilifu, shule zikajengwa. Waziri Mkuu wa sasa anaonekana hakuusimamia vizuri mradi huu na haukukamilika kama ilivyotarajiwa! Haya si majungu, bali ndiyo hali halisi. Sasa tatizo hapa si ufisadi, bali staili ya utekelezaji.
La tatu, ni kuwa tumekosa kabisa uzalendo. Kila mtu anaona kuwa ni mwingine, na siye yeye anayehusika na kuinua uchumi wa  nchi katika eneo lake lolote lile, kama ni mzoataka, mhudumu au karani ofisini, dereva au fundi-mitambo, injinia, daktari au mwanasheria, ofisa au kiongozi kwenye halmashauri au wizarani, na hata viongozi wa kisiasa, kama madiwani, wabunge hata mawaziri! Kukosa uzalendo ndiko kunakotufanya tushindwe kujitegemea na kutokuwa na uchungu na kuchukua hatua kwa wachache wanaoharibu mambo. Tunashindwa kutengeneza na kutumia vitu vya kwetu na tunaagiza kutoka nje kwa kutumia fedha za kigeni, hata vijiti vya kuchokonoa meno! Tunashangaa nini sasa kuwa thamani ya shilingi, si tu inashuka kila siku, bali inaporomoka. Halafu tunalalamika!


Tunahitaji, mwenye maono, mtendaji jasiri, mfuatiliaji na siyo mnafiki, mwoga, goigoi, lofa na mbinafsi. Katika hali ambayo Uchumi wetu uko sasa hivi, anahitajika mtu atakayeweza kusimamia utekelezaji kwa ufanisi ili kuweza kuvuka, kwa muda mfupi ujao. Staili ya kukaa ofisini kuandika barua ili mtendaji fulani afanye na mkubwa anasubiri kwa barua, majibu ya maelekezo yake, haifai kabisa! Ndiyo maana tuna rasilimali nyingi, lakini bado tunashindwa kuinuka kiuchumi. Ni ufisadi au kushindwa utekelezaji?
Nchi ndogo kama Rwanda inapata sifa katika mambo mbalimbali kwa sababu wanaamua, wanatekeleza. Tuliamua kuwa na barabara za juu (fly-over) tangu mwaka 2006 kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, hadi leo hakuna hata nguzo moja iliyowekwa kutengeneza barabara hizo. Mabasi yaendayo kasi nayo yako wapi? Msongamano wa magari Dar es Salaam unazidi kila siku. Wakubwa hawajali kwa vile wanapopita barabarani, askari polisi wanayasimamisha magari yote yasipite, mpaka misafara yao ipite. Hawajui adha ya msongamano. Nairobi waliamua kutengeneza fly-over baada ya sisi kuamua hivyo, na sasa wenzetu wamemaliza kazi hiyo na kuna ahueni wanayopata katika kupunguza msongamano wa magari.


Unaweza ukajiuliza, hivi ni kwa nini haya malori ya mizigo, makontena na matenki ya mafuta yamezagaa jijini Dar es Salaam kuongezea msongamano? Serikali inashindwa nini kutenga eneo kwa mfano, Kibaha, Mlandizi au Ruvu, na kuweka aina ya Bandari Kavu ili mizigo isiyokuwa ya Dar es Salaam isombwe kwa treni kutoka bandarini na kupelekwa huko ili malori sasa yaanzie kubeba mizigo hiyo kuanzia huko kwenda mikoani na nchi jirani? Inashindikana vipi na kwa nini haifanyiki?
Kwa nini usafiri wa uhakika wa njia ya reli unashindikana kufufuliwa ili kuzihudumia nchi jirani na kupata mapato makubwa ya biashara ya usafirishaji, badala ya hali ya sasa ya malori kuharibu barabara nyingi tunazozijenga? Inashindikana vipi? Tunasubiri nini, tunamsubiri nani? Jibu, tunaogopa na tunashindwa kufanya uamuzi mgumu na utekelezaji! Viwanda karibu vyote vikubwa vya Dar es Salaam, kwa mfano; Kioo Ltd., Mabati, Sigara, Urafiki, Bakhresa Group, vimeunganishwa na njia ya reli kutoa mizigo na malighafi bandarini na kupeleka viwandani na pia kubeba bidhaa za viwandani kupeleka bandarini au kwenye eneo la kupakia mizigo ya treni kwenda bara na nchi jirani.


Mbona hizo njia za reli zimeota majani, nyingine zimeng’olewa na hazitumiki tena. Kuna nini? Kwa nini hata jambo hili linashindikana? Haya ni maeneo machache ambayo kutokana na kushindwa kufanyiwa uamuzi na utelekelezaji, basi mambo hayaendi na matatizo yanalundikana. Inaonekana viongozi wanashindwa kutatua matatizo na likizuka jambo, badala ya kutatua, wanajificha chini ya meza. Tunashuhudia  Rais anahangaika peke yake kujaribu kukwamua mambo, lakini wasaidizi wake wengi, mawaziri, wanaonekana kama wamechoka.
Baadhi ya mawaziri wengine wanaotangaza nia ya kuwania urais, wanaahidi kufanya mambo makubwa ya ajabu, lakini hawaelezi, kwa nafasi zao za sasa wamefanya nini na kufanikiwa kwa lipi? Wanasubiri mpaka wawe marais!


Huu unazi wa ufisadi ndio unanifanya nikumbuke alichosema Waziri Mkuu wa zamani, Mheshimiwa Frederick Sumaye, ambaye naye amajitokeza kwa mara nyingine tena kutaka kugombea urais. Badala ya kusema atafanya nini, naye eti analaumu ufisadi na kujaribu kudandia mafanikio aliyoyapata Rais Benjamin Mkapa wa Awamu ya Tatu, kujidai kuwa yeye ndiye aliyefanya kazi yote hiyo! Si kweli kwa sababu, pamoja kuwa alidumu kwa miaka 10, akiwa Waziri Mkuu aliyekaa kwa muda mrefu kwa mfululilizo kuliko Waziri Mkuu mwingine yeyote nchini, hakutenda kwa matarajio ya Rais na ikafika wakati Rais Mkapa alimuondolea Waziri Mkuu Sumaye, kazi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kupeleka shughuli hiyo yote kwenye Ofisi yake ya Rais, na kumpa Jenerali Hassan Ngwilizi, kazi hiyo!
Waziri Mkuu Sumaye aliachiwa kuendesha Idara ya Maadhimisho ya Taifa na Usimamizi wa Maafa (kama yakitokea)! Sasa Waziri Mkuu ukimuondolea usimamizi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, unamuachaachaje? Haya si majungu, ndiyo ukweli ulivyokuwa! Huyu naye analaumu ufisadi, ndiyo maono yake! Mara ya mwisho Mheshimiwa Sumaye alipojaribu kugombea, mwaka 2005, hakutokea hata katika “Tatu Bora”! Nini kimebadilika sasa ili adhani kuwa anaweza akashinda?

Hata Mwalimu Nyerere alichangiwa Fedha
Hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alichangiwa fedha na wafanyabiashara na watu mbalimbali wakati wa TANU.
Kuna watu wanaomlaumu Lowassa kwa kupokea fedha kutoka kwa marafiki zake, zile ambazo huwa anazitoa kwenye harambee mbalimbali, anazoombwa azifanye na ambazo zimekuwa za mafanikio makubwa hadi wenzake walikuwa wakimuonea gere na kijicho, hadi mipango ikafanywa ili harambee hizo asiendelee nazo tena, kwa madai kwamba zilikuwa ni kama kujisafishia njia ya kuomba urais. Sasa ni nongwa Lowassa kupewa fedha na marafiki zake ambao wengi ni wafanyabiashara na wananchi wengine wenye uwezo na wenye nia ya kusaidia?
Swali la kujiuliza: Hivi si kweli kwamba viongozi wengi humu humu nchini, mara zote huwa wanajikomba kwa baadhi ya wafanyabishara maarufu na wanapewa fedha za kuchangia miradi ya maendeleo kwenye majimbo yao? Kwa zile harambee ambazo huendeshwa na viongozi wengine mbalimbali, kwani wao fedha huwa wanazipata wapi mpaka ionekane kwamba kwa Lowassa kufanya hivyo ni dhambi?


Hivi siyo mara kwa mara, baadhi ya wafanyabiashara maarufu, kwa mfano Mzee Reginald Mengi; Said Salim Bakhressa; Rostam Aziz, wamekuwa wakifuatwafuatwa na viongozi kuombwa fedha za kuchangia kwenye harambee? Dhambi kwa Lowassa, kwa wengine ni sawa!
Hata Mwalimu Nyerere wakati wa harakati za kuijenga TANU na kupigania uhuru wa nchi hii alikuwa anasaidiwa na wafanyabiashara mbalimbali na watu waliokuwa na uwezo. Hata fedha za kununulia tiketi ya kumpeleka Mwalimu Nyerere kwenye Umoja wa Mataifa (UNO) katika harakati za kudai Uhuru, alichangiwa na watu mbalimbali, wakiwamo wafanyabiashara wa wakati huo.
Hata katika maisha yake ya kawaida Mwalimu Nyerere naye alikuwa anasaidiwa na watu waliokuwa na uwezo na wenye moyo wa kusaidia. Wakati huo, kina Mzee John Rupia; kina Sykes; Dosa Aziz (alikuwa pia mfanyabiashara, aliyepata kandarasi ya kusambaza vifaa vya ujenzi hata kabla ya Uhuru), walimsaidia kifedha Mwalimu. Ukiacha hao wachache, ambao walikuwa na uwezo, lakini hata wazee wa kawaida tu wa Dar es Salaam, wengine wakiwa wavuvi na wachuuzi wa samaki (Mzee Mshume Kiyate) na wengine wachuuzi wa bidhaa sokoni, walikuwa wakimsaidia Mwalimu na viongozi wengine wa TANU, wakati huo. Vipi misaada ya aina hii imegeuka kuwa haramu na dhambi hii leo?  Tusiisahau na kuitupilia mbali historia hii.


Lakini hata Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipong’atuka na kuanzisha Taasisi ya Mwalimu Nyerere, aliendesha harambee ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuijenga taasisi hiyo. Alichangiwa na matajiri na watu wa kawaida. Mbona hilo halikuwa nongwa? Je, ina maana kuchangiwa kwa Mwalimu kabla na hata baada ya Uhuru kuliondoa utendaji kazi wake au uadlifu kwa Taifa kwa kuwapendelea waliomsaidia? Kwa nini kwa Lowassa kuwe na shaka hiyo?
Si tu michango ya wafanyabiashara, mbona watu wanachangiana mamilioni ya fedha siku hizi kwa ajili ya harusi, kwani wanaochanga wanatarajia nini baadaye? Watu wanaweka tafsiri mbovu ya michango anayopewa Lowassa, kwamba kwa vile anachangiwa na “Marafiki wa Lowassa” (wanaomtakia mema na wenye moyo wa kutoa), basi itabidi alipe fadhila Fulani haramu baadaye! Wamachinga, madereva wa Boda Boda, Mama Lishe nao pia wamekuwa wakimshangia Lowassa, si wafanyabiashara tu. Fadhila ambayo wote hao wanatarajia kuipata ni uongozi wake bora!
Kama alivyosema Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, hata wana-CCM wote milioni sita wakimpigia kura mgombea wa CCM hawezi kushinda urais kwa kuwa wapigakura nchini ni zaidi ya milioni 23.
Watanzania, tusidanganyane! Tunamhitaji mbunifu, mchapakazi hodari, mwenye rekodi ya kutenda. Haya majungu ya ufisadi na kuundiana kashfa zisizokuwapo, yatatufanya daima tubaki nyuma, tusiendelee, ingawa tuna rasilimali zote za kupiga hatua kubwa ya maendeleo na Watanzania, kila mmoja wetu, kuwa na hali bora ya maisha.


Mtu anayeweza akayasimamia mambo kwa uhakika na yakatekelezeka, si mwingine, isipokuwa Edward Ngoyai Lowassa!
Kama alivyosema Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete wakati anafungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, mjini Dodoma hivi karibuni: Tunataka mtu anayekubalika na wana- CCM ndani ya CCM na Watanzania wasiokuwa wanachama wa CCM na hata wa vyama vya upinzani. Sababu wana-CCM wote wapatao milioni 6 hata wote wakimpigia mtu wao kura, lakini kama watu wengine hawakumuunga mkono, basi mtu huyo hawezi kushinda urais. Kuna jumla ya wapiga kura milioni 23.


Kwa kishindo kilichotokea Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Jumamosi Mei 30, 2015, uwanja ulifurika kupita kiasi, ni dhahiri kuwa Lowassa anakubalika ndani na nje ya CCM! Wapinzani wake, kwa kukosa hoja, wanadai eti ameanunua watu hao! Hivi ana fedha kiasi gani na ameiba wapi, kiasi kwamba anaweza akawanunua watu wanaojaza uwanja wa mpira? Utamnunua kwa hela ngapi mkongwe wa siasa nchini, Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, ambaye naye alikuwapo uwanjani na kutoa hotuba ya kumfagilia Lowassa?
Vile vile kama alivyosema Mzee Kingunge: Kwa wana-CCM, siyo tu tunamchagua Rais, bali tunamchagua Mwenyekiti wa CCM, ili chama hicho kiwe kwenye mikono salama ya mtu mwenye uzoefu nacho na aliyekuzwa nacho! Na kwa Watanzania, siyo tu tunamchagua rais, bali tunamchagua Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania.


Sasa kazi hizo zote unampa nani? Lowassa, amekulia kwenye Chama Cha Mapinduzi na anakijua vizuri na anakubalika; ni mtendaji mzuri na mchapakazi, atakuwa rais mzuri wa kuendesha uchumi. Alipata pia mafunzo ya kijeshi na ya uongozi, Monduli na akashiriki katika Vita ya Kagera. Hata wanajeshi wanaweza kumkubali kuwa Amiri Jeshi Mkuu wao! Kwa waliojitokeza, hakuna anayemzidi Lowassa, mwenye rekodi hii na ujasiri wa kutenda!

Makala hii meandikwa kwa kukusanya takwimu na taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali rasmi na kufuatilia mwenendo wa kisiasa nchini kwa muda mrefu.

 
2132 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!