Serikali ya Wilaya Tunduru mkoani Ruvuma imesema,itawakamata na kuwatoza faini wafugaji wote wanaoishi kiholela na kuchunga mifugo nje ya maeneo yaliyotengwa(vitalu).

Kauli hiyo imetolewa jana na mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro,wakati akizungumza na wafugaji wakati wa ufunguzi wa nyumba ya kulala wageni ya Kajima Guest House iliyojengwa na mfugaji wa jamii ya Kisukuma Mahembo Shamba.

Mfugaji huyo amelazimika kuuza sehemu ya mifugo yake na kujenga nyumba ya kulala wageni, ikiwa ni utekelezaji wa agiza la serikali linalowataka wafugaji kupunguza mifugo na kuwekeza kwenye miradi mingine ya maendeleo.

Aidha Mtatiro amesema,wafugaji watakaochelewa kwenda kwa hiari kwenye vitalu vilivyotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kukuta vimejaa wataondolewa kwa nguvu na kupelekwa nje ya mipaka ya wilaya hiyo.

Amesema,hatua hiyo ni maamuzi halali ya serikali katika kumaliza migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima iliyoanza kutokea wilayani humo huku chanzo kikitajwa ni kuwepo kwa baadhi ya wafugaji wasiotaka kufuata sheria na taratibu.

Amesema,katika utekelezaji wa operesheni hiyo,serikali itatumia vikosi vya ulinzi na usalama,ikiwa ni juhudi za kuwaondoa kabisa wafugaji na ufugaji holela unaofanywa na wafugaji wauni katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

“Serikali inawapenda wananchi wote wakiwamo wafugaji na ndiyo maana imeandaa utaratibu wa kutenga jumla ya vitalu 279 vyenye ukubwa wa ekari 500 kila kimoja kwa ajili ya shughuli ya ufugaji”alisema Mtatiro.

Kwa mujibu wa Mtatiro,licha ya mapenzi makubwa ya serikali kwa jamii ya wafugaji wilayani humo,lakini bado kuna wafugaji wanakahidi na kufanya ufugaji kiujanja ujanja kwenye makazi ya wakulima na kusababisha migogoro mingi kati ya makundi hayo mawili.

Alisema,wilaya ya Tunduru ni ya kilimo licha ya kukaribisha wafugaji,hata hivyo suruhisho la migogoro inayojitokeza kati ya wakulima na wafugaji ni lazima wafugaji wakapelekwa katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli zao.

Mtatiro,amempongeza mfugaji huyo kwa kuitikia wito wa serikali kwa kupunguza idadi ya mifugo yake na kufanya uwekezaji wa nyumba ya wageni na kuwataka wafugaji wengine kuiga mfano huo.

Kwa upande wake mfugaji huyo alisema,amelazimika kujenga nyumba ya wageni baada ya kupoteza sehemu kubwa ya mifugo yake mkoani Mbeya na Morogoro na amelazimika kuja wilayani Tunduru baada ya kusikia kuna mazingira mazuri kwa ajili ya kuchungia.

Amesema,hadi kukamilika kwa nyumba hiyo yenye vyumba 10 vya kulala wageni ametumia fedha nyingi baada ya kuuza Ng’ombe 220 na kuwataka wafugaji wengine kupunguza mifugo yao na kuwekeza katika miradi mingine ya kiuchumi.

By Jamhuri