Home Makala Ukarimu ni mzuri, ubahili ni mbaya

Ukarimu ni mzuri, ubahili ni mbaya

by Jamhuri

Binadamu anaweza kuwa na tabia ya ukarimu au ya ubahili katika kuweka uhusiano mzuri au mbaya na wanadamu wenzake. 

Ukarimu unajenga na unaenzi, na ubahili unaharibu na kubomoa uhusiano kati ya wanadamu. Hadhari kwa binadamu haina budi kutangulia kukinga ubaya kutokea.

Tabia mbili hizi kamwe haziwezi kuwekwa katika nafsi moja ya mtu kwa wakati mmoja. Lakini inawezekana kuwekwa kwa zamu. Mfano, ukarimu ukaanza na baadaye ukafuata ubahili, au kinyume chake. Mazoea yanaonyesha kila moja ina inda kumiliki nafsi ya mtu kwa muda wote.

Katika hali hii, wanadamu wanajikuta katika mgawanyiko wa wanadamu wema wenye tabia ya ukarimu na wanadamu wabaya wenye tabia ya ubahili.

Mfano, wale wema hutoa kwa hiari fedha au chakula kwa wanadamu wenzao. Na wale wabaya hawako tayari kutoa chochote kwa wenzao.

Ukarimu ni tabia ya utoaji wa fedha, mali, chakula na vitu vingine kwa ajili ya kusaidia wengine bila kutarajia malipo. Hapa tuangalie masuala ya hisani, wema, takrima, fadhila, jamala na upaji. Mambo haya unapoyafanya unakuwa karibu na Mungu, watu na Pepo, na unakuwa mbali na jahanamu.

Ubahili ni tabia ya mtu ya kutokuwa tayari kutumia fedha na mali zake kwa kuwasaidia wengine au kwa kutatua baadhi ya mahitaji yao. Hapa tuangalie masuala ya uchoyo, ugumu na unyimivu. Mambo haya unapoyafanya unakuwa mbali na Mungu, watu na Pepo. Unakuwa karibu na motoni.

Watanzania tumo katika makundi haya ya tabia, kuanzia kwenye kaya hadi taifa. Ndiyo maana katika nyumba zetu, kwenye taaluma zetu, katika shughuli zetu na katika uongozi wetu, wakarimu na mabahili hawakosekani. Ni juu yetu kujichunguza na kujirekebisha kitabia.

Baadhi ya wanadamu wanatambua ukarimu ni kutoa fedha, mali na chakula tu, bila ya kutarajia malipo. Hapana. Ni zaidi ya haya. Angalia katika maeneo ya hisani, fadhila, jamala, kusalimia, kuhimiza matendo mema na kadhalika. Ukweli unapofanya ubahili unajitenga na fadhila za Mungu na za watu.

Unapofanya ibada na kuzingatia taratibu zake, unapotoa hukumu na kuzingatia kanuni zake, unapokula chakula kilichopatikana kwa njia halali na unapohubiri mambo ya upendo unafanya ukarimu, na hauidhulumu nafsi yako. Matendo yote haya yanakuweka karibu na Mungu, watu na Pepo.

Wanadamu wengine wanatambua ubahili ni kutotumia na kutotoa fedha au mali tu kwa kuwasaidia wengine. Hapana. Ni zaidi ya haya. Hebu angalia katika maeneo ya uchoyo, unyimivu, kuhimiza watu kufanya matendo mabaya, au uasi na uchochezi. Yote ni ubahili.

Unapojijengea tabia ya kutosalimia watu, kujaa kiburi na kudharau wengine, kutomcha Mungu, kuwa na majivuno, kutoheshimu mamlaka na kufanya chochote kinyume cha ubinadamu, ni ubahili na upo karibu na motoni. Unaposoma fasihi hii vuta hisia wewe na jirani yako mpo Peponi au motoni?

Mataifa mengi yametumbukizwa katika kuvunja diplomasia ya kiuchumi na ya kisiasa kutokana na viongozi wao kuwa na tabia ya ubahili (choyo, wivu na ufisadi). Tazama yanayotokea sasa kati Iran na Marekani. Taifa lenye tabia ya ubahili dhidi ya taifa lenye ukarimu.

Baadhi ya viongozi wa siasa wakishirikiana na viongozi wa sheria na haki wa Afrika wanavyosema na kulalama dhidi ya viongozi walio madarakani (walioshika dola). Kisa na mkasa ni tabia hizi mbili – ya ukarimu na ubahili. Waafrika tunatazama matendo haya kama vile tunafurahia malumbano haya.

Viongozi wa serikali, vyama vya siasa, wa sheria na haki, wawakilishi wa wananchi, wa asasi za jamii na viongozi wa dini muwe wamoja kujenga tabia ya ukarimu ili muwe karibu na Mungu, watu na Pepo, na muwe mbali na motoni.

Nasi wananchi wa Afrika tuwe na tabia ya ukarimu na tusiwe na soni kuwataka viongozi wetu hawa kuwa wakarimu. Wote tunapokubaliana na kushirikiana kuvaa tabia ya ukarimu, tunaiweka Afrika katika hali ya neema, salama na amani. Tuwe karibu na pepo na tuwe mbali na motoni.

You may also like