Kadiri Uchaguzi Mkuu unavyokaribia, ndivyo joto lake linavyozidi kupanda miongoni mwa wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa.

Watanzania wanataka mabadiliko. Ni kwa sababu hiyo, wagombea wakuu wa urais, Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), anasikika akisisitiza mabadiliko.

Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, anasisitiza mabadiliko, lakini akiongeza kionjo cha “Mabadiliko Yaliyo Bora”.

Hii ni habari njema kutoka kwa wagombea wote kwamba wanatambua kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko makubwa, si tu katika maisha yao bali pia kwenye mfumo mzima wa uendeshaji nchi.

Kama kweli Watanzania wanataka mabadiliko, swali la kujiuliza ni je, nao wako tayari kubadilika, au wanataka mabadiliko tu kama miujiza ya kuboresha hali zao za maisha?

Rais Jakaya Kikwete alipokuja na kaulimbiu ya “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania” wapo ambao hadi leo wanauliza kuhusu utekelezaji wa ahadi hiyo. Bila shaka ni wale waliodhani kuwa akishaingia madarakani tu, basi kila kitu kwao kinachohusu maisha yao kingekuwa ‘barabara’.

Kwa namna mhemko wa sasa unavyoonekana miongoni mwa wananchi wengi, taathira zile zile za mwaka 2005 za Maisha Bora kwa Kila Mtanzania zinaelekea kujirudia, pengine kwa kasi na kwa kiwango kikubwa zaidi.

Wanasiasa huwa wanapata wakati mgumu kuwaeleza wapigakura yale yaliyo machungu kuyasikia. Sidhani kama kuna mgombea yeyote awaye kwa sasa aliye tayari kuwaambia wananchi kuwa bila mtu mmoja mmoja kuwa tayari kubadilika katika suala zima la kupigania maisha mazuri, ndoto ya mabadiliko inaweza na kwa kweli itakuwa ngumu!

Kazi kubwa ya Serikali ni kujenga fursa. Kiongozi mkuu wa nchi kazi yake kubwa ni kuhakikisha zinakuwapo fursa nyingi za kuwawezesha wananchi wenyewe – mmoja mmoja au katika vikundi – kuweza kujipatia maisha mazuri.

Ujenzi kama wa barabara, njia za mawasiliano ya simu, usafiri wa anga, usafiri wa reli, usafiri wa meli, na miundombinu mingine ya aina hiyo ndiyo kazi kuu ya Serikali yoyote makini.

Wajibu wa Serikali ni kuhakikisha inapambana na kuondoa urasimu kwenye upatikanaji huduma za msingi za kijamii; lakini wakati huo huo kuhakikisha huduma kama maji, afya na elimu vinapatikana kwa urahisi ili muda mrefu unaopotea sasa kuvisaka vitu hivyo uweze kutumiwa kwenye uzalishaji.

Hakuna shaka kuwa endapo huduma ya maji safi na salama itaenea maeneo mengi ya vijijini na mijini, wananchi, hasa kina mama watatumia fursa hiyo kwenye uzalishaji. Hali ilivyo sasa ni kuwa wapo wengi, hasa watoto ambao wakiamka asubuhi kazi yao ni kuyasaka maji yaliko na kujikuta wakikosa haki ya msingi ya kupata elimu. Kwa hiyo, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha mambo kama haya ya maji yanakuwapo ili muda uliokuwa ukipotea uweze kutumiwa kwenye kusaka elimu na kupambana na mambo mengine ya kimaisha.

Wananchi wanataka mabadiliko ili waone kuwa elimu ya Tanzania inakuwa haki ya kila mtoto na kila mtu mwenye shauku ya kuelimika.

Wale waliosoma kabla au baada yetu watakumbuka kuwa zama hizo mtu kujitambulisha kuwa anasoma shule inayomilikiwa na mtu binafsi au taasisi, ilikuwa fedheha. Wale waliopata nafasi ya kusoma katika sekondari za Serikali waliowaona wenzao waliosoma shule binafsi kama watu waliokuwa hawana uwezo mkubwa wa akili darasani. Hawakuwahukumu hivyo kwa kutambua ufinyu wa nafasi za kujiunga na masomo ya sekondari.

Kwa upande wa afya, watu waliotibiwa katika hospitali binafsi au za taasisi walionekana wanafanya hivyo kwa kupenda wenyewe, na si kwa sababu ya kufuata huduma zilizo bora.

Leo mambo kwenye huduma hizi mbili za – elimu na afya – ni kinyume. Mtoto anayesoma shule ya sekondari ya Serikali anaonekana ni hohehahe. Ndiyo hawa wanaoitwa wa shule za kata! Hata watoto wanaofaulu darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga katika shule za Serikali, wazazi wao hawawapeleki huko, badala yake wanawapeleka shule za binafsi.

Ukimweleza mtu kuwa mgonjwa wako anatibiwa katika zahanati, kituo cha afya au hospitali inayoendeshwa na Serikali, ataingiwa na hofu kuwa mgonjwa wako atapoteza maisha! Utashauriwa mgonjwa wako umpeleke katika hospitali binafsi.

Rais wa Awamu ya Tano anapaswa kubadili mwelekeo huu katika nchi yetu. Anapaswa kurejesha heshima ili shule za umma na hospitali za umma ziwe ndiyo kimbilio la wengi na mahali ambako kila mwananchi anaweza kupaamini.

Hayo ni kwa upande wa Serikali. Kwa upande wa wananchi, tuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha matarajio yetu hayageuki kuwa chanzo cha chuki kwa Serikali ijayo. Hakuna Serikali itakayoleta au kutoa huduma za bure kwa asilimia mia moja.

Tusitarajie kuwa kwa kuendekeza kwetu michezo ya ‘pool’ kuanzia asubuhi hadi usiku wa manane kunaweza kuwa kitu halali; na wakati huo huo tukawa tumekodoa macho kwa Serikali tukitaka itusaidie kutulisha, kusomesha watoto wetu au kutuletea maendeleo kama tunavyoota na kuomba sasa.

Mabadiliko ya kweli katika nchi yetu yataletwa na sisi wananchi wenyewe kuamua kubadilika. Naamini kuwa tutampata rais makini atakayekuwa akitaka kuona sheria za nchi zinafuatwa na kuheshimiwa na kila mmoja wetu.

Baada ya Oktoba 25, na akishaapishwa Rais wa Awamu ya Tano, kusiwepo mwananchi wa kuwa kikwazo katika utii wa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali katika jamii na nchi yetu kwa jumla.

Tunapaswa kuanza kujiandaa kisaikolojia kuupokea uongozi ambao kazi yake kuu ya kwanza itakuwa kuirejesha nchi kwenye mstari wa kuzitii sheria za nchi. Mabadiliko hayawezi kuja kwa kuendelea kuvunja sheria na hivyo kushuhudia mamia ya wananchi wakifa kwa ugonjwa wa kipuuzi wa kipindupindu. Kanuni za usafi zinapaswa zizingatiwe na kila mmoja. Hayo ndiyo mabadiliko.

Mabadiliko yatakuja kwa kupunguza muda wa unywaji pombe na starehe zisizokuwa na ukomo. Maeneo kama Sinza kila mahali kuna baa! Nyumba za starehe zimejengwa hadi kando ya nyumba za ibada, shule, vyuo, hospitali na kadhalika. Tunapaswa kuwa na utitiri wa sehemu za uzalishaji badala ya utaratibu wa sasa wa kuwa na nyumba za starehe kila mahali. Hatuwezi kustarehe kama hatuzalishi; na tukistarehe bila kuzalisha maana yake ndiyo kusema lazima tuwe na Taifa la vibaka, majambazi na matapeli wanaofanya kila wawezalo ili wapate fedha za kustarehe.

Mabadiliko yatakayoletwa na Awamu ya Tano hayatawezekana endapo wananchi wenyewe tunakuwa chachu ya utoaji rushwa kama njia ya mkato ya kupata huduma. Dereva anakamatwa na trafiki, anaona kaonewa kabisa, anababaishwa kwa kutishiwa kuwekwa rumande. Badala ya kukubali kupambana hata kwa kuwaona wakuu wa huyo askari, wanaamua kuyamaliza (eti kuokoa muda) kwa kutoa rushwa. 

Mabadiliko tunayoyalilia kwenye vita dhidi ya rushwa hayatawezekana kama tabia zetu ndani ya uongozi wa Awamu ya Tano zitaendelea kuwa zilezile tulizokuwa nazo ndani ya Awamu ya Nne.

Moja ya mabadiliko yanayopaswa kufanywa na wananchi ili kuunga mkono hayo yatakayoletwa na Serikali ya Awamu ya Tano, ni pamoja na Watanzania kuacha tabia za kulalamika tu. Hali ilivyo sasa ni kwamba kila mmoja – kuanzia Balozi wa Nyumba Kumi hadi Ikulu – analalamika. Hatuwezi kuwa na Taifa lililoendelea kwa kukubali tabia hii ya kulalamika-lalamika.

Kila mmoja wetu katika nafasi yake aanze kuona malalamiko yameshindwa kumaliza kero zinazotukabili na kwa sababu hiyo tuna wajibu wa kuacha kulalamika-lalamika.

Mafuriko yanapotokea mitaani kwetu kwa sababu ya kuziba kwa mitaro tusilalamike. Tutafute chanzo ni nini, na ikiwezekana sisi wenyewe kwa umoja wetu tukikabili kwa lengo la kuondokana na mafuriko.

Wale wananchi wa Manzese majuzi tu waliamua kusaka chanzo cha kutotoweka kwa kipindupindu katika eneo lao. Wakabaini kuwa ni uunganishaji mipira ya maji safi kupitia kwenye mitaro ya maji machafu. Wakaamua kuingia mitaroni kuondoa mipira yote. Bila shaka baada ya muda ugonjwa wa kipindupindu katika eneo lao utakuwa historia. Wamethubutu kujua chanzo cha tatizo na mara moja wakachukua uamuzi. Hawakusubiri kulalamika. Hayo ndiyo mabadiliko yanayopaswa kufanywa na wananchi ili yakiungana na yale ya Serikali, basi tuweze kuwa na Tanzania mpya. 

Mabadiliko yanayokuja yatataka tusimalize matatizo kwa kuyaahirisha au kutafuta visingizio.

Kwa mfano, tatizo la ongezeko la ajali za barabarani hatuwezi kulikabili na kulimaliza kama akili na utashi wetu vitatutuma kila mara tuamini kuwa ajali hizo ni “mapenzi ya Mungu”. Mapenzi gani ya Mungu ya kuondoa uhai wa waja wake? Dereva aendeshe gari lisilokuwa na breki madhubuti, aendeshe akiwa kakesha kwenye viroba, asababishe ajali, watu 40 wafariki dunia, halafu tuhitimishe balaa hili kwa kusema ni mapenzi ya Mungu! Hii hapana. 

Mtu asipotaka kufanya kazi ana sababu gani ya msingi ya kuwaonea wivu wenzake waliofanikiwa kwa kufanya kazi halali? Tunapaswa kuachana na mwenendo huo.

Ndiyo maana naona kuwa mabadiliko ya kweli yatawezekana tu endapo wananchi wenyewe tutaamua kubadilika katika kila idara. Tuwe tayari kuchapa kazi kwa weledi na uadilifu. Tuwe tayari kuzilinda rasilimali za nchi yetu. 

Tuwe tayari kubadilika kwa kushirikiana na vyombo vya dola kubaini wahalifu na wahujumu uchumi. Tuwe tayari kubadilika kwa kupata ujasiri wa kuwakataa viongozi tunaoamini kwa dhati kuwa hawana msaada wa kuleta maendeleo kwa jamii na Taifa letu. Mabadiliko ya kweli yataanzia kwetu sisi wananchi wenyewe.

By Jamhuri