Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema polisi waliokuwa zamu siku ambayo mwandishi wa habari wa Wapo Redio, Sillas Mbise alishambuliwa na askari, wameanza kuchunguzwa.

Mbise anadaiwa kushambuliwa na polisi juzi Agosti 8, 2018 wakati wa mchezo kati ya Simba na Asante Kotoko ya Ghana uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Amesema jukumu la polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao na si kuwapiga raia waliotenda kosa ambao hawajakataa kutii sheria ya kukamatwa.

Mambosasa ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 10, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari, ikiwa ni baada ya kusambaa kwa video za tukio la kupigwa kwa mwandishi huyo katika mitandao ya kijamii, zikimuonyesha akishushiwa kipigo na polisi wawili.

“Tayari jeshi la polisi limefungua jalada la uchunguzi kuhusiana na tukio hili ili kubaini ukweli na tayari askari waliokuwa zamu eneo la tukio wameanza kuchunguzwa ikiwamo wawili kuhojiwa,”amesema Mambosasa.

Amesema pamoja na uchunguzi kuanza polisi wanamtaka mwandishi huyo kutoa taarifa kituo cha polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

“Tunamtaka mwandishi huyo kutoa taarifa kituo cha polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa kuwa mtu yeyote anatakiwa kutoa malalamiko pale anapoona anatendewa vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria,”amesema Mambosasa.

Please follow and like us:
Pin Share