Kauli za viongozi ziwe za hadhari, zisilete mauaji

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bashiru Ally, alipowataja wakuu wa mikoa wawili kuwa wamo kwenye orodha ya viongozi vijana watakaopelekwa kupata mafunzo ya uongozi, wapo ambao hawakumwelewa.

Siku mbili baadaye, hao waliokuwa hawamwelewi, walimwelewa vizuri. Kati ya wakuu wa mikoa wawili waliotajwa, mmoja – yule wa Mkoa wa Mbeya – akaibuka na kauli chafu akihamasisha mauaji. Je, bado yupo anayepingana na Dk. Bashiru?

Lakini kabla yake kukawapo Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni – mwanamama – aliyeagiza watuhumiwa wote wa wizi katika wilaya ‘yake’ wapigwe na ikiwezekana wapelekwe mahakamani wakiwa wameshavunjwa miguu!

Ulianza kama moto wa mabua, kwani kuna Katibu wa UVCCM wa Kata ya Sandali, yeye alisimama jukwaani na kuwataka polisi wawaache vijana wa UVCCM wawapige na kuwavunja vunja wale wote wanaombeza Mwenyekiti, Rais John Magufuli.

Akamtaka mgeni rasmi amfikishie Rais Magufuli maombi yao [yake] ya kuachwa wawavunje miguu, kwamba  wawaburuze na wawakatekate wale wote wanaomkosoa rais.

Lakini ikumbukwe kuwa kabla ya huyu, yupo mwingine kule Tarime, mkoani Mara aliyetoa kauli inayoendana na hii, akiapa kuwamaliza wote wanaopingana na serikali!

Kauli hizi zilianza kama moto wa mabua, lakini kadiri siku zinavyosonga ndivyo huu moto unavyobadilika na kuwa wa petroli. Sikusudii kurejea historia ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda, lakini itoshe kusema kuwa cheche zilizosababisha moto wa mauaji yale zilianza kwa staili hii ya kauli za hatari na za kipuuzi.

Kauli hizi zinatolewa na viongozi wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi ambao kimsingi walipaswa kuwa ndiyo dira katika malezi bora ya taifa letu. Hizi si kauli za kuzisikia na kuziacha zielee angani. Hizi ni kauli zinazohamasisha uvunjifu wa amani na umwagaji damu katika taifa letu.

Bahati mbaya mamlaka ambazo zina wajibu wa msingi wa kulinda amani, upendo, umoja na mshikamano wa jamii na taifa letu ziko kimya kana kwamba yanayosemwa ni aina fulani ya muziku mwororo unaomsababishia msikilizaji usingizi.

Watu makini walitarajia kukisikia Chama Cha Mapinduzi kikiwakana viongozi hawa hadharani. Watu walitarajia kusikia taasisi kama ile ya Mwalimu Nyerere ikijitokeza kulaani na kukemea kauli hizi hatarishi. Wale wanaojitambulisha kama Watanzania walio tayari kuifia Tanzania walipaswa kutoa kauli za kupinga matamshi mabovu kama haya. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora sina hakika kama imelaani kauli hizi.

Jeshi la Polisi ambalo dhima yake kuu ni kulinda usalama wa raia na mali zao, na ambalo limekuwa likikemea vitendo vya watu kujichukulia sheria mikononi limeziba masikio kabisa. Sidhani kama kimya hiki kingeendelea endapo kauli hizi hatari zingekuwa zimetolewa na upande wa ‘nyumba ya pili’. Kimya chao kinaashiria kukubaliana na maandalizi ya mauaji kama yanavyohamasishwa na viongozi hawa. Hii ndiyo tafsiri tunayoipata, maana huu woga na kigugumizi cha ukimya kinatoka wapi?

Ndugu zangu, maendeleo tunayofaidi sasa ni matokeo ya hali ya amani, utulivu na umoja katika taifa letu. Amani ni tunda au zao la haki. Ni jambo la hatari kuona viongozi ndio wanaoanza kuishiba na kuikinai amani.

Mwizi hana alama maalumu usoni inayomtambulisha kuwa ni mwizi. Mkuu wa mkoa anapoagiza kupigwa na kuuawa kwa wale wanaoingia katika nyumba, maana yake anaagiza kuuawa kwa yeyote hata kama hana nia wala hatia ya kutenda uhalifu.

Kauli hii itasababisha kuuawa hata wale wanaofika nyumbani kuomba maji au hifadhi. Maagizo ya RC na DC yanaweza kuwafanya hata wale wanaokimbia kujiokoa wadhaniwe kuwa ni wezi na kwa maana hiyo wastahili kupigwa, kuvunjwa vunjwa na kuuawa. Tusikubali kufikishwa huko.

Nchi yetu inavyo vyombo vya utoaji haki. Kuna vyombo vya ulinzi na usalama vyenye wajibu wa kuhakikisha raia wema wanaishi salama. Kuna mahakama ambayo kazi yake ni kutafsiri sheria na kutenda haki. Tunachoelezwa na mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya ni kuwa vyombo vyote hivi sasa vimeshindwa kazi kwa hiyo wananchi wachukue sheria mikononi. Tusikubali ufedhuli huu.

Tanzania ni nchi ya amani si kwa sababu imeumbwa hivyo. Amani hii ni matokeo ya kazi kubwa na ya kutukuka iliyotendwa na wazee wetu na sasa inaendelezwa na viongozi wetu wakuu. Makabila zaidi ya 120 kuyaweka pamoja na watu wake wakaishi katika umoja si kazi nyepesi hata kidogo. Haya ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na watangulizi wetu. Kazi hii njema isiharibiwe na viongozi waliolewa madaraka wanaodhani kubomoa si kazi ngumu kama ilivyo kujenga!

Kwa umoja wetu tuungane kuwakemea wale wote wanaohamasisha umwagaji damu katika taifa letu. Kazi iliyo mbele yetu ni ya kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja, jamii na taifa. Hilo litawezekana endapo tutaendelea kuwa wamoja na tunaoishi kwa kuheshimu na kuzingatia utawala wa sheria. Viongozi wanaohimiza mauaji hawatufai. Ni mufilisi, na kwa kweli watu wa kariba hiyo ni wa kupuuzwa.