Kama kuna mambo ambayo tuna hakika yatajirudia, tena na tena, ni matukio ya ugaidi katika sehemu mbalimbali duniani.

Katika tukio la juma lililopita raia wa Australia, Brenton Harrison Tarrant, amefunguliwa mashtaka ya mauaji nchini New Zealand akituhumiwa kupanga na kutekeleza tukio la kigaidi dhidi ya misikiti miwili na kusababisha vifo vya watu 49. Idadi kama hiyo ya watu wamejeruhiwa.

Tumezoea kusikia ugaidi kuhusishwa na imani ya dini ya Kiislamu, au tafsiri na miongozo ya dini hiyo. Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern, hakupata kigugumizi kutamka wazi kuwa kilichotokea Christchurch ni kitendo cha kigaidi. Wengine wamepata kigugumizi.

Tunaweza kushangaa chuki ya aina hii inatoka wapi, lakini hatuhitaji kwenda mbali kuelewa malengo ya Tarrant. Tarrant ni mfuasi wa imani za kibaguzi anayeamini kuwa binadamu mwenye rangi nyeupe ya ngozi ni bora kwa kila hali kuliko binadamu wenye rangi nyingine. Ni imani ambayo pia ni itikadi ya kisiasa. Ubora huo wa kufikirika hulindwa kwa hali na mali, madhumuni yakiwa kuhodhi nguvu za kiuchumi, kisiasa na kijamii dhidi ya binadamu wengine.

Ni watu wenye woga kuwa nguvu hizo ziko hatarini kupunguzwa kwa sababu ya sera za uhamiaji zinazoruhusu watu wasio wazungu kuhamia nchi ambazo yeye na wenzake wanaamini zinapaswa kubaki maeneo ya watu weupe. Ni hofu inayochochewa pia na ukweli kuwa hizo jamii nyingine, kwa desturi, zina kiwango cha juu cha kuzaa.

Kama ambavyo Mwalimu Nyerere amewahi kusema: ubaguzi hauna kikomo; hawa ni watu wanaoamini kuwa wapo wazungu wa aina fulani tu ambao wanastahili hadhi yao, si kila mzungu ni bora.

Kwa Tarrant, woga wake umemtuma kuwashambulia, kuwajeruhi, na kuwaua waislamu wa Christchurch, New Zealand.

Ugaidi wa aina hii unachochewa na vitu viwili vyenye ushawishi mkubwa: urahisi wa kusambaza habari kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano, na uhuru usio na mipaka.

Katika shambulizi lake, Tarrant alitumia mtandao wa Facebook kurusha mubashara tukio lile. Urahisi wa kurusha moja kwa moja matukio unakuwa kama kichocheo kwa watu ambao wana nia mbaya dhidi ya wenzao na wanatafuta umashuhuri kutokana na vitendo vyao.

Uhuru wa kujieleza, wa mawazo, wa fikra ni suala ambalo linaweza kuwa chanya au linaweza kuwa hasi. Uhuru huu umekuwa chachu ya baadhi ya matukio ya kigaidi tunayoyashuhudia  mara kwa mara. Tumeaminishwa kuwa uhuru wa kujieleza ni suala ambalo halipaswi kuwekewa mipaka hata kidogo, hata kama uhuru huo unahatarisha uhai wa binadamu wenzetu.

Kwenye kanuni za demokrasia tunaambiwa kuwa ni pale binadamu anaporuhusiwa kutoa mawazo na maoni yake kwa uhuru, bila vikwazo wala masharti ya kisheria na ili mradi hadhuru mtu mwingine, ndiyo demokrasia inakolea.

Mahakama ya Haki za Binadamu ya Nchi za Ulaya inatoa tafsiri pana ya uhuru wa kujieleza ikiongeza kuwa mawazo yanalindwa hata kama yanachukiza, au yanashtua. Anayetoa mawazo hana haja ya kupima ni kwa jinsi gani atawaudhi au kuwadhalilisha wengine.

Tatizo la msimamo wa aina hii ni kuamini kuwa kila binadamu ana shahada ya sheria na ana kidhibiti hasira ambacho kitazuia kuchukizwa na mawazo huru ya mtu mwingine.

Kwa hiyo makundi ambayo yanatumia uhuru huo kuchochea chuki na uhasama dhidi ya makundi mengine yanaweza kuendelea kufanya hivyo bila kuwa yamevunja sheria. Lakini tunasahau kuwa chuki ni kama mbegu iliyopandikizwa muda mrefu uliopita, na huchukua muda kuchipua na muda kukua na hatimaye hufikia muda wa kutoa maua na kuvunwa.

Tunasahau vipi kuwa mavuno ya kampeni za chuki na uhasama juu ya binadamu wengine ni matokeo ya mbegu iliyopandikizwa muda mrefu, mbegu ambayo kwa dhana potofu na ya kijinga ya kulinda uhuru wa mawazo na kujieleza isiyokuwa na mipaka tunasaidia kuipa mbolea na kuipalilia? Siku vikilipuka, kama ilivyotokea New Zealand, tunashangaa kinafiki kama vile hatufahamu kuwa sisi wenyewe tunachangia kushamiri kwa mawazo haya ya chuki na ukatili dhidi ya binadamu wengine.

Uhuru usio na mipaka ni chanzo cha baadhi ya matukio haya ya kigaidi, kwa hiyo hatuna budi kukubali kuwa ipo hitilafu ndani ya uhuru inayohitaji ukarabati.

Zipo nchi 16 za Ulaya ambako ni kosa kisheria kukana tu kuwa Wayahudi milioni 6 waliuawa na Ujerumani iliyotawaliwa na Adolf Hitler kwenye miaka ya 1930 na 1940. Inawezekana kuna haja ya kutajwa mahususi kwa kundi fulani la watu kwenye sheria kama njia mojawapo ya kutoa kinga ya uhakika dhidi ya chuki ambazo zinasababisha tukio la kigaidi kama la Christchurch.

Aidha, unahitajika uimarishwaji wa ushirikiano wa kimataifa dhidi ya vitendo vya kigaidi. Uwezo mkubwa wa mataifa makubwa wa kufuatilia mienendo ya binadamu popote duniani ungeelekezwa kikamilifu kwenye jitihada za kuzima vitendo vya kigaidi.

Lakini suala moja la msingi linahitaji mabadiliko ya fikra. Uhuru wa kujieleza ni muhimu, lakini umefika wakati sasa wa kupima iwapo uhuru huu ni chanzo pia cha kuleta maafa makubwa miongoni mwetu.

Maoni: barua.[email protected]

Please follow and like us:
Pin Share