Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), amedhihirisha wazi kuwa yeye ni kiongozi mwenye tamaa ya madaraka iliyopitiliza, tamaa inayomwezesha kuteketeza hata nchi nzima pamoja na wananchi wake ilimradi yeye abaki kuwa kiongozi mkuu. 

Kilichofanya asiweze kutimiza hilo ni kutokuwa na uwezo wa kufanya hivyo, pengine kwa maana ya kutokuwa na jeshi kama walivyowahi kuwa watu kama yeye – Dk. Jonas Savimbi wa Angola, Dk. John Garang wa Sudan Kusini na wengineo wa aina hiyo.

Hebu tumwangalie kidogo mwanatamaa Maalim Seif Shariff Hamad. Maalim Seif alianzia ngazi za chini kisiasa baada ya kuachana na ualimu wa shule, au skuli, kama inavyosemwa kwa upande wa Tanzania Visiwani.

 Alipanda ngazi kupitia nyadhifa mbalimbali zenye hadhi mpaka alipoteuliwa kuwa kiongozi mkubwa kinchi – waziri kiongozi mwaka 1984. Hiyo ni nafasi ya juu sana katika uongozi wa nchi, kwa mtu asiyekuwa mwingi wa tamaa hiyo ni nafasi nyeti sana isiyoweza kumfanya mtu aendelee kuwaka tamaa ya uongozi wa juu kinchi.

Lakini kinyume na hilo, kitendo cha kufanywa waziri kiongozi kikawa kama kimemlambisha asali na hivyo yeye kutamani kuchonga mzinga bila kujali madhara yoyote ya kutamani kufanya hivyo. 

Mtu analamba asali na utamu wake unamsahaulisha ukali wa nyuki, anakuwa kama dubu ambaye utamu wa asali humfanya kuweka kichwa mzingani kulamba asali bila kuelewa madhara anayoweza kuletewa na nyuki! Hiyo ni tamaa iliyopitiliza. Tamaa inayopofua macho, kuziba masikio na kuviza akili.

Tamaa hiyo ndiyo iliyomshawishi Maalim Seif kuvunja maadili ya uongozi wa nchi akiwa bado yuko kwenye chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kulitokea kutokuelewana ndani Halmashauri Kuu ya CCM ambapo yeye aliamua kwenda kwao Pemba na kuwaeleza wananchi mambo yaliyo kinyume cha uamuzi wa chama tawala. Mwaka huo alitimuliwa kwenye nafasi ya uwaziri kiongozi na pia kufutiwa uanachama wake wa CCM. Muda mfupi baadaye aliwekwa kizuizini ili asiendelee kumwaga sumu yake kwa wananchi.

Alipotoka kizuizini akaanzisha chama cha siasa, KAMAHURU, ambacho hata hivyo hakikuwa na sura ya kitaifa, kilikuwa ni chama cha visiwani tu. Sheria ya Vyama vya Siasa ilipoanzishwa tena mwanzoni mwa miaka ya 1990, ilikuwa ikitaka kila chama cha siasa kinachoanzishwa kiwe na sura ya kitaifa, kwa maana ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.

 Ndipo James Mapalala, aliyekuwa ameanzisha chama cha siasa kwa upande wa Tanzania Bara, alipomkaribisha Maalim Seif ili waunganishe vyama vyao na kuunda chama kimoja, Chama cha Wananchi (CUF), kilichokuwa na mwonekano wa kitaifa kwa maana halisi.

Tamaa ya madaraka ya Maalim Seif ilimlazimisha afanye njama za kumpindua Mapalala na hatimaye kumtimua kwenye chama kusudi yeye akimiliki chama hicho peke yake kikiwa kama mali yake binafsi. Viongozi wengine waliobaki kwenye chama hicho wakabaki wanaonekana kama waajiriwa!

 Ikumbukwe tangu wakati huo Maalim Seif ndiye Katibu Mkuu wa CUF, tunaweza kusema yeye ni Katibu Mkuu wa maisha. Wakati fulani alikuwapo Naibu Katibu Mkuu Bara, Wilfred Muganyizi Lwakatare, mpambanaji makini aliyekiwezesha chama hicho kupata jimbo upande wa Bara, Bukoba Mjini, ambako chama hicho kilikuwa hakijulikani kabisa. 

Lakini kwa vile mtu huyo hakuwa Mpemba akafanyiwa majungu mpaka akaondolewa kwenye nafasi hiyo bila kujali yote aliyokifanyia chama hicho. Maana chama hicho kimaneno kinajiweka ni cha kitaifa lakini kiundani, kiusiri, chama hicho kinajiona ni cha Wapemba au cha Kipemba.

Hebu fikiria Chama Cha Mapinduzi kinachowathamini wanachama wake na kuvijali vipaji vyao kimeishakuwa na makatibu wakuu wangapi kwa muda wote huo ambao Maalim Seif amekuwa Katibu Mkuu wa CUF? Ina maana chama hicho cha CUF hakina mtu mwingine anayeimudu nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 20 sasa?

Mwaka 1995 Maalim Seif alipendekezwa na chama chake kugombea urais wa Zanzibar, akagombea na kushindwa na Dk. Salmin Amour wa CCM, Seif hakuyakubali matokeo hayo akadai uchaguzi urudiwe. Haikuwezekana. Mwaka 2000 akagombea tena na kushindwa na Dk. Amani Abeid Karume. Akadai kwamba uchaguzi urudiwe ikashindikana.

 Mwaka 2005 Maalim Seif akagombea tena na kushindwa tena na Dk. Karume. Vilevile hakuyatambua matokeo hayo akataka uchaguzi urudiwe ikashindikana pia.

Mwishoni mwa kipindi cha pili cha Rais Karume, Maalim Seif akakubaliana na Dk. Karume kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hivyo Uchaguzi Mkuu wa 2010 akagombea akielewa kwamba anayo nafasi ya kuupata umakamu wa kwanza wa rais.

Kwa hiyo, hata matokeo yalipoonesha kwamba kashindwa na Dk. Shein wa CCM hakuleta matata sana. Akakubali waunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hicho ndicho kinachoonesha kwamba huko nyuma alikuwa akilalamika kwa ajili ya uchu wa madaraka. Sababu mara zote aliyokuwa akiyalalamikia yalikuwa kama hayo ya 2010. Lakini kwa vile alikuwa amehakikishiwa nafasi kubwa katika uongozi wa nchi akaachana na malalamiko yake.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, 2015, Maalim Seif akagombea tena akiwa na mbinu zilizoambatana na uzoefu wa kugombea mara 5 mfululizo, ni uzoefu mkubwa ambao hakuna mtu mwingine aliye nao katika visiwa hivyo.

 Kwa hiyo, akawa amejipanga kuuvuruga uchaguzi huo kwa namna yoyote ile. Na kweli uchaguzi ukavurugika. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambayo ndiyo yenye mamlaka pekee ya kusimamia na kuendesha uchaguzi, ilipoziona dosari kubwa kwenye uchaguzi huo na kuamua kuufuta na kuahidi kupanga tarehe nyingine ya uchaguzi urudiwe, Maalim Seif akakataa katakata! Anadai uchaguzi haupaswi kufutwa kwa vile ulikuwa sahihi kabisa. Hayo kayasema baada ya kuwa yeye kajitangazia ushindi kinyume na sheria ya uchaguzi inavyoelekeza.

 Swali linakuja kwamba kwa nini mtu ambaye muda wote huko nyuma alikuwa analalamika kwamba uchaguzi urudiwe leo hii ndiye anayekataa kwamba usirudiwe? Kumbe madai yake ya chaguzi zilizopita yalikuwa ni ya kuleta vurugu tu ili kuhakikisha nchi haitawaliki kwa amani na utulivu kisa kakosa madaraka!  Uroho, uchoyo na tamaa ya madaraka aliyo nayo Maalim Seif vinajionesha kwa namna hiyo. Ni kwamba anaamua kwa makusudi kuwachanganya Wazanzibari ili kukidhi kiu yake ya madaraka.

Kwa sasa anadai kashinda, hivyo anachotaka ni kuapishwa. Anapoambiwa uchaguzi urudiwe analikataa katakata jambo hilo. Kama kweli anaamini kwamba uchaguzi uliovurugika ulikuwa sahihi na ulimpa ushindi kinachomfanya ahofu usirudiwe ni kitu gani wakati wapiga kura ni walewale?

 Bilashaka hofu yake inaletwa na ukweli kwamba anachodai kilimpa ushindi kimeishagundulika na hakitajirudia tena. Kitu kisicho na njama chafu hakiwezi kuhofiwa hata kama kinarudiwa mara milioni.

 Hivyo, tamaa ya madaraka ya Maalim Seif isiwache nchi ikaendeshwa kwa namna anavyotaka yeye. Sheria na taratibu za nchi ziachwe zichukue mkondo wake.

1822 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!