Daima amani ni tunda la haki. Penye haki amani hutamalaki. Mwenye haki, kwa maana ya kutenda na kutendewa haki, mara zote huwa mpole na mtulivu. Kwa sababu sioni ni kitu gani kitamfanya akose utulivu kama haki yake haijaguswa.

Kwa wakati huu, nina maana mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu, ni kipindi cha kuupima uwezo wetu wa kuimiliki amani tuliyo nayo. Kwa ufupi tunaweza kukiita hiki ni kipindi cha majaribu.

Ni majaribu makubwa sana kwa maana nchi nyingi, hasa hizi za kwetu za Afrika, ambazo nyingi zimeangamia kutokana na kutotendeana haki katika uchaguzi. Watu waliyatafuta madaraka kwa njia yoyote ile halali na haramu!

Ila watu wanaomba sana Mungu atujalie amani. Lakini wengi wetu wanaomba tu amani bila kuangalia amani hutengenezwa na kitu gani. Utasikia watu wakimuomba Mungu awajalie amani bila kueleza ni kwa vipi watailinda na kuitunza amani hiyo.

Wengi hawaelewi kuwa si kazi ya Mungu kulinda amani katika jamii. Hii ni kazi na jukumu la wanajamii wenyewe. Kama wakitaka amani, basi wanalazimika kufanya yale ambayo yatawezesha amani kudumu, lakini kama wasipotaka amani, basi watafanya yale ambayo yanafukuza amani. Hilo ndilo linaleta tofauti katika jamii mbalimbali, nyingine zikiwa na amani na nyingine zikidumu katika vurugu na mapigano.

Siri ni moja tu, wale walio katika amani wamehakikisha haki imetendeka katika jamii. Maana bila haki kuitunza amani ni muali. Amani haiwezi kujengeka mahali ambako hakuna haki.

Kwa namna iliyo kubwa, kitu ambacho tungekuwa tunakitafuta kuliko vyote ni haki. Kwa kutendeana haki, kazi ya kuitafuta amani haiwi kubwa sana, kwa sababu pakishatendeka haki, amani inajileta yenyewe. Kwa hiyo, tunapoingia katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu, jambo la kusisitiza kwa vyama vyote vya siasa vinavyojiandaa kushiriki uchaguzi huo ni kutendeana haki.

Kinyume cha hapo ni lazima yafanyike maandalizi makubwa yanayoitwa ni ya kulinda amani wakati amani hailindwi na kitu chochote zaidi ya haki.

Tungekuwa tunaelewa kwamba hakutakuwepo na wizi wa kura au kufanyiana hiyana yoyote wakati wa uchaguzi, basi kusingekuwepo na tishio lolote la amani ya nchi. Lakini kwa vile kuna hofu ya kutokea kwa wizi wa kura au uchezewaji wa aina yoyote ile kutaka kughushi matokeo ya uchaguzi, kuzuia watu halali kupata haki yao ya kumchagua wamtakaye, hicho ndicho kinakuwa chanzo cha hofu ya kutoweka kwa amani wakati wa uchaguzi.

Kutotendeka kwa haki kunaletwa na hofu ya kutoamini kwamba wapiga kura watamchagua mmojawapo wa wagombea, hususan yule anayekuwa na nguvu za dola, baada ya kutokitekeleza kile alichokiahidi wakati anakabidhiwa nguvu hizo kuu.

Haiwezekani ukatenda haki ikaonekana halafu ukashindwa kujiamini, labda kama unaona ulichokitenda si haki au hakieleweki kama haki. Hapo lazima uwe na shaka na kuanza kuburuza mambo ili yaende kulingana na matakwa yako, na ikishakuwa hivyo haki itakuwa imekosa mahali pa kusimama. Katika kutafuta kuisimamisha haki wakati wapo wanaotaka isisimame tayari amani itakuwa imehama.

Katika mabishano ya kutaka haki ipewe nafasi yake na wengine wakitaka haki isahaulike mapigano yanaweza kujitokeza.

Hapo ndipo tunatakiwa kuona kuwa haki ndilo jambo muhimu katika kuendeleza amani, yeyote anayeimba amani bila kukumbuka haki ajue anaimba wimbo usio na vina na haitakaa ieleweke huo ni wimbo wa aina gani hata kama utakuwa na mdundo mkubwa kiasi gani!

Hivyo tunapokaribia Uchaguzi Mkuu kila mmoja wetu angejitahidi kuimba wimbo mmoja tu wa haki. Kwa mtindo huo neno amani litajitokeza bila kupigiwa parapanda. Kwa mantiki hii ndipo wengine wanataja Tume Huru ya Uchaguzi.

Nimesikia maneno mengi watu wakijigamba kwamba watayakubali matokeo yoyote bila pingamizi. Lakini ninadhani matokeo yasiyo na upindishaji wowote. Haiji akilini mwangu kuwa wapo ambao wako tayari kuyakubali matokeo yanayoonekana ni yakupikwa ili yakamnufaishe fulani.

Na kwa jinsi ninavyoona haki ni kitu ambacho kimeshikiliwa na Chama tawala, CCM, kwa sababu hakuna chama kingine kinachoonyesha kuishikilia haki kama chama hicho tawala.

Neno amani linaweza kutajwa na kila chama, isipokuwa neno haki ndilo tunalitazama kwa chama kilicho na mamlaka. Ndiyo, vyama vyote vinaweza kulitamka neno hilo lakini chama pekee kinachopaswa kulitekeleza ni kile kilichopo madarakani.

Na kwa vile tangu mwanzo nimesema kwamba amani ni tunda la haki, basi tunatakiwa tuone kama CCM iko tayari kutuletea amani kwa kuitanguliza haki katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.

Yapo mambo tunayoweza kuyatazama na kukiona nilichokilenga hapa, rais ambaye ndiye mwenyekiti wa CCM,  alizuia mikutano ya kisiasa kwa vyama vyote mpaka wakati wa uchaguzi ambao ndio huu, lakini kwa kipindi chote hicho chama tawala kimekuwa kikifanya mikutano!

Kwa maana hiyo ni kwamba vilivyozuiwa visifanye mikutano ni vyama vya upinzani. Kweli hiyo ni haki? Mambo kama hayo na mengine ni viashiria vya ukosefu wa amani. Ingebidi tujiepushe navyo.

[email protected]

0654 031 701

By Jamhuri