Serikali ya Uingereza imetoa msaada wa Sh 307.5 bilioni kwa Tanzania ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais John Magufuli katika elimu, mapambano dhidi ya rushwa na uboreshaji huduma za afya.

Msaada huo umetangazwa leo Ijumaa Agosti 10, 2018 na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Penny Mordaunt alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, inasema kuwa Mordaunt amesema fedha hizo zimetolewa kuunga mkono vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mordaunt amesema Sh124.5 bilioni zitaelekezwa katika kuinua ubora wa elimu hususani kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu, Sh 23.5 bilioni zitaelekezwa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa, na Sh160 bilioni zitapelekwa kuboresha huduma za afya.

“Tunafanya hivi ili kudhihirisha dhamira yetu ya kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu, tunataka kujielekeza katika kuhakikisha Mhe. Rais Magufuli anafanikisha ahadi zake kwa Watanzania na tunafurahi kuwa wadau muhimu wa hilo,” amesema Mordaunt.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameshukuru kwa msaada huo na kumuomba Mordaunt kufikisha shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kwa mchango mkubwa ambao Uingereza hutoa kuchangia bajeti ya Serikali na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Namshukuru sana Waziri Penny Mordaunt kwa kutambua juhudi zetu za kuinua elimu, kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na kuboresha huduma za afya, msaada huu utatusaidia kuongeza nguvu kwa sababu watoto wakipata elimu bora, tukikomesha rushwa na watu wetu wakiwa na afya njema tutaweza kujenga viwanda na kukuza uchumi wetu kwa kasi zaidi,” amesema Rais Magufuli.

By Jamhuri