Nilichekwa kwa kumnyenyekea Mwalimu Julius Nyerere

Nyerere2Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuishi karibu na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Nashukuru kwa sababu Watanzania wengi, na walimwengu kwa jumla waliitamani fursa hiyo, lakini hawakuipata moja kwa moja isipokuwa kupitia sauti na pengine maandishi yake.

Mwalimu Nyerere anabaki kuwa mtu wa aina ya pekee ambaye si rahisi kumweleza. Nikiri kuwa sikuwahi kumzoea au kumfahamu. Kila nilipomkaribia, niliona nimekaribiana na binadamu ambaye hazoeleki!

Wakati fulani nakumbuka mimi na ndugu zangu kadhaa tuliokuwa tukisoma maeneo mbalimbali nchini tulikwenda likizo kijijini Butiama. Ilikuwa mwishoni mwa mwaka. Mwalimu alishastaafu urais, lakini akiwa bado Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Siku fulani alipata mgeni- Katibu Mkuu wa CCM, Mzee Rashid Mfaume Kawawa.

Mimi na vijana wenzangu wa wakati huo tukawa tumeketi kando ya barabara sehemu ya makutano ya barabara itokayo Mwitongo (katika makazi yake), eneo maarufu la Stendi.

Basi, nilipoona bendera ikipepea kwenye Land Rover 110, nikajua aliyemo ni Mwalimu na mgeni wake, Mzee Kawawa. Mwalimu alikuwa akimpeleka Mzee Kawawa shambani kwake Mwibanza ili akaone kilimo na ufugaji.

Hapa msomaji atambue kuwa inapozungumzwa kuwa Mwalimu alikuwa mkulima, alikuwa akilima kweli, na si nyampara.

Gari lilipokaribia nilisimama, nikavua kofia kama ishara ya heshima kwa viongozi hao wawili wenye sifa ya kipekee ndani na nje ya nchi yetu.

Kitendo cha mimi kusimama na kuvua kofia kikawa cha ajabu  kwa wenzagu watatu niliokuwa nao. Wakiwa wananicheka, mmoja akahoji: “Yaani Kambarage ndiye anakufanya usimame na uvue kofia?” Nikamjibu: “Ndiyo”. Waliendelea kunishangaa! Haraka haraka nikadhani (na kweli nilikuwa sahihi) wale wenzangu wameniona ni mtu mwoga, nisiyemjua Mwalimu kuwa ni wa kawaida tu, na kwa sababu hiyo nilikuwa “nababaika”!

Niliwajibu kwa kuwaambia kuwa huyu mtu (Mwalimu) si mtu wa kawaida kama walivyodhani kwa mazoea ya kumuona kijijini. Nikahoji; kama marais, wafalme, malkia, matajiri, wasomi, na watu wa kila kada duniani kote wanamheshimu, mimi ni nani hata nisimpe heshima na kumuonesha utii? Wakawa hawana jibu.

Hivi karibuni nimeona video ikionyesha namna Mwalimu alipovyopwa nchini Uingereza wakati wa ziara yake ya kiserikali. Sijui wangapi wameiona video hiyo na kusikia maneno ya mtangazaji. Mtangazaji alisema: “London ni kama imesimama shughuli zote kumshuhudia kiongozi maarufu.”

Sikuwashangaa sana marafiki zangu hao kwa sababu maisha ya Mwalimu Nyerere mahali popote alipokuwa yalimfanya afanane na hapo alipo. Alipokuwa kijijini, maisha yake yalikuwa kama ya mwanakijiji mwingine. Kwa mtu ambaye hakuwahi kuwa karibu na Mwalimu jijini Dar es Salaam, au katika mikutano ya kimataifa sehemu mbalimbali duniani, ilikuwa vigumu sana kumfahamu Mwalimu namna alivyopendwa, alivyonyenyekewa na alivyoheshimiwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja na kuzungumza bila hofu.

Mwalimu alipokuwa Butiama aliishi kama wanakijiji wengi wa kawaida. Hata viatu vyake vilipochanika, vilirekebishwa na fundi wa kawaida kijijini. Nguo zake za shambani zilipopata nyufa zilipelekwa kwa mafundi wa hapo hapo kijijini zikarekebishwa. Kwa mazingira ya aina hiyo ambayo nguo ya mkulima inawekwa kwenye kasha moja na nguo ya mtu anayetajwa kuwa ni maarufu, nani ataamini kuwa Mwalimu ni mtu mashuhuri?

Mwalimu aliendelea kuwa mtu wa kawaida miongoni mwa Watyama (wakazi wa Butiama) wengi hadi alipofariki dunia Oktoba, 1999. Siku ya mazishi yake, mizinga ilipopigwa ikiwa ni heshima kwa mtu aliyepata kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Watyama wengi walisema: “Awe hene omutu wuno yari mukuru!” Yaani:  Hivi kumbe huyu mtu alikuwa mkubwa!”

Nimetoa mifano hii michache ili kuonesha namna ilivyokuwa vigumu kumtambua au kumzoea Mwalimu.

Mwaka 2015 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Tunakaribia kumpata Rais wa Awamu ya Tano. Tunaelekea kwenye Uchaguzi wakati nchi yetu ikikabiliwa na changamoto nyingi. Wale maadui watatu walioainishwa na Mwalimu miaka zaidi ya 50 iliyopita- Ujinga, Maradhi na Umaskini- wakingali wana nguvu kubwa. Watanzania hawajafanikiwa kuwakabili.

Mwalimu Nyerere huyo huyo, aliweza kuainisha mambo manne aliyoamini kuwa ni muhimu kwa Taifa lolote kuyatumia ili kujiletea maendeleo. Mambo hayo ni Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora.

Ukianza na Watu, Tanzania ina watu wa kutosha. Sensa za Watu na Makazi ya mwaka 2012 ilionesha kuwa Watanzania kwa wakati huo walikuwa wanakaribia milioni 45. Ukijumlisha muda uliofanyika sensa, idadi ya waliopinga kuhesabiwa na kasi ya ongezeko la uzazi nchini mwetu, haitashangaza kusikia kuwa idadi hiyo sasa inaelekea kugota kwenye watu milioni 50. Kwa hiyo suala la watu kama nguvu kazi, si tatizo hata kidogo. Watu wapo, wamesoma na wana uwezo katika fani mbalimbali za kimaendeleo.

Ardhi: Tanzania ina ardhi kubwa ya kutosha. Ukubwa wa ardhi ya Tanzania unazidi ukubwa wa ardhi za nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zikiwekwa pamoja. Bado tuna mapori yaliyo wazi na yanayofaa kwa shughuli za kilimo na ufugaji. Licha ya kuwapo kasi kubwa ya upokwaji wa ardhi, bado Tanzania haina uhaba wa rasilimali hiyo. Kwa hiyo suala la ardhi hapa si tatizo hata kidogo.

Siasa Safi: Hapa pengine ni ile siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo kwa muda wote ndicho kinachoongoza nchi yetu. Ukisoma siasa ilivyoanishwa ndani ya Katiba ya CCM na ile sheria mama, yaani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sioni kama kuna tatizo la kukatisha tamaa. Nimepata kuandika kuwa kwangu mimi suala la Katiba mpya si tatizo kubwa sana, maana wapo Watanzania wanaoamini kuwa kwa kupata Katiba mpya, basi mabomba ya nchi hii yatatoa asali na maziwa! Tanzania inazo sheria nyingi na nzuri zinazoipa mamlaka nguvu za kuwashughulikia wezi, mafisadi na wahujumu uchumi. Tuna sheria zinazoruhusu hadi kunyongwa kwa watu wenye makosa ya aina mbalimbali. Kwa hiyo kwangu sioni kama tatizo kubwa ni kukoseakana kwa Katiba mpya.

Pengine kwa wakati huu ambao Tanzania haijulikani inafuata mfumo wa kijamaa au kibepari, ni vema hilo tukalitazama ili kujua tunataka kujenga nchi yenye mwelekeo gani. Kwa sasa mambo yalivyo ni kama hatujui tuendako na kwa maana hiyo hatuoni kama tunapotea!

Tatizo kubwa la Tanzania, hasa kwa uongozi wa Awamu ya Nne unaomaliza muda wake, ni kukosekana kwa Uongozi Bora. Uongozi Bora maana yake ni kusimamia sheria na uwajibikaji katika nchi. Unaweza kuwa na sheria nzuri, Katiba nzuri, lakini ukikosa uongozi bora, ni kazi bure.

Majizi ya mali za umma yanapokwapua fedha halafu uongozi wa nchi ukayaomba majizi hayo yarejeshe fedha ili yaachwe-mambo yaishe, huo si Uongozi Bora. Uongozi wa kuwachekea wezi, mafisadi na wavunja sheria wa aina zote si uongozi unaotakiwa.

Mwalimu Nyerere, aliongoza nchi ikiwa kwenye wakati mgumu sana. Alianza kuongoza nchi ikiwa na madaktari ambao leo hii ni kama madaktari wa kituo cha afya kimoja tu! Nchi haikuwa na wahandisi wala wataalamu wa fani mbalimbali; lakini aliweza kuhakikisha hao hao waliopo wanafanya kazi kwa manufaa ya wananchi wote.

Mwalimu Nyerere alishakiri kuwapo dosari za hapa na pale wakati wa uongozi wake, zikiwamo kama zile za uanzishwaji wa vijiji vya ujamaa, lakini dosari hizo haziondoi ukweli kwamba manufaa yaliyopatikana ni makubwa. Nchi hii isingeweza kufuta ujinga kwa kiwango kile, kusambaza huduma za maji safi na salama, au kuboresha huduma za afya, kama watu wangekuwa wakiishi mbali. Kuwapo kwao pamoja kumesaidia kuwafanya Watanzania wengi wafikiwe na huduma muhimu za kijamii, hasa kwa miaka hiyo.

Awamu zilizofuata zilitangaza kumuenzi Mwalimu Nyerere, kwa kuhakikisha yale mazuri aliyoyasimamia kwa nguvu na akili zake zote, yanaendelezwa. Watanzania na walimwengu wengi wameona hadaa za wanasiasa waliolia na kugalagala kwenye kaburi la Mwalimu wakiahidi kumuenzi.

Kinyume cha ahadi zao, mazuri mengi ya Mwalimu Nyerere yametupwa. Yanakumbukwa machache wakati huu wa Uchaguzi Mkuu. Hata hayo machache, yanachujwa yale ambayo wanasiasa wanaona kwa kuyatumia watawakamata wapigakura ambao wengi bado wanamheshimu.

Mwalimu alihimiza suala la maendeleo kwa wananchi wote. Alipinga kwa maneno na kwa vitendo- pengo kati ya walionacho na wasionacho. Kukosekana kwa uongozi bora kumesababisha kuwapo kwa tofauti kubwa mno kati ya maskini na tajiri. Tena alionya kuwa tofauti hiyo ikiachwa iendelee kukua, amani na mshikamano miongoni mwa wananchi vitatoweka.

Miaka 16 baada ya kifo cha Mwalimu tunaona hatari zinazosababishwa na tofauti ya kipato miongoni mwa Watanzania. Mara zote sichoki kuonya kuwa huu ujenzi wa kuta kuzunguka nyumba za kifahari zilizopatikana kwa njia haramu hauwezi kuzuia kasi ya vibaka wanaohangaika huku na kule kujipatia mlo wa siku. Huwezi kuwa na kundi dogo la watu wanaoifaidi nchi, halafu ukatarajia hasira za makabwela zikagota au zikazuiwa na kuta za Masaki, Oysterbay, Mikocheni au Mbezi Beach. Hakuna ukuta wala uzio wa kuweza kuzuia hasira za maskini wanaosaka kitu cha kuwawezesha kuishi.

Mshindi wa urais mwaka 2015 atambue kuwa ana wajibu mkubwa wa kurejesha misingi ya utu iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere. Ahakikishe watoto wa maskini wanapata stahiki za kijamii kama walivyo watoto wa wanasiasa na matajiri.

Rais ajaye ahakikishe umoja na mshikamano wa Watanzania ndiyo nguzo kuu yenye kuwezesha haya mengine ya kimaendeleo kuweza kufikiwa. Awe tayari kulinda Katiba ya nchi kwa kupinga aina zote za ubaguzi na uonevu.

Si hivyo tu, kuanzia Awamu ya Tano tuone kweli mambo makubwa na mazuri yakifanywa kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu Nyerere na waasisi wengine. Jina la Mwalimu Nyerere ni jina kubwa lenye kustahili kuwa na hadhi ya kipekee.

Iwe fedheha kuruhusu watu kuanzisha shule au vyuo vyenye jina la Mwalimu, lakini kwenye matokeo hizo shule na vyuo vikawa ndivyo vyenye matokeo mabaya zaidi. Mwalimu hakuwa wa mwisho kwenye mambo yake, yawe ya darasani au katika siasa. Jengo linapopewa jina la Mwalimu, liwe jengo la kweli, na si “kiberiti”. Ukumbi unapopewa jina la Mwalimu, uwe ukumbi wa mikutano wenye hadhi inayolingana na jina la Mwalimu.

Lakini hayo yote si kitu, isipokuwa kuhakikisha kizazi cha Watanzania kinapata fursa shuleni na vyuoni, ya kufundishwa falsafa mbalimbali za Mwalimu. Walimwengu wengi walishalijua hilo na haishangazi kuona katika vyuo vyao wakiwafundisha vijana wao maarifa makubwa kutoka kwenye maandiko ya Mwalimu Nyerere. Hakuna aliyempuuza Mwalimu kisha akafanikiwa.