Tusherehekee haki ya kupata taarifa kwa vitendo

Na Deodatus Balile

Leo ni siku ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki ya Kupata Taarifa au wengine wanasema ni ‘Siku ya Haki ya Kujua’ kama inavyojulikana kwa wadau wengi duniani. 

Siku hii ilitambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka 2019. Ilianza kuzungumzwa mwanzoni mwa miaka ya 2000. Tangu mwaka 2015, huadhimishwa kila mwaka Septemba 28.

Sitanii, wadau wa habari duniani baada ya kufanya utafiti mkubwa walibaini kuwa nchi yoyote au familia yoyote isiyo na taarifa sahihi, haipati maendeleo ya kweli na ya haraka. Taarifa sahihi zinamwezesha mwananchi kufikiri kwa usahihi au kufanya uamuzi sahihi bila kubahatisha.

Mifano ni mingi, ila hapa nitatoa inayoigusa jamii. Familia nyingi za Kiafrika kwa kutokuwa na taarifa sahihi za tiba na kinga ya kiafya, zimeparaganyika. 

Mwanafamilia akifariki dunia, iwe amekufa kwa ukimwi, malaria, shinikizo la damu au ugonjwa mwingine, jibu la kwanza linakuwa ni kwamba mtu wao amerogwa. 

Wakianza kutuhumiana uchawi wanauza hata mali kidogo walizonazo kutafuta ukweli juu ya nani amemloga ndugu yao, matokeo yake wanafilisika.

Wakulima wengi duniani wasipokuwa na taarifa sahihi za hali ya hewa na masoko, huo unakuwa mwanzo wao wa kufilisika. 

Mkulima asiye na taarifa sahihi atalima wakati wa kiangazi, mazao yatakaukia shambani. Atapeleka mazao katika soko lisilo sahihi. Kwa mfano, haitarajiwi mkulima apeleke magunia ya mahindi katika soko la vyuma chakavu. Lakini akijulishwa lilipo soko la chakula atakutana na wateja wenye uhitaji.

Huduma za jamii pia zinahitaji uelewa. Ninaposema huduma za jamii ninamaanisha mambo mengi. Hata kulipa kodi ni huduma ya jamii. 

Wapo wananchi ambao si wakaidi kulipa kodi, lakini hawalipi kodi kwa sababu hawajapewa taarifa sahihi juu ya taratibu za kulipa kodi. 

Au wamachinga hawapendi kuwa barabarani kuwakiwa jua na kunyeshewa mvua. Suala ni kwamba hawana taarifa sahihi za wapi wanaweza kufanyia biashara zao kwa heshima kubwa na wakapata faida.

Sitanii, kuna wananchi wanaopoteza haki zao za ajira, mahakamani au elimu kwa sababu ya kutopata taarifa sahihi kwa wakati. 

Sheria nyingi zilizoachwa na wakoloni zililenga kudhibiti taarifa kwa makusudi ili watu wengi wawe mbumbumbu, wasisimame kudai haki zao. 

Matokeo yake unakuta mtu ana haki ya kutibiwa, lakini akifika hospitalini anazungushwa na nesi au mlinzi, anatukanwa hadi anafia mapokezi.

Nchi kadhaa zimejitahidi kutunga sheria. Sheria hizi zinaazisha vyombo vya kuzisimamia, lakini bahati mbaya vyombo hivi havijaanzishwa. Hata vyombo hivi vilipoanzishwa, havijapewa bajeti ya kutosha kujiendesha. 

Wadau wa mawasiliano mwaka huu wanasema kuna umuhimu wa kutekeleza sheria za upatikanaji wa taarifa kwa kujenga taasisi imara, kwa masilahi ya umma, kwa maendeleo pamoja na kuimarisha haki ya kupata taarifa.

Wanatambua katika kufanya hivyo, hakuna anayeweza kwenda peke yake. Wanahamasisha ushirikiano wa kimataifa katika kutekeleza haki hii ya kibinadamu. 

Haki ya kupata habari ni haki ya msingi inayowezesha haki nyingine kufanya kazi. Mfano, mwandishi wa habari anapokufikishia taarifa kuwa kuna watu wanabambikiwa kesi, hii inakuwezesha kufungua kesi mahakamani kupinga ubambikiaji huu. 

Hapo haki nyingine za kuwa huru, kushirikiana na jamii, kushiriki masuala ya kijamii zitarejea mara ukiachiwa huru kama umebambikiwa kesi.

Sitanii, Tanzania inazo sheria kama ile ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya Haki ya Kupata Habari na nyingine. Sheria hizi zimeanzisha vyombo kadhaa, ambavyo hadi leo havijapata kuanzishwa. Sisi tukiwa wadau wa haki ya kupata habari, tunaendelea kufanya utaratibu wa kuikubusha serikali kutekeleza sheria hizi kwa vitendo ili kurahisisha upatikanaji wa habari.

Tunafahamu baadhi ya sheria zina vifungu vibaya vinavyozuia upatikanaji wa habari. Vinafanya suala la kupata habari liwe kama uuzaji wa bangi, kwamba liendeshwe kwa usiri mkubwa. Tunasema msitari huu tunapaswa kuuvuka. Tanzania ibaki kuwa nchi ambayo serikali na taasisi zake zinatoa taarifa bila kusubiri kuombwa.

Sitanii, Mama Samia Suluhu Hassan ameanza vema. Kitendo cha kuihamisha Idara ya Habari kutoka iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuipeleka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kimetutia moyo mno. Tunaamini kuwa kwa nia ile ile ya kujenga Tanzania ambayo taarifa zinapatikana kwa uhuru, hata sheria kandamizi zitarekebishwa.

Tunaamini pia waziri, naibu waziri na katibu mkuu waliopewa dhamana ya kusimamia masuala ya habari, watakuwa wadau wakubwa wa vyombo vya habari na hawatajiandaa kujenga uadui. 

Hatutarajii kusikia kauli za kukemeana kabla ya kusikilizana. Tujenge utamaduni wa kuzungumza kama Watanzania, na hii itatupa heshima kubwa ya kujenga mifumo imara na uwajibikaji katika kutekeleza haki hii ya kupata taarifa. Mungu ibariki Tanzania.