Na OWM – TAMISEMI, Iringa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kujenga vijana wenye afya bora, nidhamu, uzalendo, kujiamini na uwezo wa kushindana katika mazingira ya kitaifa na kimataifa.
Prof. Shemdoe amesema hayo leo Juni 09, 2026 mjini Iringa, wakati akifungua mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ambayo yanafanyika kitaifa mwaka huu mkoani Iringa.
“Hapa hatukuzi tu vipaji bali tunajenga viongozi wa kesho, mabalozi wa taifa letu na nguvu kazi yenye tija kwa maendeleo ya taifa,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amehimiza kuwa jukumu la kuendeleza michezo na Sanaa ni la kila kiongozi katika eneo lake la utawala na si la wizara pekee, hivyo ameelekeza kila halmashauri iwe na shule maalum ya kukuza vipaji vya michezo na Sanaa yenye miundombinu bora na wataalam mahiri.
Prof. Shemdoe amezielekeza halmashauri zote kupitia mipango miji kutenga maeneo maalum ya michezo huku akizitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga na kuyalinda maeneo ya huduma za kijamii yakiwemo ya shule, huduma za afya, sehemu za kupumzikia na za kufanyia mazoezi.
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, UMITASHUMTA na UMISSETA si mashindano ya kushinda medali au vikombe pekee, ni chuo cha malezi ya vijana na msingi wa kujenga taifa la watu wanaojiamini, wanaowajibika na wenye ushindani na uzalendo.
Kutokana umuhimu wa michezo na Sanaa, Prof. Shemdoe ameahidi kwamba Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu, michezo na utamaduni na itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila mtoto mwenye kipaji anapata fursa ya kukiendeleza kipaji chake bila kikwazo chochote.
Aidha, Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kuwasilisha salaam za upendo kwa wananchi wa Iringa kutoka Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi ambao kwa pamoja wanatambua umuhimu wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa kuendelea kujenga miundombinu bora ya kukuza michezo na sanaa nchini ambayo inafungua fursa za ajira kwa wenye vipaji.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Bw. Atupele Mwambene amesema kuwa lengo kuu la mashindano hayo ni kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya wanamichezo na Sanaa miongoni mwa wanafunzi, nakuongeza kuwa michezo na sanaa si burudani pekee bali ni sehemu muhimu ya mtaala na taaluma inayomjenga mwanafunzi katika ukamilifu wake.
“Kupitia mashindano haya tunatekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya kuimarisha sekta ya michezo na Sanaa ili zizalishe vijana ambao watajiajiri na baadae kuwaajiri wengine kwa kadiri watakavyokuwa wamejengewa umahiri,” amesisitiza Bw. Mwambene.
Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa mwaka huu wa 2026 yanabebwa na kaulimbiu isemayo: Michezo na Sanaa Shuleni, Daraja la Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa.













