DODOMA

Na Mwandishi Wetu

Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala juu ya uhalali wa kuwapo wabunge 19 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kama sehemu ya Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni takriban miezi mitano sasa tangu kuapishwa kwa kundi la wabunge hao wa Viti Maalumu wakiwakilisha Kambi ya Wabunge Walio Wachache linalotekeleza majukumu yake kwa muhula wa mwaka 2020 hadi 2025.

Kwa upande mwingine, wabunge hawa wanawakilisha kundi la wanawake ambalo kwa muda mrefu limekuwa likilalamika kuwa na uwakilishi mdogo ndani ya Bunge, ambalo ni chombo mahususi kwa ajili ya kutunga sheria na kuisimamia serikali katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

Hivyo, pasipo kujali itikadi za vyama, ni dhahiri kuwa uwepo wa wanawake hao ndani ya Bunge ni fursa na faraja kwa wanawake wengine wengi wa Tanzania. 

Faraja hiyo inatokana na ukweli kuwa kupitia nafasi hiyo wataweza kusemea changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wanawake nchini katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.

Ni bahati mbaya kwamba uwepo wa wabunge wa Viti Maalumu wa Chadema bungeni umechukuliwa na baadhi ya watu kama tatizo na si fursa ndani ya chama hicho, wakasahau kuwa kwa kupata wawakilishi, kundi la wanawake watajengewa hoja bungeni na watashirikiana na wabunge wengine kulisaidia taifa kufikia malengo yanayotarajiwa.

Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, kumekuwa na juhudi na nguvu kubwa kutoka kwa baadhi ya viongozi ndani ya Chadema kuwavunja nguvu akina mama hawa wenye weledi mkubwa katika majukwaa ya siasa nchini, kwa kutaka wavuliwe ubunge kwa madai kwamba wamevuliwa uanachama wa Chadema kupitia vikao vya Kamati Kuu. 

Kwanza kabla ya Chadema kutoa malalamiko juu ya mchakato wa kupatikana kwa wabunge hao, chama hicho kilipaswa kutangaza kuitambua serikali iliyopo madarakani na kutengua kauli ya kutoitambua serikali, kauli iliyotolewa na viongozi wa Chadema mara baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Tunapozungumzia uhalali wa wabunge 19 wa Viti Maalumu kutoka Chadema, ni vema kuanzia na mchakato mzima wa kikatiba uliotumika kuwapata. 

Kupatikana kwa wabunge hao 19 kumetokana na uchaguzi wa mwaka 2020, ambapo Chadema ndicho chama cha upinzani pekee kilichokidhi vigezo. 

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndicho chombo pekee chenye mamlaka ya kuteua na kutangaza majina ya wabunge walioshinda au walioteuliwa kutoka katika vyama mbalimbali vya siasa pamoja na walioteuliwa na Rais. 

NEC iliteua wabunge hao wa Chadema na ilimuarifu Spika wa Bunge kama Katiba inavyoelekeza.

Ibara ya 78(1) ya Katiba inaeleza kwamba; Kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge wanawake waliotajwa katika ibara ya 66(1) (b), vyama vya siasa vilivyoshiriki katika Uchaguzi Mkuu, kwa kufuata utaratibu uliowekwa, na kupata angalau asilimia tano ya kura zote halali za wabunge, vitapendekeza kwa Tume ya Uchaguzi majina ya wanawake kwa kuzingatia uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata katika uchaguzi wa wabunge. 

Aidha, imeeleza kuwa NEC ikiridhika kuwa mtu yeyote aliyependekezwa anazo sifa za kuwa mbunge itamtangaza mtu huyo kuwa amechaguliwa kuwa mbunge.

Kwa mujibu wa Ibara ya 78 ya Katiba, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kwa pamoja zinaainisha utaratibu wa uchaguzi wa wabunge wa Viti Maalumu kama ni suala la ndani ya vyama vya siasa vilivyoshiriki katika Uchaguzi Mkuu ambapo vyama hupaswa kupeleka NEC majina ya wanaopendekezwa kuwa wabunge wa Viti Maalumu. 

Kwa kuzingatia msingi huu wa kikatiba, NEC iliwasilisha barua kwa Spika iliyowatambulisha wabunge wa kuwakilisha chama hicho bungeni.

Baada ya kupokea majina haya kutoka NEC, Spika wa Bunge alitimiza wajibu wake kwa kuwaapisha wabunge hao wateule kwa mujibu wa Kanuni ya 30 (1) (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni, 2020 ili waanze kutimiza majukumu yao ya kibunge yaliyoainishwa na Katiba.

Katika hali ya kushangaza, siku chache baada ya wabunge hao kuapishwa rasmi na Spika, viongozi mbalimbali wa Chadema walianza kujitokeza hadharani na kutoa tuhuma kadha wa kadha dhidi ya Spika wakihoji kwa nini amewaapisha wabunge hao.

Miongoni mwa tuhuma iliyozua mshangao kwa jamii ni kudai wabunge hao si halali kwa kuwa uteuzi wao haukufuata taratibu za ndani ya Chadema,  na kwamba kuapishwa kwao hakukuwa halali, hivyo kumtaka Spika awavue haraka nyadhifa hizo muhimu za uwakilishi wa wananchi.

Ni vema ifahamike kuwa, viongozi hao wamesahau kwamba jukumu la kikatiba la Spika wa Bunge ni kupokea majina kutoka NEC na kuwaapisha, hivyo kwa kufanya hili, Spika alitimiza wajibu wake.

Mbali na kumlaumu Spika kwa kuwaapisha, uongozi wa chama hicho uliwasilisha barua Ofisi ya Spika ukidai kwamba Kamati Kuu ya chama hicho imewafuta uanachama, hivyo wanakosa uhalali wa kuendelea kuwa wabunge wakimtaka Spika kuwaondoa mara moja.

Jambo linaloshangaza barua hiyo ambayo Chadema walimuandikia Spika ili awaondoe bungeni wabungeni hao, haikuwa na uthibitisho wowote kama vile muhtasari wa kikao cha Kamati Kuu pamoja na orodha ya wajumbe waliokaa kwenye kikao kinachodaiwa kufanya uamuzi ya kuwavua uanachama wabunge hao.

Ibara ya 5.4 ya Katiba ya Chadema inazungumzia kukoma kwa uanachama ambapo Ibara ya 5.4.3 inaeleza kuwa mwachama atakoma uanachama iwapo ataachishwa ama kufukuzwa na tawi lake ama ngazi nyingine ya chama, kwa mujibu wa Katiba kwa kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama ama kuwa na mwenendo usioendana na Itikadi, Falsafa, Madhumuni, Kanuni, Maadili na Sera za Chama. 

Katiba hiyo inaeleza kuwa mwanachama atakuwa na haki ya kukata rufaa kwa ngazi ya juu kama hakuridhika na adhabu hiyo.

Aidha, Kanuni ya 6.5. ya Kanuni za chama za mwaka 2016 inaeleza taratibu za kuzingatia katika kuchukua hatua za kinidhamu kwa wanachama wa Chadema. Kanuni ya 6.5.1 inaainisha kuwa mwachama yeyote wa Chadema hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa, kuachishwa au kufukuzwa uanachama bila kwanza: 6.5.1(a) kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.

Kanuni ya 6.5.1(b) inaeleza kwamba: mwanachama atapewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kinachohusika.  

Swali la kujiuliza hapa ni kama wabunge hao walipewa nafasi hiyo kama Kanuni za chama chao zinavyoagiza, na kama ni kweli kulikuwa na ugumu gani wa kumpelekea Spika vielelezo vya jambo hilo?

Aidha, Kanuni 6.5.1(d) inaeleza kwamba Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura bila kuzingatia utaratibu wa kifungu (a) na (b) cha kanuni ya 6.5.1 kama itaona masilahi ya chama kwa ujumla yanaweza kuathiriwa, isipokuwa mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa atalazimika kuitwa kwenye kikao husika.

Hata hivyo mtu anaweza kujiuliza hivi kulikuwa na dharura gani ya kuwafukuza wabunge hao bila kuzingatia kifungu (a) na (b) vya Kanuni ya 6.5.1, kulikuwa na masilahi gani ambayo wabunge hao walikuwa wanahatarisha ndani ya chama mpaka kusababisha utaratibu wa kikatiba wa chama hicho usifuatwe? Na kibaya zaidi ni kwa nini mambo haya Spika asiyafahamu?

Aidha, kwa kuzingatia kifungu cha 5.4.3 cha Katiba yao, mwanachama anayo haki ya kukata rufaa kwenye ngazi za juu za chama ambapo rufaa yake itasikilizwa na kupewa majibu yake. Kwa mujibu wa maelezo ya wabunge hao, waliwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Chadema  barua yao ya kukata rufaa ya Desemba 23, 2020 kama Katiba ya chama chao inavyoelekeza. 

Katika hali ya kusikitisha, mpaka hivi sasa ambapo ni zaidi ya miezi sita tangu wawasilishe barua yao ya rufaa, kwenye mamlaka za Chadema, chama hicho hakijakaa kusikiliza rufaa hiyo kama Katiba yao inavyowataka ili kutoa haki kwa wabunge hao kujitetea dhidi ya shutuma hizo.

Kwa kuzingatia haya, ni dhahiri kuwa Chadema imekwenda tofauti na matakwa ya Katiba yake yenyewe kwa kutokuzingatia taratibu za chama hicho kama inavyopaswa, hivyo kuleta walakini wa namna mamlaka za Chadema zinavyoshughulikia migogoro yao ndani ya chama.

Hali hii inaleta ugumu wa kutekeleza madai hayo kutokana na walakini wa chama hicho kuzingatia matakwa ya sheria na hata katiba yao.

Katika maelezo yake bungeni Mei 7, 2021, Spika alifafanua kuwa anaongoza Bunge kwa kufuata Kanuni, Katiba, Sheria, Utaratibu, tamaduni na uamuzi wa maspika wengine na uamuzi wake unaweza kutumiwa na maspika wengine baadaye. 

Hivyo, alieleza kuwa anaweka misingi kwamba kwa vyama vyovyote vyenye kufukuza wanachama ambao ni wabunge, wanapaswa kila wanapomuandikia barua Spika, kumnakilia Msajili wa Vyama vya Siasa na kwamba ni lazima barua hiyo iambatane na katiba husika ya chama, muhtasari au mihtasari ya vikao vilivyohusika katika kuwafukuza wabunge hao na kutaja sababu za kufanya hivyo. 

Alifafanua kuwa utaratibu huu utarahisisha kutenda haki na kuonekana iwapo ni kweli haki imetendeka. Alisisitiza kwamba utaratibu huo utasaidia wengine wanaofukuzwa kwa kuonewa na yeyote kupata haki zao.

Kwa maelezo hayo, wabunge 19 wa Viti Maalumu wa Chadema ni halali kwa mujibu wa Katiba na taratibu zote za kupatikana wabunge na ni uthibitisho kuwa taratibu zilifuatwa. 

Halikadhalika Spika anayo haki ya kuwalinda wabunge wake ili kukomesha tabia ya vyama vya siasa ya kuwafukuza wabunge wake kiholela bungeni kwa madai ya kuwafukuza uananchama ili kupoteza nafasi zao za ubunge.

Ni vema sasa Chadema wenyewe waangalie mchakato wao wa ndani na kama wana jambo mahususi waliwasilishe Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambao ndio wahusika wa masuala ya uchaguzi badala ya kumuandama Spika.

1108 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!