Home Makala Tuwe na ushujaa wa kweli na nasaha

Tuwe na ushujaa wa kweli na nasaha

by Jamhuri

Ama kweli kuna njama za kuendeleza kufisidi uchumi wa Mtanzania daima dumu. Njama hizo si ndogo ni kubwa na zinatekelezwa usiku na mchana sehemu mbalimbali nchini, Afrika na duniani kote.
Nimeanza na msemo huo wa kufisidi uchumi wa Mtanzania kwa nia ya kuangalia utu wetu Watanzania unavyodhalilishwa badala ya kuheshimiwa kutokana na rasilimali tulizonazo, ambazo tumezipokea kutoka nchi ya Tanganyika na Zanzibar.

Watanganyika na Wazanzibari walipounganisha nchi zao mnamo Aprili 26, 1964, walikuwa na lengo la kuunganisha jamii hizo kwa nia ya kuweka umoja kutokana na matukio ya kihistoria na kujenga mfumo wa uchumi na utamaduni wetu chini ya Serikali moja ya Muungano.
Tangu awamu ya kwanza hadi hii ya tano, Serikali yetu katika jitihada zake za kujenga Taifa huru, tulivu na tajiri kwa wananchi wake, linapata misukosuko ya kisiasa, uharibifu wa utamaduni na ufisadi wa uchumi wa Taifa kutokana na baadhi ya wananchi wenyewe.

Mapambano hayo yanayotokea kati ya Serikali na baadhi ya raia wake wasio waaminifu, malipyoto na wahujumu uchumi waliyomo ndani na nje ya nchi ni makubwa. Ili Serikali iweze kushinda ni lazima wananchi na raia waaminifu washiriki mapambano haya.
Wanaohitajika ni wazalendo, wakweli, waaminifu na wajasiri wa moyo na matendo kwa maana ya ushujaa. Kwani “haja ikishughulikiwa kwa matendo hupatikana upesi, lakini ikishughulikiwa kwa maneno huchelewa kama sadaka.” (Shaaban Robert mwana fasihi).
Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, imedhamiria kupambana na wahujumu uchumi wa Taifa kwa matendo. Wananchi hatuna budi kushirikiana na Serikali katika hili kwa sababu mali inayoibwa na kufisidiwa ni yetu Watanzania.

Naamini Watanzania wote; kila mmoja anahitaji kuishi maisha bora kwa maana ya kuishi mahali pazuri; kula chakula kizuri na kuvaa mavazi mazuri. Mambo haya yanahitaji wajibu na uwezo wa mtu kufanya kazi halali na kuwa shujaa katika kuhifadhi na kulinda rasilimali za Taifa.
Yule Mtanzania aliyetoa madini yetu na akapewa ‘Pick -Up Truck’ – gari dogo la kubebea mizigo, na wahujumu uchumi inawezekana alitafuta maisha bora. Ukweli mwenzetu hakututhamini. La haula! Sina uhakika iwapo gari hilo bado analimiliki.

Rais Magufuli alipokuwa anazindua mradi wa maji katika Kijiji cha Nyamazugo, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wiki iliyopita, alirudia kauli yake ya mara kwa mara ya kututaka Watanzania tumuombee mema kwa Mwenyezi Mungu apate ushujaa wa kupambana na vita hii kubwa ya uchumi na tumuunge mkono kwa matendo.
Naomba kwanza ifahamike kwamba Wanafasihi na Wanafalsafa wanasema kuwa ushujaa ni husuni kubwa na hazina bora ya kudumishwa. Ushujaa kwa mtu ni ngao, kwa nchi ni tegemeo, na kwa taifa ni uwezo. Ndiyo maana Rais Magufuli anatuomba tushirikiane naye.

Inaelezwa ziko namna mbili za ushujaa ambazo hazina budi kufikiriwa mbalimbali siyo pamoja. Ushujaa wa nguvu na silaha, na namna ya pili ni ushujaa wa kweli na nasaha. Watanzania wenzangu hebu tuangalie nadharia hii kwa makini.
“Kwa ushujaa wa kwanza wanadamu huipata amani ya kitambo na fahari ya kifauongo – ule mmea usiohimili kuguswa – lakini hufuatwa na vita mara kwa mara. Kwa ushujaa wa pili, yafikiriwa kwa sababu kabisa kuwa wanadamu wataipata amani ya daima.”(Shaaban Robert).
Ushujaa wa pili wa KWELI NA NASAHA ndiyo ambao marais wetu wote (awamu ya kwanza hadi ya tano) wameutaka na kutunasihi Watanzania tuuzingatie na kuutekeleza katika mapambano yetu ya vita ya uchumi. Hili linawezekana kwa sababu tumepigwa mno hata kutufanya tuonekane kama viziwi na vipofu, ilhali si kweli.
Furaha iliyoje na amani iliyoje Watanzania tukapokea na kujibu kauli ya Rais wetu katka vita hii ya uchumi. Mungu ibariki Tanzania.

You may also like