LONDON

Na Ezekiel Kamwaga

Mwanzoni mwa miaka ya 1980, mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Serikali ya Tanzania alipata safari ya kwenda nchini Yugoslavia kikazi. 

Siku moja kabla hajaondoka, akaitwa Ikulu na aliyekuwa Rais wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere. Akapewa bahasha ya kuifikisha kwa mtu mmoja mashuhuri aliyekuwa ughaibuni wakati huo.

Mtu huyo alikuwa hayati Edward Sokoine – aliyeombwa na Mwalimu aachie uwaziri mkuu akajiangalie afya yake na kuongeza elimu. Akaenda Yugoslavia ya wakati huo. Mwalimu Nyerere,  akimpenda sana Sokoine, aliamua kumtumia ‘kijana wake’ fedha za kujikimu. Nyerere alikuwa kama baba kwa Sokoine na kwake huo ulikuwa ni sehemu ya wajibu wake.

Kiongozi huyo aliyekwenda, sina sababu ya kumtaja jina kwa sasa, alifikisha bahasha ile kwa Sokoine. Na katika mazungumzo yao, mbunge huyo wa zamani wa Monduli aliyekuwa pia akifahamiana vizuri na mgeni wake huyo, alimweleza kuwa Mwalimu Nyerere amemdokeza anataka awe mrithi wake.

Lakini Sokoine alimweleza mwenzake huyo kuwa yuko tayari kubeba jukumu hilo lakini itabidi Mwalimu Nyerere amwachie aiongoze nchi kwa maono yake. Wakati huo, kuondoa Nyerere, hakukuwa na mwanasiasa aliyependwa hapa nchini kuliko Sokoine. Kwa mujibu wa maelezo niliyopewa.

Kwa bahati mbaya, ndoto za Nyerere na Sokoine zilisitishwa siku ile ya Januari 12, 1984 wakati ajali ya gari mkoani Morogoro ilipokatisha maisha ya mwanasiasa huyo aliyekuwa amerejea nchini na kuteuliwa kuwa waziri mkuu. Ziko picha zinazomwonyesha Nyerere akilia hadharani wakati akimuaga Sokoine katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam. Alishindwa kuficha maumivu yake.

Edward mwingine, mbunge

mwingine wa Monduli

Monduli iliyo mkoani Arusha ilikuja kupata mbunge mwingine baadaye. Anaitwa Edward Lowassa, ambaye naye alipata kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania. Kuna mambo yanafanana kuhusu Edward hawa wawili – ukiondoa mfanano wa majina. Kubwa ni tabia ya kutosita kufanya uamuzi. Wakati akitajwa kuwania urais baada ya Jakaya Kikwete – wasifu wake uliokuwa ukitajwa zaidi ni ule wa ‘Maamuzi Magumu.’

Lakini Lowassa aliibuka kuwa mwanasiasa mahiri zaidi kumzidi Sokoine. Ukitaka kufahamu hilo, mahali pazuri pa kuanzia ni kwenye kile kilichokuja kujulikana kama ‘Mtandao’ ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa maoni yangu, hakujawahi kutokea – na sidhani kama itakuja kutokea, timu ya kisiasa iliyosheheni watu wa kada tofauti kama mtandao.

Mtandao huo ulikuwa na wazee kwa vijana, wanawake kwa wanaume, maskini na matajiri, wafanyabiashara na watumishi wa serikali, watumishi wa vyombo vya dola hadi viongozi wa dini. Nashukuru nilikuwa tayari mwandishi wa habari wakati wa kilele cha mtandao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Kama mtandao ulikuwa na gundi, basi ilikuwa ni Lowassa. Na kila mwishoni mwa mwaka, alikuwa akiandaa sherehe za mwisho wa mwaka ambako watu walikwenda kijijini kwake, Ngarash, kula nyama na kufurahia.

Tukiwa Dodoma, mara kadhaa nilikuwa nikipata habari za namna Lowassa alivyokuwa akifanya mikutano na watu mbalimbali – kuanzia wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, maaskofu na makundi mengine, kwa sababu yoyote ile. Stamina yake ya kufanya mikutano mingi haikuwa na mfanowe.

Lakini wawili hao pia walikuwa na tofauti – maisha ya kisiasa ya Lowassa, tangu angali kijana wa miaka 30 yalikuwa yakigubikwa na tuhuma za kuwa na utajiri usio na maelezo. Nilipata kuelezwa hili pia ndilo tatizo alilokuwa nalo Nyerere kwake. Umashuhuri wa Sokoine ulijengwa kwenye dhana ya usafi. Kulikuwa na maneno kwamba ana jozi zisizozidi tatu za viatu.

Haukuwa na ukweli, kwa sababu – kulinganisha na Watanzania wengi, Sokoine hakuwa lofa wala kuwa na jozi chache za viatu. Lakini ilikuwa dhana na ndiyo alikwenda nayo kaburini.

Ilikuwa wazi kwamba Lowassa alikuwa anakwenda kumrithi Kikwete katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 hadi 2007. Mkasa wa kisiasa wa Richmond, ukawa mwanzo wa kushuka kwa Lowassa na ingawa alitoa upinzani mkali kwa John Magufuli mwaka 2015, kazi ilikuwa nzito kwake. Bila Richmond, na kama angegombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM mwaka 2015, bila shaka Lowassa angekuwa Rais wa Tanzania.

Nampenda Abdulrahman

Lowassa na Sokoine walitokea Monduli lakini – kwa sadfa tu, Abdulrahman Kinana; mwanasiasa mwingine kutoka Arusha aliyepata kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, alipata mafunzo ya kijeshi na kuwa mkufunzi katika Chuo cha Kijeshi cha Monduli mkoani humo.

Siku moja, rafiki yangu marehemu Godfrey Dilunga (amewahi kuwa Mhariri wa Gazeti hili la JAMHURI), alipata kunisimulia kuhusu mazungumzo yake na aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale – Mwiru. Siku hiyo, Kingunge alimweleza Dilunga kuwa katika vijana waliokulia na kulelewa na chama hicho – vijana watatu walikuwa wa kipekee; Kikwete, Lowassa na Kinana. Kingunge alimwambia Dilunga kwamba yeyote kati yao angeweza kuwa Rais wa Tanzania na taifa likabaki salama.

Nyerere alikuwa na maoni kama ya Kingunge mwanzoni lakini alikuja kubadilika baada ya kupewa taarifa kuhusu mali za Lowassa. Jambo moja ambalo Kingunge amewahi kuambiwa na Mwalimu Nyerere ni kwamba shida pekee ya Kinana ni kwamba watu wangembagua kwa sababu ya asili yake ya Kisomali. Kwa maneno ya Kingunge, Mwalimu alimwambia: “Nampenda Abdulrahman, lakini atapata shida.”

Na woga huu wa Mwalimu ulitiwa nguvu na namna wana CCM walivyoanza kumbagua Dk. Salim Ahmed Salim kuwa ni Mwarabu mara tu ilipoonekana anaandaliwa kuwa Rais.

Ilikuwa wazi, kwa Mwalimu, kwamba siku ambayo ingeonekana au Kinana kutangaza tu kuwa anataka urais, ndiyo siku mashambulizi na ubaguzi ungeanza.

Chukulia mfano mdogo wa Hussein Bashe. Alikuwa na sifa zote za Utanzania hadi alipotaka kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM). Hapo ikaibuka mizengwe yote kuhusu uraia wake. Sina shaka yoyote kuwa ikifika wakati akatangaza nia ya kuwania urais, tutasikia maneno mengine wakati huo. Lakini huu ni mjadala wa siku nyingine.

Katika wanasiasa hao watatu wa Arusha, naamini Kinana angefaa zaidi kuwa Rais kuliko wawili hao. Kila nikisimuliwa habari za Sokoine, namwona mtu anayefanana na Magufuli. Nina kila sababu za kuamini kwamba endapo Sokoine angefanikiwa kuwa Rais, kuna watu ‘wangelimia meno’, nikimnukuu Magufuli.

Sokoine mwenyewe alijua hilo na ndiyo sababu alikuwa na wasiwasi kwamba pengine Mwalimu Nyerere angegombana naye baadaye. Ndiyo sababu alipanga kumweleza Mwalimu kuwa kama anamtaka yeye – basi amwache aongoze kwa namna yake.

Lowassa angeweza pia kuwa Rais mzuri. Hata hivyo, binafsi nilikuwa na shaka pia na urais wake. Kuna nyakati alikuwa na dalili za ‘Umagufuli’ kama alivyokuwa akijieleza kama mtu wa kufanya ‘maamuzi magumu’.

Yeye binafsi alijua hilo kuhusu mimi na nakumbuka wakati mmoja mwaka 2014 alipata kuniita nyumbani kwake Dodoma na mojawapo ya maswali aliyoniuliza lilikuwa ni; “Kwa nini hunipendi?”

Nilimwambia kwamba sikuwa na chuki naye binafsi isipokuwa nilidhani kwa wakati ule kulikuwa na wagombea waliokuwa na sifa nilizotaka kuliko za kwake. Hatukugombana.

Kinyume chao, Kinana ni mtulivu na mwenye vipaji vingi. Pamoja na kuwa mwanasiasa – lakini unaweza kumweka kwenye kundi la wanadiplomasia, wafanyabiashara na watu wachapakazi na bado ‘akafiti’ bila shida. 

Mara zote ninaamini Tanzania inahitaji kiongozi mchapakazi, msikilizaji, mwenye maono na anayejua biashara. Kinana anazo sifa hizo lakini hakuwahi kujiweka katika nafasi ya kufikiriwa kama Rais. Labda hakutaka ‘kupata shida’ ambayo Nyerere aliwahi kumdokeza Kingunge.

Kizazi cha dhahabu

Ni ajabu kwamba pamoja na kumtoa Sokoine, Lowassa na Kinana, Arusha haikufanikiwa kutupa Rais wa Tanzania. Mikoa michache ya nchini imefanikiwa kutoa wanasiasa wa viwango hivi vya Arusha na kutoka kapa.

Sina shaka kwamba wanasiasa wawili mahiri kutoka Pwani walikuwa ni Ali Hassan Mwinyi na Kikwete na wote wamekuwa marais.

Sidhani kama Mtwara imewahi kutoa mtu wa aina ya Benjamin Mkapa na hatimaye akaja kuwa Rais wetu. Dk. Salim alikaribia kuwa Rais wa kwanza kutoka Zanzibar lakini ‘akapata shida’ na ikashindikana. Lakini unaweza kusema kwamba Tanzania ndiyo iliyopoteza kwa kutokuwa na Rais wa aina yake katika miaka ya 1980.

Lakini Unguja sasa imetoa Rais – Samia Suluhu Hassan, hata kama ni katika mazingira ambayo hakuna aliyetarajia. Leo Unguja imeweka historia kwamba sasa ina Rais na si mwanasiasa mdogo, kwa sababu yuko katika Kamati Kuu ya CCM kwa takriban miaka 20 sasa.

Ni bahati mbaya kwamba Arusha haikufanikiwa kutupa Rais wakati wa kizazi chake cha dhahabu. Kila nikiitazama Arusha ya sasa, sioni kama itakuja kupata wanasiasa wa aina ya Sokoine, Lowassa na Kinana katika miaka ya karibuni.

Labda hii ni zamu ya mikoa mingine. Na naiona mikoa miwili mitatu ikiwa ina aina ya wanasiasa unaoweza kusema wanaweza kufanya kitu kwa nchi yetu kama wakifanikisha ndoto zao za urais.

Lakini huo ni mjadala wa siku nyingine. Leo, nilikuwa naililia Arusha.

Mwandishi wa makala hii (imechapwa kwa mara ya kwanza katika tovuti ya Udadisi) kwa sasa ni mwanafunzi anayesomea Masuala ya Siasa za Afrika katika Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS). Amewahi kuwa mhariri wa magazeti kadhaa ya Tanzania. Anapatikana kupitia email: [email protected].

By Jamhuri