Home Michezo Ujio wa Everton ni fursa

Ujio wa Everton ni fursa

by Jamhuri

Tanzania imeendelea kunufaika kiuchumi na ujio wa baadhi ya wachezaji wanaokuja kupumzika baada ya kukamilika kwa ligi katika nchi hizo.
Wachezaji hao ambao wengi wanatoka katika Ligi Kuu ya Uingereza wamekuja nchini kwa mapumziko ya msimu baada ya kumalizika kwa ligi kuu nchini humo (EPL).
Wachezaji waliokuja nchini ni Morgan Schneiderlin wa klabu ya Everton ya Uingereza, David Beckham, Mkenya Victor Wanyama na Christen Ericksen wa Klabu ya Tottenham Hotspur.
Wengine ni Mamadou Sakho toka klabu ya Liverpool na Leon Osman, kiungo wa zamani wa Everton, inayotarajiwa kuwasili Dar es Salaam, mapema mwezi Julai katika ziara ya maandalizi ya msimu ujao.
Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi wa Kampuni ya Sportpesa Tanzania, Tarimba Abbas amesema lengo la ziara hiyo kujenga ushirikiano na kuwapa hamasa ya vijana kuupenda mchezo wa soka.
“Ni jukumu letu sote kuhamasisha ukuaji wa soka hapa nchini kwa manufaa ya vijana, na taifa zima kwa ujumla” amesema Tarimba.

Akiwa hapa nchini kiungo wa zamani wa klabu ya Everton Leon Osman alifanya mazoezi na vijana wadogo katika uwanja wa Karume na kusema Tanzania kuna vipaji vinavyotakiwa na mipango ya kuwaendeleza.
“Baada ya kufanya mazoezi na vijana nimegundua uwepo wa watoto wengi wenye vipaji vya hali ya juu vyenye uwezo wa kucheza mpira,” amesema Osman.
Akizungumzia ujio wa wachezaji na Klabu ya Everton Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi amesema ni ujio wenye manufaa makubwa kwa nchi.

“Kwa mfano alipokuwa nchini mchezaji wa zamani wa Klabu hiyo Osman alipata muda wa kuwapa mafunzo vijana wetu kwa siku mbili na kuwapa mbinu mbalimbali,” amesema Madadi.
Madadi amesema katika nchi nyingine chama cha soka kinakuwa na jukumu la kuandaa mazingira mazuri ya timu za Taifa na siyo kutengeneza wachezaji kama ilivyozoeleka hapa nchini kwa kila jukumu kuachiwa TFF.
Ametoa mfano wa kikosi cha timu ya Ghana, chini ya umri wa miaka 17 kilikachoshiriki michuano ya Afcon yaliyomalizika hivi karibuni nchini Gabon, wengi walitoka katika vituo vya michezo.
Amesema pamoja na vyama husika kuwa na jukumu hilo lakini vijana wetu wanapaswa kuwa na wivu wa kimaendeleo na kujifunza kitu na ujio huu.

“Vijana wajifunze kwa Victor Wanyama aliyekuwepo nchini kwa mapumziko ambaye kwenye miaka ya 2006 alikuwa akichezea Nairobi City Stars, lakini leo ni mchezaji mkubwa duniani,” amesema Madadi.
Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga Afrika, Charles Mkwasa amesema ni jambo la heri kwa sababu uongozi wa klabu umekubali kutoa ushirikiano wa kiufundi na vilabu vya hapa nchini.
“Litakuwa jambo jema kama baadhi ya vijana wetu wa Serengeti Boys watapata nafasi ya kwenda kupata mafunzo katika chuo cha klabu hiyo,”amesema Mkwasa.

Katika ziara yake nchini Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Everton, Robert Elstone alinukuliwa na vyombo vya habari akisema timu yake ipo tayari kutoa ushirikiano kwa klabu au taasisi yoyote yenye nia ya dhati kuendeleza mchezo wa soka.
Amesema ni wajibu wa wadau wa soka kuwa tayari kujifunza kutokana na ziara ya klabu hiyo ambayo imewahi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza kwa miaka minane tofauti.
Amesema klabu yake ipo tayari kushirikiana na klabu au taasisi yoyote yenye nia ya dhati ya kuendeleza vipaji vya watoto wadogo kwa faida ya klabu na taifa husika.
“Ni viombe vyama vya soka kuwa na mipango endelevu hasa kwa vijana wadogo wenye vipaji, na klabu yangu haina kinyongo kwa kutoa msaada wa aina yoyote,” alinukuliwa akisema Elstone.

You may also like