Julai 3, mwaka 1964 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alizungumza na watoto katika Ikulu ya Dar es Salaam. Kupitia mazungumzo hayo, alizungumza pia na watoto wote nchini kwa njia ya redio.

Aliwaeleza watoto wajibu walionao kwa wakati huo, ikiwa ni maandalizi ya wao wakiwa wakubwa kubeba mzigo mkubwa wa kuleta maendeleo ya taifa letu. Kama ilivyokuwa ada ya Mwalimu, alisisitiza sana suala la watoto kusoma kwa bidii ili kupata maarifa yatakayowasaidia wao wenyewe na taifa kwa jumla.

Akasema: “Wajibu wenu ni kujifunza…Kazi ya kujifunza kujua mambo na kutumia ujuzi huo ni lazima kuutumia kwa ajili ya kazi za maendeleo ya nchi na watu wake. Ni lazima kila mara [mtoto] ujiulize swali hili – ‘Nifanye nini kumsaidia mwananchi mwenzangu?’ Au ‘Nifanye nini kuisaidia nchi yangu?’”

Akaendelea kuwaambia watoto: “Na wale ambao wamepata bahati ya kusoma shuleni wana wajibu maalumu katika kazi ya kusaidia maendeleo ya taifa letu.”

Nimenukuu maneno haya ya Mwalimu yenye umri wa miaka 55 kwa sababu ukweli na umuhimu wake bado uko pale pale.

Serikali ya sasa na zilizopita zimejitahidi kuhakikisha watoto wa Tanzania wanapata elimu – japo tatizo kubwa bado lipo kwenye aina na viwango vyenyewe vya hiyo elimu.

Tunashuhudia Serikali ya Awamu Tano ikitenga mabilioni ya fedha kuhakikisha watoto katika shule za msingi na sekondari wanapata elimu bure. Hadi mwaka jana Sh bilioni 23 zilikuwa zikitengwa kila mwezi ili kukidhi suala hilo muhimu. Hili ni jambo la kupongezwa.

Hata hivyo, kiasi hiki cha fedha hakiwezi kukidhi mahitaji makubwa ya wanafunzi na walimu hasa kutokana na kasi ya ongezeko la watoto wanaoanza shule kila mwaka. Ongezeko la watoto linasababisha kila mwaka kuwepo mahitaji mapya ya vyumba vya madarasa, vitabu vya ziada na kiada, vifaa vya kufundishia, walimu, nyumba za walimu na hata watumishi wengine. Kwa ufupi ni kuwa mzigo huu wa kusomesha watoto wa taifa letu ni mkubwa mno.

Tangu kutangazwa uamuzi wa kutolewa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, wazazi katika baadhi ya mikoa wameisukumia mzigo wote serikali. Tumeshuhudia na kusikia baadhi ya wazazi waliosikia tangazo hilo la serikali wakienda shuleni wakidai warejeshewe fedha walizochanga na wengine wakidai vitu au thamani walizotoa kwa ajili ya kuwasaidia watoto kusoma vizuri. Hoja yao ikawa kwamba wanafanya hivyo kwa sababu serikali imesema ‘elimu ni bure’.

Mbaya zaidi, mikoa iliyo nyuma kielimu ndiyo yenye wazazi wengi waliofanya vituko hivyo. Mikoa iliyotambua na kuthamini elimu kabla na baada ya Uhuru inaendelea kuboresha hali ya elimu katika maeneo yake bila kusubiri nguvu za serikali.

Mwaka 1964, kama nilivyosema hapo juu, Mwalimu alieleza wajibu wa vijana baada ya kuwa wameshapata elimu. Tangu kipindi hicho kuna mamilioni kwa mamilioni ya vijana wa taifa hili waliopata elimu, tena elimu bora kabisa.

Mwalimu alisema: “Ni lazima kila mara ujiulize swali hili – ‘Nifanye nini kumsaidia mwananchi mwenzangu?’ Au ‘Nifanye nini kuisaidia nchi yangu?’”

Kwa wale waliopata elimu hawana budi kurejea swali hili na kuona anafanya nini kwa ajili ya jamii na taifa lake.

Vijana na wazee waliopata elimu hawana budi kurejea kwa wananchi kuona nini wanapaswa kukifanya kwa ajili ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa jumla. Nadhani katika hili, pamoja na misaada mingine mingi inayopaswa kutolewa kwa jamii, suala la elimu linapaswa kupewa kipaumbele.

Mwalimu huyo huyo alipata kusema kama kweli unataka kumsaidia maskini, hakikisha mtoto wake unampatia elimu. Wale maadui watatu wa taifa – Ujinga, Maradhi na Umaskini – adui hatari kuliko wote ni ‘Ujinga’. Adui huyu akidhibitiwa vilivyo ni rahisi mno kuwatokomeza maadui wengine wawili – Maradhi na Umaskini.

Ni kwa kulitambua hilo, nashauri tufanye mapinduzi kadhaa. Napendekeza uongozi wa kila kijiji nchini uwe na kanzidata ya watu wa asili ya kijiji hicho ‘waliofanikiwa’ kielimu na pia kifedha. Nashauri kila kata iwe na kanzidata ya ‘waliofanikiwa’, na kwa utaratibu huo huo twende hadi katika wilaya na mkoa.

Naamini kwa kufanya hivyo, hasa katika ngazi ya kata, kutasaidia kuwatambua na kuwashirikisha watu wote ambao kama ni suala la harambee, watashiriki na kutoa mchango mkubwa wa maendeleo katika sekta mbalimbali.

Si jambo la fahari kuona watoto wakisomea chini ya miti au watoto wa madarasa mawili wakitumia chumba kimoja cha darasa ilhali kijiji au kata hiyo ikiwa na watu wengi waliofanikiwa kimaisha ambao endapo wakishirikishwa wanaweza kabisa kubadili hali ya mambo.

Tumefanikiwa mno kwenye michango ya harusi na sherehe nyingine za kila aina. Sioni ni kwanini tusifanikiwe kwenye hili la kuchangia maendeleo ya elimu katika maeneo yetu.

Tutakuwa tukijidanganya kwa kuamini kuwa serikali pekee inaweza kuboresha hali ya elimu kwa watoto wetu. Tushirikishe wadau kwenye elimu bila kuwashurutisha, maana miongoni mwa mambo yaliyoishawishi serikali kufuta ada na michango ni kero walizopata wazazi na walezi wakati wa kudaiwa michango hiyo.

Wale wa vijiji, kata, wilaya na mikoa watakaobweteka kwa kuamini kuwa elimu kwa watoto wao ni wajibu wa serikali pekee, wataachwa mbali sana kimaendeleo. Mzazi au mlezi ndiye mwenye jukumu la kwanza la kuboresha hali ya elimu ya mtoto. Hili linapaswa lianzie kwetu wananchi wenyewe. Serikali ni nyongeza tu.

By Jamhuri