Mangula(4)Sisi sote tunajua na tunakubali kwamba Rais John Magufuli ni mchapakazi.

Alijibainisha kwamba ni mchapakazi tangu alipokuwa waziri. Wizara yoyote aliyoshika Dk. Magufuli haikusinzia wala haikulala. Na hakuwahi kuitwa ‘waziri mzigo’.

Lakini pamoja na ukweli wote huo, ni ukweli pia kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana wapo waliomkataa Dk. Magufuli, tena si wachache. Ni vyema tukaendelea kukumbushana kwamba wananchi hawakumkataa Dk. Magufuli; walikikataa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni kweli huko nyuma Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alituaminisha kwamba rais bora atatoka CCM!

Nadhani sasa mambo yamebadilika. Hatuwezi kuaminishwa kwamba rais aliyeondoka madarakani alikuwa bora. Lakini pamoja na hayo watu hawakuikataa CCM tu, waliukataa mfumo mzima wa CCM wa kulindana.

Kwa hiyo, tumeshuhudia mfumo huo ukiendelea au ukifuga maovu kwa sababu tu ya kulindana. Kwa kawaida wanachama wa CCM wakiwamo wabunge hufanya kila juhudi kulinda chama chao na viongozi wao hata pale ubovu unapoonekana waziwazi. Kwa njia hiyo Serikali imeendelea kufuga ufisadi na maovu mengine Tanzania.

Kwa hiyo, katika uchaguzi wa mwaka jana, pamoja na uhodari wa Dk. Magufuli katika kutekeleza majukumu yake, wengi waliona kwamba asingeweza kupambana na mafisadi wakubwa waliomo CCM na kuwachukulia hatua.

Wananchi kadhaa waliona na wanaendelea kuamini kwamba serikali ya wapinzani ingeweza kukomesha ufisadi Tanzania kwa kuwachukulia hatua kali mafisadi walioko ndani ya CCM bila kuwaonea aibu.

Tukitaka kusema kweli hadi sasa Rais Magufuli ameonesha uwezo mkubwa katika kupambana na mafisadi. Lakini anapambana na anawachukulia hatua mafisadi walioko mashirika ya umma. Hajagusa mafisadi wa Serikali ambao ndiyo wakubwa zaidi.

Mafisadi wa Serikali ambao wako wazi kabisa ni wa Akaunti ya Tegeta Escrow. Rais Magufuli asiwaonee aibu wala asiendelee na mafisadi wa Escrow waliolitia aibu Taifa letu.

Akiwanyamazia, wananchi watasema kwa haki kabisa bora wangempeleka Ikulu rais kutoka Kambi ya Upinzani. Angefichua kila kitu. Wapo wanaomini kwamba mhusika mkuu wa Tegeta Escrow ni Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete.

Kwa mambo matatu, Rais huyo mstaafu hawezi kupona katika sakata hili la Tegeta escrow. Kwanza, mgogoro kati ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ulikuwa umetakiwa umalizwe na Mahakama.

Kwa hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) alipotakiwa kutoa fedha hizo awape IPTL, alikataa.

Alipoendelea kuchoshwa akataka Rais atoe uamuzi. Rais akamtumia mtu wake, Prosper Mbenna, kuiandikia barua Hazina kuidhinisha fedha hizo kutolewa. Zikatolewa BoT kupitia benki za Stanbic na Mkombozi.

Pili, Rais huyo mstaafu aliendelea kumtetea mmiliki wa IPTL ambaye hadi leo anaendelea kulipwa fedha ya umma kiasi cha Sh bilioni tano kwa mwezi. Rais Magufuli hajui hilo? Mbona hachukui hatua za kupambana na fisadi huyo ambaye katika nchi nyingine angekuwa ameshughulikiwa?

Tatu, Rais huyo mstaafu aliamuru fedha zote za mgogoro zilizowekwa BoT wapewe IPTL huku akijua kuwa sehemu ya fedha hizo zilikuwa za TANESCO au za umma.

Si bure, Rais huyo mstaafu aone haki ya IPTL kupata fedha hizo zote; na kupoteza fedha zote za umma! Lakini pia zilipatikana habari za kutolewa mabilioni ya shilingi kutoka Benki ya Stanbic ambazo walichotewa watu wengi, wamiwamo watumishi wa Ikulu.

Ilisemekana kwamba mke wa mkubwa mmoja wa Ikulu alichotewa Sh bilioni 5! Lakini pia kuna uwezekano mkubwa kwamba mafisadi wa Ikulu ambao leo huenda wakawa wanamsaidia Rais Magufuli, pia waliochotewa fedha za Escrow. Ikulu ya wakati huo ‘ilioza’ kabisa na hapakuwa mahali patakatifu tena kama Mwalimu Nyerere alivyosema.

Kubwa zaidi tuulizane haki iko wapi? Wakati majina ya wakubwa waliochotewa fedha chache kutoka Benki ya Mkombozi hayakufichwa, kwa nini mafisadi wakubwa wa Ikulu waliochotewa fedha nyingi zaidi kutoka Benki ya Stanbic wameendelea kulindwa na kufichwa hadi leo?

Kwa kifupi, hadi sasa Rais Magufuli anashughulika na majipu madogo madogo. Majipu makubwa (majipu tambazi) yaliyoko serikalini hajayatumbua. Ingawa ni mapema kutoka na muda wake Ikulu, wananchi wangejawa imani zaidi kama wangeona mapapa nao wakishughulikiwa.

Halafu tumesikia kwamba marais wastaafu ambao walipoingia madarakani hawakusita kutaja mali zao, leo baada ya kuondoka madarakani hawataki kutaja mali  walizochuma. Kwa nini? Walihubiri utawala wa sheria na sasa hawafuati sheria. Na hakuna anayewachukulia hatua! Je, wametangaza kimya kimya? Bila shaka wana mali nyingi walizojipatia kifisadi.

Sasa kuna habari kwamba mali zote za mafisadi zinataifishwa. Lakini mali za marais wastaafu hazitaguswa kutokana na sheria inayokataza rais mstaafu kushitakiwa!

Mwizi ni mwizi na fisadi ni fisadi. Ni kukiuka haki kuwachukulia hatua watu fulani kwa kosa fulani huku ukiwaacha watu wengine waliofanya kosa hilo hilo.

Ndiyo maana tuna haki ya kuamini kwamba ufisadi wote katika Tanzania ya leo umeongozwa na Ikulu ya wakati huo na kwa hiyo Rais Magufuli anatakiwa kuwachukulia hatua bila woga. Wakati wa kampeni aliahidi kuwa hatabagua na hatapendelea. Tunaamini atafanya hivyo punde.

Jipu jingine kubwa lililoko serikalini ambalo Rais Magufuli anatakiwa kulitumbua liko Wizara ya Elimu. Viongozi na watendaji wa Wizara ya Elimu wametumia fedha za rada kifisadi. Ni shule chache mno zilizopata madawati kutokana na fedha za rada. Waligeukana wakubwa wa wizara. Fedha za rada zilizotakiwa kununua vitabu ziliwanufaisha wakubwa wa wizara.

Kuna habari kwamba mchapishaji mmoja wa vitabu vilivyoteuliwa, alilipwa Sh bilioni 6 za ziada ambako alitakiwa aiuzie Serikali vitabu vyake vyote.

Akauza vitabu vibovu na leo hana vitabu. Basi, Rais Magufuli atumbue majipu haya yaliyoko serikalini. Ukarimu huanzia nyumbani. Namtakia kila la heri katika utumbuaji majipu.

By Jamhuri