Huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Tutapata fursa nyingine ya kuwachagua viongozi wa kuendesha gurudumu letu la maendeleo kwa miaka mitano ijayo. 

Hapa nchini tunasema demokrasia ya kupokezana vijiti kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu. Mwaka huu tutachagua tena madiwani katika halmashauri zetu, wabunge na rais.

Ni matakwa ya Katiba kuchagua viongozi kila baada ya kipindi fulani, na kwetu sisi Watanzania huu umekuwa ni utamaduni wetu tangu tulipoanza kuchaguana mwaka ule wa 1958/59.

Nimepata kuandika huko nyuma juu ya haja ya kuwa na elimu ya uraia kwa wapiga kura na kwa wagombea. Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) imepata kukaribisha taasisi zinazotaka kutoa elimu namna hiyo kwa wapiga kura hapa nchini ziombe nafasi ya kufanya hivyo kwa tume kati ya Januari 15 hadi 31 mwaka huu ili tume iweze kuratibu elimu hiyo kwa wapiga kura ili uchaguzi wetu mwaka huu uende vizuri.

Katika historia ya mambo haya ya uchanguzi kumewahi kutokea ubabe katika kampeni au baada ya uchaguzi ukawepo utawala wa kibabe, hivyo kuwafanya wananchi kukosa ile raha ya utawala bora uliokusudiwa kwa huo uchaguzi wa kidemokrasia.

Ningependa kwanza nilitafsiri hili neno ubabe kabla sijaendelea na mada yangu. Tukiangalia katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya TUKI toleo la 3 uk. 584 pale neno ‘ubabe’ limeonyeshwa kuwa na maana ya ‘hali ya kutumia mabavu wakati wa kufanya jambo fulani’.

Tukienda kwenye ile kamusi ya Kiswahili – Kiingereza ya TUKI toleo la 2 kwenye uk. 495 limetafsiriwa tu kama – ‘bruteness, strongness, heroism”. 

Tuendelee sasa na neno ‘bruteness’ kwa Kiswahili sanifu lina maana ya ‘ukatili’, ‘unyama’, ‘mabavu’.

Baada ya kulijua vizuri hili neno ubabe, sasa naona nijieleze kuhusu mtazamo wangu katika siasa za nchi yetu.

Hili suala la ubabe limekuwapo tangu enzi za Wayahudi, kwa hiyo si jambo la ajabu, bali ni tabia ya kawaida kwa binadamu wapendao kutumia vibaya nguvu zao za kimwili. Tulipokuwa shuleni tukisoma enzi zetu zile, matumizi ya nguvu ya ziada tuliyaita kwa Kiingereza ‘the use of surplus energy’ (matumizi ya nguvu za ziada). 

Hii ilionekana pale vijana walipokuwa wakichapana makonde baada ya kuudhiana. Tukiwaambia “you have used your surplus energy properly” au “you have spent your surplus energy properly” (umetumia vema nguvu zako za ziada)Hiyo ni hali yakutumia mabavu kupata unachokitaka na kuridhia roho yako.

Kwa lugha za mitaani neno hili ubabe linajulikana kama kutunishiana misuli au kupimana nguvu za mwili. Lakini huko kutunishiana misuli ni tabia ya kutumia nguvu ili kupata unachotaka. Wenye tabia namna hii daima huwa waporaji, wakabaji na ni watu wasioweza kutawala silika zao.

Kwa wanyama kule msituni inatumika kanuni ya kimazingira inayoitwa kwa Kiingereza “the rule of the jungle”, yaani kuishi kwa mabavu – kwa lugha za misitu, “the survival of the fittest” (mwenye nguvu mpishe)Penye ustaarabu, hakuna utawala wa kutumia mabavu, ndiyo maana kuna uchaguzi wa kidemokrasia. Lakini hapa duniani wametokea watawala walioonyesha ubabe.

Sote tunaona namna wanyama (hasa madume) wanavyopigana kutafuta kumiliki kundi la mitamba. Swala, nyumbu, simba hata majogoo katika kaya zetu tunaona jinsi wanavyopigana mara kwa mara ili kudhihirisha mwenye nguvu anamiliki kundi.

Upo mtandao mmoja hapa nchini, unatumia tangazo lisemalo “mwenye nguvu mpishe”. Mtandao ule umetumia picha za vijibwa kadhaa vimelizunguka jibwa kubwa, kwa hofu na woga. Vijibwa vile vimefyata mikia yao pale, jibwa lilipowabwatukia kwa maneno “mpisheni au mtakiona.” Tangazo hili ni uthibitisho wa “the survival of the fittest” pale vijibwa vyote vile havina uhakika wa maisha yao.

Naona mtandao ule ulitaka kujidhihirishia tu ule uwezo wake mkubwa wa kuwafikia watu wengi, ndiyo maana ukasema, “anayeongoza mpishe!” ukweli wenyewe ni kuwa “mwenye nguvu mpishe”.

Ubabe wa wanyama

Kwetu sisi wanadamu, ubabe umeonekana tangu pale mataifa yalipokuwa yanaanzisha vita ili kuteka na kutawala taifa jingine au kabila jingine dhaifu. Hilo tunaliona hasa katika Biblia pale Goliath alipokuwa anawanyanyasa Waisraeli. Hadithi yenyewe inasema hivi: Enzi za Waisraeli, ubabe ulijitokeza wakati wa ile vita kati ya Wafilisti na Waisraeli. Alijitokeza mbabe mmoja, jitu kubwa na la majigambo lililoitwa Goliath wa Gathi. Hili jitu Mfilisti lilijigamba kwa kusema “nayatukana leo majeshi ya Israeli nipeni mtu tupigane.” (1 Sam: 17:10).

Kwa ubabe wake, Waisraeli, wakiwa chini ya utawaka wa Sauli wakagwaya, wakifadhaika na kuogopa sana. (1 Sam. 17:11). Hawakujitokeza kupigana naye.

Kumbe ubabe ule wa Goliath ulikomeshwa na kijana mdogo Mwisraeli aliyeitwa Daudi mwana wa Yese. Majigambo na kejeli za mara kwa mara za Goliath kwa Waisraeli zilimkera kijana Daudi ndipo akathubutu kuomba kwa wakuu wa jeshi la Israeli wamruhusu akapambane na jitu lile la Wafilisti. Waisraeli hawakumwamini kijana Daudi.

Siku moja kijana Daudi alipomwomba Sauli ridhaa ili akapambane na lile jitu Goliath alisema: “Mtumishi wako alimuua simba na dubu pia, na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai…” (1 Sam. 17:36). Hapo akakubaliwa, lakini mimi ninasema kukubaliwa kule kulikuwa kwa shingo upande.

Kwa kufupisha hii hadithi ndefu ya Daudi na Goliath, kijana Daudi aliruhusiwa kwenda kupambana na lile dude Goliath lenye majigambo. Tunasoma maneno haya: “Ikawa hapo Mfilisti alipojiinua akaenda kumkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio kulikimbia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso, jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti akamuua, walakini, Daudi hakuwa na upanga mikononi mwake.” (1 Sam:17:48-51).

Huo ni mfano mmoja wa ubabe, dharau na kejeli vinavyoshindwa katika mapambano. Iko mifano mingi kuonyesha kuwa ubabe hauna tija hapa duniani.

Mfano hai katika miaka yetu hii ni ule wa ubabe wa Adolf Hilter wa Ujerumani (1939). Yeye alidharau vitaifa vya Ulaya kama Poland, Uholanzi, Ubelgiji na Ufaransa na hata Uingereza. Kwa ubabe wake tu akavamia Poland, akavamia Uholanzi, Ufaransa na hata Uingereza katika ile Vita Kuu ya II ya Dunia (1939 – 1945). Baba na babu zetu hapa Tanganyika walishiriki kama askari –  KAR. 

Kumbe Marekani na Urusi wenye nguvu kubwa zaidi yake wakihofia athari za ubabe wa Hilter wakaingia vitani na wakamtwanga vizuri Hilter na kumfutilia mbali duniani.

Mwaka 1978 jirani yetu Iddi Amin Dada naye alionyesha ubabe wa hali ya juu alipovamia Kagera na kusema: “Mpaka halisi sasa ni ule Mto wa Kagera”, eti pande lote la nchi ya Tanzania kaskazini mwa Mto Kagera ni Uganda. Watanzania tunajua ubabe ule ulivyokomeshwa na Mwalimu Julius Nyerere mpaka Amini aliikimbia nchi yake.

Lakini mada yangu hapa imelenga kwa ubabe wa kisiasa, hususan ni kuhusiana na uchaguzi. Wakati wa kampeni ndipo vituko vya ubabe vinajitokeza.  Watu wako tayari kutumia siasa za kutupiana maneno ya kukebehiana na kadhalika ili mradi wapate kura waingie kwenye halmashauri za wilaya zao au waukwae ubunge au hata wawe marais katika nchi.

Wababe wengi wanapoongea wanafoka huku povu likiwatoka vinywani na mishipa ya kichwani au shingoni inavimba karibu ipasuke.

Nchini Tanganyika mtu wa kwanza kutumia siasa ya ubabe alikuwa Gavana Edward Twinning. Huyu hakupenda hata kidogo kusikia habari za Chama cha siasa cha TANU. Alifunga matawi kadhaa ya TANU kule Musoma, Geita, Mahenge na kwingineko. Aliwakamata viongozi kadhaa wa siasa akawashikisha adabu kwa kuwashtaki mahakamani. Mathalani, Rais wa TANU, Julius Nyerere na wazee kama akina Migeyo, akina Chifu Makongoro na kadhalika, waliwahi kushitakiwa.

Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa JWTZ

By Jamhuri