Wiki kadhaa zilizopita Rais John Magufuli alitoa kauli nzuri yenye kuleta matumaini kwa waliopoteza au walioelekea kupoteza matumaini.

Julai 18, mwaka huu, akiwa Kongwa mkoani Dodoma, alitamka maneno haya: “Mlinichagua kwa ajili ya watu wote, hasa wanyonge wanaopata shida. Siwezi nikatawala nchi ya machozi. Machozi haya yananiumiza. Siwezi kutawala wanaosikitika, wako kwenye unyonge na unyonge wenyewe ni wa kuonewa…Nitaendelea kuwa mtumishi wenu. Naomba Mungu aendelee kunilinda. Kazi hii nisiifanye nikiwa na kiburi, nikawe mtumishi wa kweli bila ya kupendelea mtu na huruma ya kweli ya upendo wa Mungu ikanijae katika moyo wangu.”

Maneno haya si mepesi. Ni mazito kama ulivyo uzito wa aliyeyatoa. Kuna mabadiliko makubwa yenye tija ameyafanya kwa masilahi mapana ya nchi yetu. Bahati mbaya si kila linalofanywa linapaswa kutangazwa.

Kuna mabadiliko yamefanywa. Sipendi kuyataja, maana wenyewe walishaweka sheria ya kutojadiliwa.

“Siwezi nikatawala nchi ya machozi. Machozi haya yananiumiza. Siwezi kutawala wanaosikitika, wako kwenye unyonge na unyonge wenyewe ni wa kuonewa.” Ningeomba maneno haya yawaingie wananchi wengi maana yanatoa mwongozo wenye matumaini ya haki.

Rais japo ni kiongozi mkuu wa nchi, kimwili hayuko kila mahali. Kwa kutambua ugumu wa yeye kuwapo kila mahali, ikaonekana ni vizuri akawa na wasaidizi kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi taifa. Wale wanaochaguliwa au kuteuliwa kumsaidia kazi mbalimbali wana wajibu wa kumsaidia kweli.

Wanapaswa kuwa watu wa kutenda haki bila woga wala uonevu. Wanapaswa kuwa wakweli kwa wananchi na wakweli kwa yule wanayefanya kazi kwa niaba yake. Inapotokea mtu anayetakiwa kumpa ukweli aliyemteua akashindwa kufanya hivyo, matokeo yake ni kuibuka kwa mikanganyiko na sintofahamu katika jamii.

Mara zote Rais Magufuli anapozungumza na wasaidizi wake huwataka watende haki kwa wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote. Alipozungumza na watendaji wa kata alisisitiza sana suala la uadilifu na haki kwa wananchi.

Pamoja na kurejea mwito au maelekezo hayo kila anapopata nafasi za kuzungumza, bado tatizo la wananchi kupata haki zao kwa wakati ni kubwa. Kwanini haki ipatikane pale tu rais anapoagiza? Kwanini usiwe ndiyo utaratibu wa kila mtumishi wa umma kwa wakati wote?

Tunaelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wiki chache zijazo. Dalili za kupunguza uonevu katika nchi yetu zinaonekana. Kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli na wasaidizi wake kwenye suala hili inaonekana.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndiyo uchaguzi wa tija kwa wananchi kuanzia ngazi ya chini kabisa. Endapo wananchi watafanya makosa kwa kuchagua viongozi wasiowasaidia kumaliza kero zinazowakabili, tusitarajie muujiza.

Wenyeviti wa vitongoji, mitaa na vijiji ni viungo muhimu sana katika kustawisha au kufifisha haki za wananchi. Kwa maneno mengine ni kuwa machozi ya wanyonge aliyosema rais yatafutika tu endapo watendaji kuanzia kwenye ngazi hizi watatekeleza wajibu wao kwa haki.

Uchaguzi wa viongozi katika Serikali za Mitaa ni msingi utakaobeba Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Kama huku kwenye Serikali za Mitaa tutakosea, basi itakuwa rahisi pia kukosea kwenye Uchaguzi Mkuu.

Kelele za watu wanaoonewa au kusumbuliwa kwa sababu ya unyonge wao ni nyingi. Zimetanda katika mitaa na vijiji vyote nchini. Migogoro ya ardhi, uharibifu wa mazingira, wananchi kudaiwa fedha wanapohitaji huduma kutoka kwenye ofisi za umma; ni baadhi tu ya mambo yanayoendelea kuwaumiza wananchi.

Kwenye ziara za rais tunashuhudia mamia kwa mamia ya wananchi wakiwa na malalamiko. Wengine husafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine kwa lengo la kumwona rais ili awamalizie kero zinazowakabili. Wanalia dhuluma wanazofanyiwa.

Sijui ni kwanini viongozi wanaosababisha machozi ya wananchi yamwagike mbele ya rais waendelee kukalia viti vya ofisi. Tukubaliane kuwa kiongozi anayeshindwa kutatua kero ya mwananchi iliyo ndani ya uwezo wake amepoteza sifa ya kuendelea kuwa katika ofisi husika.

Si haki kumwachia rais pekee mzigo huu wa kuondoa machozi ya wanyonge. Kila kiongozi atende kazi kadiri ya mwongozo wake wa kazi. Basi, tushiriki sote kwa pamoja kuhakikisha dhamira ya Rais Magufuli ya kutoona machozi ya wanyonge wanaoonewa ikitekelezwa kwa vitendo. Anayeonewa asisite kusimama imara kudai haki kwa mujibu wa taratibu.

582 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!