Watu wengi walishitushwa na kushangazwa na sababu zilizotumika kuwaengua watu wengi walioomba kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika siku chache zijazo.

Kinachoshitua ni kuwa karibu wote walioenguliwa kuwania nafasi hizo ni wanasiasa kutoka vyama vya upinzani. Ni kweli wapinzani wanaweza kuwa mbumbumbu wa kushindwa kujaza fomu kwa uhakika. Lakini kama wapinzani hawa ni sehemu ya Watanzania inakuwaje wagombea wengine kutoka chama tawala, ambao nao ni sehemu ya Watanzania hao hao waweze kuepuka umbumbumbu huo katika nchi ile ile yenye mifumo inayofanana ya elimu na siasa?

Figisu zilizojitokeza wakati wa uchujaji wa wagombea ndizo zimesababisha Chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema, kujitoa katika uchaguzi huo. Wapo ambao wanaweza kushangilia hali hiyo kwa sababu za kisiasa, lakini wasisahau ukweli kuwa hatua ya Chadema kujitoa katika uchaguzi huo ina athari kubwa kwa nchi. Tusije tukajisahau tukadhani kuwa Tanzania ni kisiwa.

Ni jambo la bahati mbaya sana kuwa figisu za kuwaondoa wagombea wa upinzani zinatokea siku chache tu baada ya Watanzania kuonyesha mwamko mdogo sana wakati wa uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo. Serikali ililazimika kuongeza muda wa uandikishaji ili kuokoa jahazi. Sijui serikali itafanya nini iwapo waliojiandikisha watasusa kupiga kura.

Inaonekana kana kwamba hatukujifunza chochote kutokana na watu kususa kujiandikisha. Kwa figisu hizi na hatua ya Chadema kujitoa mtu unaweza kutabiri kabisa kuwa watu wachache wanaweza kujitokeza kupiga kura.

Ni kweli uchaguzi unaweza kufanyika na matokeo kutangazwa, lakini wale watakaoshinda watapata uhalali wa kisiasa kupitia uchaguzi ambao wapiga kura wachache tu ndio walijitokeza kupiga kura.

Itashangaza sana iwapo watakuwapo watakaoshangilia ushindi katika uchaguzi uliogubikwa na mizengwe kiasi cha kulazimisha wengine kujitoa.

Inavyoonekana kuna ambao wanapaswa kufanya siasa nchini wakati wengine hawana haki hiyo. Huko ni kujenga matabaka na kuwagawa Watanzania, kwa sababu wapo Watanzania wengi tu ambao wanaviunga mkono vyama vya upinzani ambavyo vimewekewa vigingi vya kufanya siasa.

Mgawanyiko huu kisiasa unaweza kusambaa na kuwagawa Watanzania katika nyanja nyingine. Tukifika hapo, hatutakuwa na taifa lenye umoja.

Kwa hakika, kwa haya tuliyoyashuhudia kwenye mchakato wa kupitisha wagombea kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, hakuna mshindi. Badala yake tumepanda mbegu ambayo isipofukuliwa na kuchomwa, itazaa bomu ambalo litatuangamiza sote kama taifa.

700 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!