Tuzungumze, tujenge nchi pamoja

DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Wakati wa harakati za kudai uhuru, viongozi wa Kiafrika waliwaunganisha wananchi kwa kuanzisha vyama vya siasa, pamoja na mambo mengine vyama hivyo vilianzishwa kwa madhumuni  ya kutafuta umoja ambao ulikuwa ni silaha namba moja katika hatua mbalimbali za kudai uhuru wa Waafrika kutoka kwa wakoloni.

Katika hatua nyingine, Mei 1963 nchi zilizopata uhuru ziliunda  umoja uliojulikana kwa jina la ‘Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU)’ makao makuu yakiwa Addis Ababa, Ethiopia.

Moja ya madhumuni ya kuanzishwa kwa OAU (sasa Umoja wa Afrika – AU), ni kudumisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa mataifa ya Afrika huku suala la kujitegemea kwa nchi hizo likipewa kipaumbele.

Baada ya uhuru viongozi wazalendo wa Kiafrika, akiwamo Rais wa Kwanza wa Ghana, Dk. Kwame Nkrumah, waliendelea kuhubiri umoja na mshikamano wa mataifa haya kuweza kupambana na ukoloni mamboleo.

Rais huyu kuanzia mwaka 1957 hadi 1966, alisema: “Tukigawanyika tutakuwa dhaifu, tukiungana Afrika itakuwa miongoni mwa mataifa yenye nguvu sana duniani.”

Hata hivyo, mataifa huru ya Afrika yameendelea kukumbwa na migogoro na machafuko ya kisiasa na kusababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe, hali inayozalisha wakimbizi na kusababisha kudorora kwa amani na kuyumba kwa uchumi.

Pamoja na kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa barani Afrika katika miaka ya 1990,  lengo likiwa ni kudumisha na kuimarisha demokrasia, pamoja na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, bado mfumo huo umeendelea kukumbana na vikwazo mbalimbali, vikiwamo ukiukwaji wa haki za binadamu, tamaa ya madaraka  na matumizi mabaya ya rasilimali za bara hili lenye utajiri mkubwa.

Akilihutubia na kuliaga Bunge la Muungano Julai 29, 1985, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alieleza mambo kadhaa kuhusu ujenzi wa taifa.

“Kazi moja muhimu sana kwangu mimi na kwa watu wa nchi hii ambayo nilieleza kwenye hotuba ya uzinduzi Desemba 1962 ilikuwa ni kujenga taifa lililoshikamana, na misingi ya ujenzi  wa taifa letu itakuwa ni uamuzi wa kiungwana wa kuheshimu utu na usawa wa binadamu,” alisisitiza Mwalimu Nyerere.

Mwalimu alisema suala la umoja lilikuwa hoja yake kuu wakati alipohutubia Bunge Aprili 25, 1964 na kuliomba kuridhia makubaliano ya kuunganisha nchi mbili huru za Zanzibar na Tanganyika.

“Ninaamini naweza kusema bila wasiwasi kwamba katika hili la msingi zaidi kati ya malengo yote tuliyokuwa nayo baada ya miaka chini ya 25 ninayo sababu ya kusema kwa fahari, tuna taifa, taifa lililoshikamana, tuna taifa lililojengwa juu ya misingi ya usawa wa binadamu,” alisema Mwalimu Nyerere.

Pamoja na misingi ya demokrasia kubaki ile ile kuwa ni serikali ya watu iliyowekwa madarakani na watu kwa ajili ya watu hao na inaweza kuondolewa na watu hao hao kwa utaratibu wa kura (uhuru) na mara nyingine kwa kulazimishwa.

Ni dhahiri kuwa tafsiri ya dhana ya demokrasia inaweza kutofautiana kutoka nchi moja na nyingine kutegemeana na mazingira, historia, utamaduni na hata mtazamo wa jamii husika.

Juni 1991 akiwa ziarani nchini Brazil, Mwalimu Nyerere alisema demokrasia haiwezi kufananishwa na chupa ya Coca Cola kwa kusema kwamba inapaswa kutokana na mazingira.

“Demokrasia si chupa ya Coca Cola ambayo unaweza kuagiza kutoka nje ya nchi. Demokrasia inapaswa  kutokana na mazingira ya nchi husika,” alibainisha.

Baadhi ya wanaharakati na wanasiasa wameendelea kutumia mwavuli wa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kuleta migogoro ya kisiasa baina ya makundi hayo na vyama vilivyopo madarakani badala ya kudumisha umoja na mahusiano mema ya kisiasa.

Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mei 30, 1995, alizungumza na viongozi wa vyama vya siasa jijini Dar es Salaam alipokuwa katika ziara ya kikazi nchini.

Mandela aliwataka viongozi wa vyama vilivyopata usajili rasmi kufanya kazi na serikali iliyopo madarakani kuwaletea wananchi maendeleo na kuondokana na umaskini uliokithiri.

Jumapili ya Aprili 18, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza vipaumbele vya serikali yake, ikiwa ni pamoja na  kuimarisha misingi ya utoaji haki, usawa, uhuru na demokrasia  na kwamba serikali yake inaboresha  mazingira ya biashara na uwekezaji na kukuza uhusiano wa kimataifa.

Kwa nyakati tofauti Rais Samia ameendelea kusisitiza umoja wa kitaifa, kufanya siasa za kistaarabu, kuheshimiana na kuthaminiana huku akitaka watu wa kada zote kuzungumza lugha moja katika ujenzi wa Taifa la Tanzania.

Katika uzinduzi wa ripoti ya miaka 10 ya mtandao wa utetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC)  Mei 15, mwaka huu Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi  aliwataka watetezi hao  na asasi za kiraia kubadili mtindo wa ufanyaji shughuli zao kutoka harakati za mapambano na badala yake wafanye kazi pamoja na serikali ili watatue changamoto za ukiukwaji wa haki za binadamu.

Alisisitiza kwamba hakuna haja ya harakati za mapambano badala yake kudumisha ushirikiano na serikali kujenga nchi.

“Mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ni Katiba ya Tanzania, ndiyo sheria mama, lazima tujiulize hawa tunaowatetea wanaijua? Ninawapa hii kazi hakikisheni watu wajue haki na wajibu wakielimishwa vizuri watajua haki yao ya kikatiba,” alisema.

Rais Samia amewakaribisha wanahabari ili wazungumze pamoja katika madhumuni ya kujenga nchi pamoja badala ya kuendesha harakati za mapambano ambayo mara nyingine hayana tija kwa taifa na dunia kwa ujumla.

“Kuna watu wanataka kuharibu urithi wa dunia, mnapotetea angalieni lipi lina afadhali hamjakaa mkae mzungumze, ninaliacha kwenu, kuna mengi ya kufanyia kazi, ninawaambia njooni tufanyeni kazi,” alisema.

Mei 7, mwaka jana akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rais Samia alisema serikali yake itaendelea  kufanya mabadiliko mbalimbali katika safu ya uongozi na kwamba anachohitaji ni weledi wa mtu katika nafasi anayopewa, si kuangalia itikadi ya chama cha siasa kabila wala dini yake.

“Lengo letu ni kujenga umoja wa Watanzania na kila Mtanzania anapaswa kuchangia katika ujenzi wa uchumi wa nchi bila kujali tofauti za kijinsia, rangi, dini wala itikadi za kisiasa,” alifafanua Rais Samia.

Katika hatua za kuimarisha umoja wa kitaifa wenye lengo la kujenga nchi kwa pamoja Machi 4, mwaka huu  Rais Samia alikutana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini, Freeman Mbowe, Ikulu jijini Dar es Salaam na kuzungumzia ujenzi wa taifa.

Rais Samia ametaka kuwepo kwa siasa za kuheshimiana na za haki nchini, huku akiahidi kuendeleza msingi wa kujenga taifa moja.

Kwa mujibu wa Rais Samia, jambo kubwa walilozungumza ilikuwa ni kushirikiana kuijenga Tanzania katika kuaminiana kwa misingi ya haki.

“Tunaposimamisha misingi hiyo ya kuaminiana, haki na kuheshimiana ndiyo tutapata fursa nzuri ya kuendesha nchi yetu na kuleta maendeleo ndani ya nchi yetu,” alisema Rais.

Kwa upande wake Mbowe alisema kwamba wamekubaliana kuwa msingi mkubwa wa kujenga taifa katika  maridhiano na umoja unaokubalika ni kusimama katika misingi ya haki.

“Tumekuwa na urafiki wa shaka kati ya vyama vyetu hivi viwili kwa muda mrefu na tumepata madhira mengi hatuhitaji kuyataja zaidi ya kusonga mbele ili tufanye siasa za kistaarabu, kuungana na kusaidia serikali ifanye majukumu yake vizuri,” alisema Mbowe.

Kama hiyo haitoshi, Mei 20, 2022 Rais Samia amekutana na viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, Ikulu jijini Dodoma na kuzungumzia mambo mbalimbali yahusuyo mustakabali wa nchi yetu.

Kikao hicho cha kihistoria pamoja na mambo mengine kilijadili mambo ya kisiasa, demokrasia na maridhiano kadhaa yenye lengo la kuleta ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Akizungumzia madhumuni ya kikao hicho, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema uamuzi wa Chadema kushiriki mazungumzo hayo una baraka za Kamati Kuu na Baraza Kuu na kwamba hawatazuia maoni na mitizamo tofauti ya wanachama wao.

Kwa upande wake Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamidu Shaka, alisema vikao hivyo vinaashiria mwanzo mzuri wa kuendeleza maridhiano ya kisiasa, majadiliano, mapatano na hatimaye kuwa na taifa lenye afya, umoja, amani na mshikamano.

“CCM ipo tayari kuendelea na mijadala ya aina hii yenye lengo la kuendeleza na kuimarisha demokrasia endelevu kwa masilahi mapana ya taifa,” alisema Hamidu.

0755-985966