Kuna msemo wa Kiswahili kwamba wagombanapo fahali wawili ziumiazo ni nyasi. Nimeukumbuka msemo huu kutokana na malezi yetu ya ufugaji na uchungaji wakati huo, hasa pale ambapo tulikuwa tukikutanisha madume wawili wa ng’ombe au mbuzi wapigane. Ukweli ni kwamba chini palikuwa panakuwa si salama kabisa kutokana na vita ile ya madume wawili.

Hili linataka kufanana kabisa na maisha ya familia ndani ya nyumba moja. Inapotokea mama na baba wakagombana kiasi cha kuleta taharuki ndani ya nyumba, watoto hupata shida ambayo kimsingi haikuwa yao ila imesababishwa na wazazi wao.

Katika ugomvi huo watoto wanaweza kujikuta wakisambaratika kutoka ndani na kila mmoja kushika njia yake kwenda kupambana na maisha mapya ya kujitegemea katika umri mdogo. Lakini pia watoto hao wanaweza kukosa huduma muhimu kwa maisha yao kwa sababu ya ugomvi huo. Hii ndiyo maana ya msemo huo wa wagombanapo fahali wawili ziumiazo ni nyasi.

Kama taifa, tunapaswa kujipanga kujitegemea, si kutegemea kutoka kwa taifa jingine ambalo hatujui litakwazika kiasi gani na vita yoyote. Siku za hivi karibuni nimewasikia watu wakizungumzia dalili za vita huko Mashariki ya Kati, eneo ambalo nchi za Afrika zinalitegemea sana kwa nishati ya mafuta. Iwapo kweli vita itatokea, ni dhahiri nishati hiyo tutaikosa na kusababisha hali ya uchumi wetu kuathirika kwa kiasi kikubwa.

Dhana kamili ya fahali wawili itakuwa imetimia kwa kutufanya tuyaone maisha kuwa magumu kutokana na vita isiyotuhusu. Pamoja na watu wachache kushangilia na kukoleza moto kwa vita hiyo, sina hakika kama watakuwa wanajua kuwa vita ile itakuwa ikipiganwa katika uchumi wetu kwa ujumla.

Kwanini leo nimeamua kuandika waraka wenye ujumbe huu? Ninataka tuelewe maana halisi ya kujitegemea ni ipi, hasa katika mazingira kama haya ya kuishi kwa wasiwasi kutokana na vita ya mataifa mengine pamoja na umbali wake.

Wakati tukipata uhuru tulikuwa na kaulimbiu ya kujitegemea. Kimsingi, kujitegemea maana yake ni uwezo wako wa kukidhi mahitaji yako bila kuhitaji msaada kutoka kwa mtu mwingine. Kujitegemea ni kuwa na kila kitu bila kusubiri mtu au taifa jingine lije kutoa mchango wake. Leo hii taifa letu lina kila aina ya vitu ambavyo vinaweza kutufanya tujitegemee.

Tunaendelea na utafiti kuhusu mafuta na kuna dalili kuwa yapo. Lakini ili tuweze kufikia hatua ya kuwa na mafuta yetu, hatuna budi kuwa na umiliki wa kila kitu, hasa katika suala la mtaji na teknolojia. Kasi tuliyokwenda nayo wakati wa kupata uhuru ni dhahiri kuwa labda leo tungekuwa mbali.

Wakati tunapata uhuru tulijitahidi kumiliki viwanda vingi vya bidhaa mbalimbali hapa nchini. Tuliweza kuchakata wenyewe bidhaa zetu na kuuza nje, tulikuwa na mapato zaidi kuliko sasa hivi ambapo thamani ya bidhaa zetu ni duni kwa kutochakatwa hapa nchini. Tuliuza viatu nje kwa kuwa ngozi tuliitengeneza hapahapa nchini na tuliuza almasi kwa kuwa kiwanda cha kuchonga kilikuwa hapahapa nchini.

Nilitegemea kwa miaka mingi ya kujitawala, leo tungekuwa wazalishaji wa bidhaa nyingi na kuuza nje na matokeo ya kuuza nje yangefanya serikali kuwa na fedha nyingi za kigeni na kuweza kuingia katika teknolojia ya kutafuta mafuta na kuzalisha mafuta kama mataifa mengine.

Matokeo ya kuzalisha bidhaa nyingi yangefanya taifa letu kuwa tajiri na lenye nguvu ya kiuchumi na kuzitisha nchi ambazo zinataka vita na sisi hasa ya kiuchumi.

Haya tunayaona katika nchi ambazo tulipata nazo uhuru na tukaanza pamoja siasa ya ujamaa na kujitegemea, wenzetu sasa wanajitegemea na bado wanatukopesha fedha zao kwa ajili ya maendeleo yetu, lakini kubwa zaidi hawafikirii juu ya vita ya watu wengine kwa kuwa nao ni mafahali pia.

Nadhani tumejifunza kutoka kwa wenzetu wa China. Nadhani tumejifunza maana halisi ya utumishi ulioacha alama ya maendeleo na siyo siasa. Nadhani tumejifunza tulipojikwaa mpaka tunatibiwa na yule tuliyeongozana naye katika safari.

Tujiulize, kwanini sisi tunawaza vita ya mbali kwa mustakabali wa taifa letu lakini wengine hawawazi kuhusu vita hiyo bali wanawaza biashara kufanyika kupitia vita hiyo? Kalaghabaho.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri