Mtume  Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Ni bora kwa mtu kuchukua kamba akaenda mlimani na kuleta mzigo wa kuni mgongoni mwake na kuziuza ili Allaah ailinde heshima yake kuliko yeye kuomba kutoka kwa watu bila kujali kama watampatia au watamnyima.”

Makala yetu leo inaangazia Uislamu na kazi. Mafundisho ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) yaliyotufungulia makala hii yanatuonyesha uwepo wa aina mbili ya watu katika suala la kutafuta chumo la kukidhi mahitaji ya mtu katika maisha yake hapa duniani; aina ya kwanza, ni mtu afanyaye kazi na kupata pato lake, hivyo kulinda heshima yake. 

Aina ya pili, ni yule anayefanya kuomba kutoka kwa watu ndiyo kazi yake; mtu anayepata mapato bila ya kutumia jasho lake; mtu mwenye nguvu asiyekabiliwa na kikwazo chochote cha kufanya kazi na ameamua kuishi kwa kuwategemea wengine, na huyu ndiye aliyeuridhia udhalili katika maisha yake.   

Baadhi ya wataalamu wa lugha wamefafanua neno kazi kuwa juhudi za kimwili au kiakili zilizoelekezwa kufanya shughuli fulani au kutengeneza kitu fulani. Neno kazi pia ni malipo anayopewa mtu kwa amali, biashara, utaalamu, shughuli au ufahamu.

Katika Uislamu, kazi inamaanisha juhudi anazozifanya mtu katika shughuli yake binafsi au ya kuajiriwa ili kupata pato la halali na katika mipaka ya maagizo ya Mwenyezi Mungu na kanuni zake.

Kufanya kazi na kupata pato halali linalomuwezesha mtu kuendesha maisha yake akitafuta radhi za Mola wake na kuyaandaa maisha yake ya kesho ahera ndio utekelezaji wa mafunzo ya Uislamu kama tunavyosoma katika Qur’aan Sura ya 28 (Surat Al-Qas’as’), Aya ya 77 kuwa:

“Na utafute, kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya ahera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyokufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.”

Uislamu ni dini inayotambua na kuthamini umuhimu wa mali. Bila ya mali Muislamu hawezi kutekeleza ibada za Hijja, Zaka, Sadaka, kulea yatima na wajane, kujenga misikiti na madrasa, kuuguza wagonjwa hospitalini na majumbani, kuhudumia wazazi na kadhalika.

Uislamu unamtambua mwenye mali kwamba anazo ibada zaidi ambazo anaweza kuzifanya kuliko yule ambaye hana mali.

Kutokana na umuhimu mkubwa wa mali, Uislamu unamtambua Muislamu ambaye ameuawa wakati wa zoezi la kutetea mali yake asinyang’anywe kuwa amekufa akiwa ni miongoni mwa Mashahidi (watu waliopata ujira mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu).

Kuna njia nyingi za kupatia mali lakini njia bora kuliko zote ni mtu kufanya kazi akapata mali kutokana na jasho lake. Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Hakika bora ya chumo ni chumo la mtu linalotokana na mkono wake (kazi yake).”

Akafafanua zaidi Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) akasema: “Mwenyezi Mungu anampenda mja mwenye kufanya kazi na yeyote mwenye kuhangaikia familia yake anakuwa ni kama anayepigana Jihadi katika dini ya Mwenyezi Mungu.”

Akaongeza tena akasema: “Hakika katika madhambi kuna madhambi ambayo hayafutwi na Swala wala Swadaka wala Hijja na inayafuta madhambi hayo ile tabu anayoipata mja katika kutafuta maisha yake.”

Kutokana na umuhimu huo wa kufanya kazi ili kila mja apate riziki yake ya halali, akatufundisha Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) akatuambia: “Mkimaliza kuswali alfajiri msilale mkaacha kwenda kutafuta riziki zenu.”

Uislamu haukuishia tu kuelekeza na kufundisha umuhimu na ulazima wa kufanya kazi bali Uislamu umeelekeza mfumo wa kazi na ujira. Uislamu umemuelekeza muajiri kwamba Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amekataza kumpa mtu kazi yoyote mpaka kwanza ujira wake uwe wazi. Habari ya mapatano kwamba muajiriwa afanye kazi halafu mapatano ya ujira wake yawe baada ya kazi, hilo halikubaliwi na Uislamu.

Uislamu umemuelekeza muajiri pia kwamba baada ya kukamilika kazi ule ujira waliokubaliana na muajiriwa usicheleweshwe na ulipwe kwa mujibu wa makubaliano yao yalivyokuwa. Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Watu watatu mimi ni mgomvi wao siku ya Kiyama (mmoja wao) ni mtu aliyempa mtu kazi kisha hakumtekelezea ujira wake.”

Akaongeza tena kwa kusema: “Kumdhulumu mfanyakazi malipo yake ni miongoni mwa madhambi makubwa.”

Akamalizia Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) kwa kusema: “Mpeni mfanyakazi ujira wake kabla halijakauka jasho lake.”

Pia Uislamu umeelekeza kwamba katika kufanya kazi kuna nidhamu. Miongoni mwa nidhamu za kazi ni kutomuadhibu mfanyakazi kwa kosa ambalo limefanyika kwa bahati mbaya bila ya uzembe wake. 

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Msiwapige watumishi wenu kutokana na kuvivunja vyombo vyenu, hakika vina hivyo vyombo ajali kama ajali za watu.” Hapo tunapata mafunzo kwamba makosa yote ya bahati mbaya hatakiwi muajiri kutoa adhabu.

Kanuni nyingine ya nidhamu ya kazi inayoelekezwa na Uislamu ni mfanyakazi kuwa muadilifu na mkweli kwa muajiri wake na ajue kwamba kwa dhuluma yoyote anayomfanyia muajiri wake, hayo hayataishia hapa duniani, kwani kwa hakika kesho (Siku ya Hukumu) ataulizwa mbele za Mwenyezi Mungu na atapoteza thawabu nyingi atakazonyang’anywa na Mwenyezi Mungu kama fidia ili kumlipa muajiri aliyedhulumiwa na muajiriwa.

Amesema Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam): “Na mtumishi (mfanyakazi) ni mchunga katika mali ya bwana wake na yeye ataulizwa juu ya uchungaji wake.”

Kutokana na muktadha wa yote, kufanya kazi ni wajibu kwani ndiyo njia ya kupatia kipato, kipato ambacho kitamsaidia mtu kujikimu, kuikimu familia yake na kutenda mema yanayomridhisha Mola Muumba ambayo yanahitaji mali na bila ya mali hayatendeki kama vile kutoa Zaka na Sadaka.

Umuhimu na ulazima wa kufanya kazi unatimia zaidi pale ambapo mwanadamu anahitajia matumizi ya lazima kama vile mavazi, makazi, chakula, matibabu na kadhalika, na yote hayo yanahitajia mali. Na mwanadamu anaweza kupata mali kwa njia tatu:

Njia ya kwanza ni kurithi. Mwanadamu anaweza kurithi mali kutoka kwa wazazi wake. Si vema mtu kubweteka na kulemaa eti akisubiri wazazi wake wafe ili arithi mali apate kuendesha maisha yake kwa mali ya kurithi, na hata akiipata hiyo mali ya mirathi kama hana ‘akili’ ya kuiendeleza itakwisha yote. Njia nzuri ya kupata mali ni kujituma ili kupata pato halali.

Njia ya pili ya kupata mali ni kupewa sadaka, kuokota au kuletewa zawadi. Njia hizo nazo si endelevu na mwanadamu hutakiwi kuyapanga maisha yako kwa kutegemea vyanzo vya mapato visivyo endelevu.

Njia ya tatu ni kupata faida ya kibiashara au ujira wa kazi au fungu la ujira wa ushirika. Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) ameisifu sana hii njia ya tatu ya kuhangaika kufanya kazi za kuajiri au kujiajiri ili kupata chumo la halali na akakemea sana mtu kuyapanga maisha yake kwa kuyaendesha kwa njia ya kuombaomba. 

Jambo la kuombaomba amelikemea sana Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) kwa kusema: “Hakutaacha kuombaomba kwa mmoja wenu mpaka atakutana na Mwenyezi Mungu ilhali hana katika uso wake hata kipande kimoja cha nyama.”

Mafunzo ya Uislamu yanamkemea mtu mvivu asiyependa kufanya kazi na anayepanga maisha yake ayaendeshe kwa njia ya kuombaomba labda kwa yule mwenye dharura ya msingi, mgonjwa asiyejiweza, mlemavu, aliyeharibikiwa na mambo yake ya uchumi. 

Kwa kuwa kufanya kazi ni wajibu kwa kila mwanajamii ili apate pato lake la halali amudu na aweze kuyaendesha maisha yake; tumuunge mkono Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano, Dokta John Pombe Magufuli, katika kaulimbiu yake ya “Hapa Kazi Tu” yenye lengo la kutuhamasisha kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa, kwani kaulimbiu hii inakwenda pamoja na mafunzo ya Uislamu.

Hivyo basi, tunadi sote kwa kauli moja kwamba kila mwenye afya ya kufanya kazi afanye kazi kwani Uislamu unaamrisha kufanya kazi.

Tukutane wiki ijayo Inshaallaah.

Mwandishi wa makala hii ni Mwenyekiti wa ARRISAALAH ISLAMIC FOUNDATION. 

Unaweza kuwasiliana naye kwa namba: +255 754 299 749, +255 784 299 749.

By Jamhuri