Ufafanuzi muhimu kuhusu usajili wa Acacia

Kwa kutumia kigezo cha usajili, Tanzania tunazo aina kuu mbili za kampuni. Kampuni za ndani (local companies) na kampuni za kigeni (foreign companies).

Kampuni za ndani ni zile zilizoanzishwa hapa nchini na kusajiliwa hapa nchini. Hata kama wanahisa wake wote ni raia wa kigeni kwa sababu tu ya kuanzishwa hapa na kusajiliwa hapa, zinakuwa ni kampuni za ndani.
Kampuni za kigeni ni zile zote zilizoanzishwa na kusajiliwa nje ya Tanzania, lakini zikaanzisha ofisi/biashara/tawi hapa Tanzania. Sheria Na. 12 Sheria ya Makampuni kifungu cha 433 kinasema hivyo. Kampuni kama imeanzishwa nje hata kama wanahisa wake wote ni Watanzania, hapa kwetu hiyo bado ni kampuni ya kigeni.

Kampuni ya ndani inaposajiliwa hupatiwa cheti cha usajili kiitwacho Certificate of Incorporation kwa mujibu wa kifungu cha 15(2) Sheria ya Makampuni. Kampuni ya ndani inapopata cheti hiki, basi usajili wake huwa umekamilika na inatambulika rasmi kama kampuni ya ndani.

Kampuni ya kigeni inaposajiliwa hapa Tanzania hupatiwa cheti kiitwacho Certificate of Compliance kwa mujibu wa kifungu cha 435(1) Sheria ya Makampuni.
Kampuni ya kigeni inapopata cheti hiki, basi usajili wake huwa umekamilika na hutambulika rasmi kama kampuni ya kigeni.
Acacia ni kampuni ya kigeni. Kwa maana kuwa ilianzishwa nje ya Tanzania na kufungua shughuli zake hapa nchini. Kwa hiyo ili ihesabike imesajiliwa Tanzania ilitakiwa kuwa na cheti kiitwacho Certificate of Compliance. Kutokuwa na cheti hiki maana yake ni kuwa haijasajiliwa Tanzania na haitambuliki.

Ni juzi tu nimesikia mjadala BBC SWAHILI wanaojadili wakijiuliza inawezekanaje kampuni kubwa kama hii ikafanya biashara bila usajili? Watanzania wengi pia wanajiuliza swali hili.
Jibu lake ni hili; Acacia ni kampuni tanzu (Subsidiary Company) ya Barrick. Kampuni inakuwa tanzu pale ambako zaidi ya nusu ya hisa zake zinamilikiwa na kampuni nyingine. Ile inayomiliki huitwa holding company na inayomilikiwa huitwa subsidiary company. Kwa hiyo Barick ni holding wakati Acacia ni subsidiary.
Barrick inamiliki hisa za Acacia 63.9%. Kwa kusema hivi maana yake Barrick ndiye mwenye Acacia. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hizi zinahesabika kampuni mbili tofauti na kila moja inabeba wajibu na hatia zake yenyewe (its own responsibilities & liabilities).

Basi, kumbe kilichotokea ni kwamba Acacia walikuwa wakifanya biashara kwa jina la Acacia, lakini wakibebwa na mgongo wa Barrick. Walijificha hapa na wakaweza kuishi bila usajili wa kwao kama wao. Walijibeba kwenye usajili wa Barrick.
Barrick wao wanao usajili, na wanayo Certificate of Compliance ya kwao ambayo tayari wameitoa hadharani. Kwa kuwa hizi ni kampuni mbili tofauti kila moja inatakiwa kuwa na cheti chake kwa mujibu wa kifungu cha 487 Sheria ya Makampuni; na kutokufanya hivyo ni kosa kabisa. Kwa hiyo hivi ndivyo ilivyowezekana kampuni hii kufanya biashara bila usajili miaka hii yote.
Baadhi ya watu wanasema – hapana Acacia hapa Tanzania ilikuwa ikiitwa African Barrick Gold plc kwa hiyo Africa Gold Barrick ndiyo Acacia na kuwa wanacho cheti cha usajili (Certificate of Compliance) chenye jina la African Barrick Gold.
Sawa, lakini tunachosema ni kuwa hawa watu miaka yote wamefanya biashara kwa jina la acacia. Swali ni je, ipo Certificate of Compliance yoyote yenye jina la Acacia? Kwenye rejesta ya Msajili wa Kampuni (BRELA) limo jina Acacia? Hakuna, ipo Barrick. Unafanya biashara kwa jina la Acacia wakati kilichosajiliwa ni Barrick, ni kosa. Basi hiki ndicho kinachoitwa kufanya biashara bila usajili.

Adhabu ya kosa kama hilo ni kifungo jela. Sheria Na.12 Sheria ya Makampuni iliyofanyiwa Marekebisho mwaka 2002, kifungu cha 472 inasema hivyo.
Swali hapa litakuwa je, nani atafungwa jela? Jibu lake ni hili. Ni kweli kuwa kisheria kampuni na wamiliki wake kila mtu ana hatia yake. Kwa maana kuwa kosa la kampuni huwezi kumshitaki mmiliki au mfanyakazi. Halikadhalika, kosa la mmiliki au mfanyakazi huwezi kuishitaki kampuni. Sheria imevifanya hivi kuwa vitu viwili tofauti kabisa.

Kanuni hii huitwa ‘Separate Legal Entity’ na iliingia kwenye sheria duniani mwaka 1897 kupitia hukumu katika kesi maarufu ya Solomon vs Solomon. Kwenye sheria yetu hapa Tanzania kanuni hii iliwekwa na ipo kifungu cha 15(2) Sheria ya Makampuni.
Kumbe basi, kwa msingi wa kanuni hii yatupasa tuishitaki Acacia kama kampuni kwa kuwa kanuni hii inatuzuia kuchanganya wamiliki au wafanyakazi wa kampuni na kampuni yenyewe. Lakini je, Acacia kama kampuni tukiishitaki itafungwaje na itakwenda vipi jela?
Jibu hili hapa. Sheria inasema kwamba kampuni inapofanya udanganyifu, au inapotumika kukwepa majukumu yake ya kimkataba au inapotumika kukwepa kodi, basi inayoshitakiwa si kampuni tena, bali ni mtu yeyote katika kampuni hiyo aliyehusika katika kosa hilo. Yaweza kuwa mkurugenzi, meneja, katibu au mfanyakazi mwingine yeyote wa kampuni husika. Imeamuliwa hivyo katika kesi ya PLASCO vs EFAM LTD, kesi Namba 60/2012 Mahakama Kuu ya Biashara, pia katika kesi ya M.H NASSOR CO. LTD vs RYX OIL CO., kesi Namba 16/2009, Mahakama Kuu ya Biashara, na katika kesi nyingine nyingi.

Kwa hiyo anayepaswa kushitakiwa na kwenda jela ni kila afisa wa Acacia aliyehusika katika kila kosa litakalokuwa limethibitika.

Mwandishi wa makali hii, Bashir Yakub, ni Mwanasheria na anapatikana kupitia namba 0784482959.