Wiki iliyopita katika toleo hili la Uamuzi wa Busara tulisoma jinsi watu wanavyolinganisha hali ya kupata uhuru na hali ilivyokuwa kipindi cha mkoloni. Wiki hii ni mwendelezo wa tulipoishia. Endelea…

Azimio la Arusha ni jibu la aina ya maswali. Azimio la Arusha linataka kupunguza tofauti iliyopo na iliyokuwa inaongezeka siku hata siku. Azimio la Arusha halitaki viongozi wanaojifananisha na wakoloni na kuotesha mirija ya kunyonya wananchi.

Ndiyo maana viongozi wenyewe wakajiwekea masharti ya uongozi ili kuhakikisha kuwa kiongozi atafanya ile kazi ambayo ametumwa na wananchi. Lakini yote hayo yasingefanyika hadi kulipitisha. Hivyo, uongozi bora wa TANU hauna budi kupewa heko kwa kukubali kulipitisha, maana wangeweza kukataa. 

Viongozi wetu wa chama chetu kitukufu cha TANU walikaa chini tangu tarehe 26/1/1967 mpaka tarehe 29/1/1967 na kupitisha azimio ambalo tangu tarehe 5/2/1967 linajulikana kama ni Azimio la Arusha; ni njia ya pekee ya kuleta maendeleo ya wengi katika taifa hili.

Azimio la arusha ni mwokozi wa kila aina ya dhuluma zilizokuwepo na zile ambazo zingezuka za kugandamizana.

Azimio hilo linamzuia bepari, kabaila na makupe kuwanyonya raia huru wa nchi hii, hivyo kumwacha Mtanzania ajitoe katika dhuluma na unyonge kwa kutumia vyombo vyote vya serikali ya nchi yake iliyo huru. 

Kwa kuwa linakata mirija ya wanyonyaji; mabepari na makabaila hawatakaa kimya na kutupigia makofi wakati mirija yao inaondoka. Ndiyo maana lilipotangazwa tu, wanyonyaji hao wakaanza kutoa kauli za kila aina ili kuwazuzua na kuwaghiribu wananchi ili walikatae.

Kwa upande wao, ni bahati mbaya; kwani wananchi wote waliliunga mkono kwa dhati na sasa wanalitekeleza lau kama ni miaka michache tu tangu litangazwe kwa taifa zima. Hila kadha wa kadha zitafanywa na mabepari na makabaila ili lisifanikiwe. Wakishindwa wazi wazi, basi watawatumia vibaraka wao, wengine ni Watanzania sisi wenyewe, ili utekelezaji usiwe kamilifu.

Itatubidi tuwe macho kwa kila hali, na kwa moyo wa imani na siasa yetu: siasa yetu ya ujamaa na kujitegemea itafaulu. Tukae imara — Heko kwa uamuzi huo.

TANU kukubali kuupitisha Mwongozo wa TANU 1971 

Mwongozo wa TANU 1971 ulipitishwa na kutangazwa rasmi na Rais wa TANU Mwalimu J. K. Nyerere tarehe 21/2/1971. Kwa kifupi mwongozo ni tamko la chama chetu kitukufu cha TANU, ambalo linatilia mkazo juu ya uimarishaji na utekelezaji wa Azimio la Arusha, na pia juu ya mapambano ya kujenga heshima ya taifa letu, na heshima ya Mwafrika kwa jumla. 

Shina hasa la mwongozo huu wa TANU 1971 ni juhudi ya chama kupambana na hila za wakoloni katika bidii yao ya kuzuia  mapinduzi na kuenea kwa ujamaa katika Afrika.

Njama za wapinga ujamaa zimeonekana katika uvamizi wa Guinea, 1970, usaliti katika nchi ya Sierra Leone na hivi karibuni kuangushwa kwa serikali ya UPC huko Uganda.

Halmashauri Kuu ya TANU katika kikao chake maalumu mwezi Februari ilifikiria juu ya njia mbalimbali zinazoweza kuimarisha Uhuru wetu, uchumi wetu, siasa yetu na hata fikra pamoja na utamaduni wetu. Katika kufikia mambo hayo, ilionekana dhahiri kwamba njia iliyopo ni kutilia mkazo sana katika ULINZI na USALAMA wa taifa letu, kwa kuufanya umma ushiriki katika ulinzi wa nchi yetu.

Zaidi ya hayo UCHUMI na MAENDELEO ya watu kwa ajili ya watu wenyewe hapana budi uimarishwe zaidi kwa kutekeleza yale yote yaliyomo katika Azimio la Arusha. Umuhimu wa kuwaelimisha wananchi ili waweze kuielewa siasa yao vizuri na kwa nini Bara letu la Afrika linashambuliwa kila mara. 

Mwongozo haukuishia katika kuyaeleza matatizo ya mabeberu na hila zao za kulinyonya bara letu, bali hata wanyonyaji waliomo nchini wamemulikwa na hatua kuchukuliwa. Mfano mmojawapo, majumba yametaifishwa ya wanyonyaji hawa.

Papo hapo onyo limetolewa kwa viongozi wanaojaribu kukwepa masharti ya uongozi. Zaidi ya hayo, wananchi wamefafanuliwa kwa uwazi wajibu wao katika kushiriki kwa mawazo, maelezo na vitendo – kwa kuendesha uchumi wa taifa zima. Hakika Mwongozo umetoa nafasi na wajibu mkubwa kwa kila mtu kuendeleza uchumi wa taifa.

Lakini kabla ya yote ingefaa tugusie kwa kifupi kwa nini mabeberu wanaendelea kutushambulia, hasa sisi tunaotaka kujenga Ujamaa. Na iwapo hiyo ndiyo tabia yao je, tufanyeje ili tushindane nao katika kuondolea mbali unyonyaji wao?

Historia inatueleza wazi kuwa: Mara tu baada ya kuanguka kwa himaya ya Warumi, Bara la Ulaya liliingia katika kipindi cha giza, yaani ‘Dark Ages’. Kipindi hiki kisichokuwa na ustaarabu kilidumu kwa karne nyingi, na wakati huo ukazuka mtindo wa maisha ulioitwa Ukabaila (Feudalism). 

Msingi wa Ukabaila ni ARDHI. Ndiyo kusema Siasa na Uchumi vililingana na mazingira ya umilikaji wa ardhi. Kiini cha shughuli za uchumi kilikuwa vijijini. 

Kidogo kidogo baada ya muda mrefu ukabaila ulizaa ubepari. Hii ilifutwa na mabadiliko makubwa katika mtindo wa kuzalisha mali. Ubepari kama mtindo mpya wa maisha msingi wake mkubwa ni Mtaji.

Yaani rasilimali inayoajiri vibarua kwa kuzalisha mali. Kwa hiyo, kuwa msingi wa ukabaila ni Ardhi na ule wa ubepari ni Mtaji, kiini cha shughuli za uchumi kilitoka mashambani kwenda mijini, kutoka kwenye ardhi kwenda katika mtaji, fedha, mabenki, biashara, uchukuzi, viwanda nk. vyote vikawa mijini. Mabadiliko haya yaliitwa mapinduzi ya viwanda (Industrial Revolution). 

Ubepari una tabia ya kujipanua. Viwanda viliongezeka, vikakua na kadri viwanda vilivyokua ndivyo kadiri mahitaji ya viwanda pia yalivyopanuka. Na mahitaji ya viwanda ni rasilimali ya asili (raw materials) vibarua wa ujira mdogo (cheap labour) na masoko ya kuuzia bidhaa za viwanda (markets).

Hatimaye mahitaji ya viwanda yaliyotajwa juu yanashindwa kutoshelezwa ndani ya mipaka ya nchi inayohusika. Hayana budi yatafutwe nje ya mipaka ya nchi ile. Ubepari unabadilika kuwa ubeberu. Mabepari huenda katika nchi za kigeni kutafuta uhondo wa watumwa, makoloni, masoko, n.k.

Na katika pilikapilika hizo za kujipatia makoloni kunatokea mashindano ambayo yanasababisha vita baina ya nchi za kibeberu ambazo zinakumba hata wale wasiohusika. 

Katika Ulaya na Amerika uchumi wao ulifika kiwango ambacho kilihitaji mtindo mpya wa utumwa – utumwa wa kikoloni.

Ukoloni ni aina mpya ya utumwa uliolingana na mahitaji ya uchumi wa nchi za kibeberu wakati wake. Na kulikuwa na njia mbili za kuvamia koloni. Kwanza, walitumia mikataba ya udanganyifu, na pili walitumia majeshi. 

Ingawa wananchi hujitetea kwa kupigana, lakini hushindwa kwa sababu ya ukosefu wa silaha za kisasa na ukosefu wa umoja miongoni mwao wenyewe. 

Baada ya mkoloni kuvamia nchi mpya, hujitwalia madaraka ya siasa na kubadili utaratibu. 

639 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!