“Ukitaka kujua umuhimu wa mwaka mmoja muulize mwanafunzi ambaye amerudia darasa.
Ukitaka kujua umuhimu wa mwezi mmoja muulize mwanamke ambaye amejifungua mtoto kabla
ya mwezi mmoja. Ukitaka kujua umuhimu wa juma moja muulize mhariri wa gazeti linalotoka
kila wiki.
Ukitaka kujua umuhimu wa siku moja muulize mtu mwenye kibarua cha kulipwa kwa siku wakati
ana watoto kumi wa kulisha. Ukitaka kujua umuhimu wa saa moja waulize wachumba ambao
wamepanga kukutana baada ya saa moja kufunga ndoa. Ukitaka kujua umuhimu wa dakika
moja muulize mtu ambaye ameachwa na gari stendi.
Ukitaka kujua umuhimu wa sekunde moja muulize mtu ambaye ameponea chupuchupu katika
ajali. Ukitaka kujua umuhimu wa milisekunde muulize mtu ambaye ameshinda medali ya fedha
katika mashindano ya mbio”.

– Padre Faustine Kamugisha

Rais wa 36 wa Marekani, Lyndon B. Johnson, alipata kusema hivi, “Jana siyo ya kwetu tena na
hatuwezi kuirudisha, ila kesho ni yetu ya kushinda au kushindwa’’. Ninaomba kukuuliza swali
hili: Kama leo ndiyo ingekuwa siku yako ya mwisho ya kuishi hapa duniani ungefanya nini?
Ungeitumia kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha ili akusamehe dhambi zako na kukupokea
katika ufalme wake milele? Ungeitumia kugawa urithi? Ungeitumia kuwaaga ndugu, marafiki na
majirani? Ungeitumia kufanya nini?
Jiulize. Martin Luther kwa upande wake alisema, “Hata kama leo ingekuwa siku yangu ya
mwisho bado ningefanya kazi ambayo ingezaa matunda kwa ajili yangu au kwa anayekuja
nyuma yangu’’. Wakati wote muda ni rafiki wa ‘mafanikio’ na pia ni adui wa ‘mafanikio’. Tawala
muda wako uyatawale maisha yako, poteza muda wako uyapoteze maisha yako. Furahia muda
wako uyafurahie maisha yako. Maisha ni muda.
Mshairi William Shakespeare alipata kujilaumu kwa kuandika hivi, “Nilipoteza muda, sasa muda
unanipoteza”. Mwandishi Anna Robertson Brown anashauri hivi, ”Uwe na hekima katika
kutumia muda. Swali la maisha si ‘tuna muda kiasi gani?’ swali ni tunafanya nini na muda
tulionao?” Muda ni mali. Muda ni rasilimali aliyonayo kila mtu. Mwanafalsafa Theophrastus
anasema, ”Muda ndiyo kitu cha thamani sana anachoweza kutumia mtu”. Mwandishi Carl
Sandburg anasema, ”Muda ni sarafu ya maisha yako. Ndiyo sarafu pekee uliyonayo, na ni
wewe pekee unayeweza kuamua namna itakavyotumika. Uwe mwangalifu usije ukaacha
wengine wakaitumia badala yako”.
Si mara moja umesikia au hata kuona watu wamekaa tu huku wakisema, ”Tupo hapa
tunapotezapoteza muda”. Looooo! Umewahi kufikiria uzito wa maneno hayo? Maneno haya ni
maneno ya kujiua. Ni kauli za kujiangamiza. Wakati mtu anapotezapoteza muda si kwamba
maisha yake yanakuwa salama bali nayo yanapotea na muda unapotezwa. Kupoteza muda ni
kupoteza maisha.
Kuangamiza muda ni kuyaangamiza maisha. Maisha yanaunganika moja kwa moja na dhana
nzima ya muda. Mwanasayansi Charles Darwin anatufundisha hivi, “Binadamu anayethubutu
kupoteza saa moja kwa kukaa bure, bado hajafahamu thamani ya maisha yake’’.
Jemedari Napoleon Bonaparte (1769-1821) aliyepata kuwa mfalme wa ufaransa, alipata
kusema, “Ipo aina moja ya jambazi ambaye sheria haipambani naye, lakini ndiye anayeiba
kilicho cha thamani kubwa kwa mwanadamu – ‘Muda’. Tuutumie muda vizuri. Mwandishi Petro

Feba anasema, “Muda ni mjumbe wa Mungu’’. Jana iliyopita huwezi ukaifufua. Wiki iliyopita
huwezi kuifufua.
Mwezi uliopita huwezi ukaufufua. Mwaka uliopita huwezi ukaufufua. Ukipoteza muda, muda
utakupoteza zaidi. Napoleon alizoea kuwaambia wanafunzi wake nasaha hii, “Kila saa
unayopoteza ni fursa ya kuwa na balaa baadaye”. Alfred Montapert anasema, “Ukichagua
kuchezea muda huwezi kukwepa matokeo yake ambayo siku zote ni mabaya tu’’. Muda ni mali.
Ni vizuri kuthamini muda.
Shujaa Nelson Mandela anashauri hivi, “Inatupasa tutumie muda vizuri na siku zote tukumbuke
muda huenda sahihi’’. Kila siku unayopata kuishi hapa duniani ina umuhimu wake. Methali ya
Kifaransa inasema, “Hazina zote za duniani haziwezi kurudisha fursa moja iliyopotea’’.
Ndiyo kusema, utajiri wote wa ulimwengu hauwezi kurudisha nyuma dakika moja iliyopotea.
Nukta moja ya muda iliyokwishapita haifanani na ile mpya inayokuja. Kila sekunde, dakika, na
saa mpya ni tofauti kabisa na zilizokwishapita. Kila nukta moja ya muda huja na kuacha chapa
yake ambayo ni tofauti na chapa itakayoachwa na nukta nyingine ya muda.
Mwanafalsafa Heraclitus anasema, ”Muda ni kama mto. Huwezi kuyagusa maji yale yale mara
mbili, kwa sababu mtiririko uliokwishapita hautopita tena”.
Ndiyo kusema, muda ni kama matone yashukayo kutoka mawinguni na kuinyeshea ardhi.
Yakishanyunya kutoka angani huwa hayarudi tena yalikotoka. Kama yatashuka mengine hayo
ni mapya tofauti kabisa na yaliyokwisha kushuka kwanza.
Muda si kiporo cha wali ambacho unaweza kukitunza na kukipasha badaye ili upate kukila tena.
Mafanikio ya mtu yanategemea namna anavyotumia muda wake. Siku zote zina saa sawa,
lakini hazilingani. Jumatano si Ijumaa na wala Alhamisi si Jumapili.
Kuishi ni fursa na muda ni fursa. Mwanadamu anaishi mara moja tu hapa duniani. Tunaloweza
kulifanya sasa, tulifanye kwa sababu hatuishi mara ya pili hapa duniani. Kubahatika kuishi
duniani ni fursa. Ni fursa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Ni fursa ya kuwa sikio kwa wale
wasio na sikio.
Ni fursa ya kumgeukia Mungu na kuyapa mgongo matendo ya giza. Ni fursa ya kuchukia
dhambi. Kuwapo kwetu duniani iwe sababu ya mwanga palipo na giza. Kuishi ni fursa. Ni fursa
ambayo tumezawadiwa bure na Mwenyezi Mungu. Fursa hii inatudai kuishi maisha ya uadilifu,
upendo, amani, umoja na msamaha.
Mfalme Daudi anatufundisha kumwomba Mwenyezi Mungu kwa sala hii, “Utufundishe ufupi wa
maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima’’ (Zab 90:12). Kila siku ni mpya. Kila siku tuwe wapya
wa kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitii. Kila siku Mwenyezi Mungu anakupa fursa ya
kuyatathmini maisha yako.
Anakupa fursa ya kuwasamehe waliokukosea. Anakupa fursa ya kuwaomba msamaha wale
uliowakosea. Anakupa fursa ya kuboresha mahusiano yako na familia yako na jamii
inayokuzunguka. Anakupa fursa ya kuwawekea watoto wako msingi imara wa kiimani, kimaadili
na kindugu. Itumie fursa hii vizuri na kwa muda unaofaa.
Rais Thomas Jefferson aliwahi kusema hivi, ”Watu wengi hufa kwenye umri wa miaka 25, lakini
wanazikwa wakiwa na umri wa miaka 70”. Tujiulize ni kwa nini Jefferson aliandika fumbo hili. Ni
kwamba umri wa maisha siyo miaka ni muda.
Mfano mzuri ni huu: ‘Kijana anaweza kufa akiwa na umri wa miaka 30 lakini kuishi kwake
kukawa na thamani ya miaka 100 kutokana na yale aliyoyatenda enzi za uhai wake. Na
kinyume chake ni kwamba, mzee aweza kuishi miaka 100 lakini kuishi kote huko kukawa na
thamani ya miaka 30 kutokana na yale aliyoyatenda enzi za uhai wake’.

Ishi kabla ya kufa. Kuna watu wanakufa kabla ya kuishi. Kivipi watu wanakufa kabla ya kuishi?
Nakujibu nisikilize kwa makini. Mtu yeyote aliyekata tamaa na maisha ni kama amekufa ingawa
bado anavuta hewa katika sayari hii ya dunia.
Kila mara tunapoacha kufanyia kazi ndoto zetu tulizonazo au tupoamua kuacha kutumia vipaji ni
kama tunaanza kufa. Tunapoacha kutenda matendo yenye kuleta ustawi kwetu na kwa
wenzetu, tunaanza kufa. Tunapolalamika kwa kila jambo ni kama tunaanza kufa. Unaposoma
makala ya kitabu hiki fufuka. Fufua ndoto zako upya.
Padre Faustine Kamugisha katika makala yke ya ‘Kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa’,
iliyochapishwa na gazeti la JAMHURI, ISSN1821-8156, Toleo No. 310, September 5-11, 2017
aliandika hivi, ”Usipopanga basi fahamu kuwa unapanga kushindwa. Makaburi mengi yamejaa
watu walioaga dunia wakiwa na mipango mingi, lakini hawakuitekeleza”. Ninakubaliana kabisa
na andiko la Faustine.
Mchungaji Dwight L. Mood anasema, ”Maandalizi ya uzee yaanze ukiwa kijana. Maisha ambayo
yana utupu wa lengo mpaka miaka 65 hayatajazwa ghafla ukistaafu”. Kuna Methali ya Kiafrika
isemayo, ”Vinavyoliwa na nywele nyeupe viliandaliwa na nywele nyeusi”. Nywele nyeusi
zinawakilisha umri wa ujana. Nywele nyeupe zinawakilisha umri wa uzee.
Liwezekanalo leo lisingoje kesho. Mchezaji wa mpira, Jerry Rice, anasema, “Leo nitafanya
ambayo wengine hawatataka kufanya ili kesho niweze kutimiza ambayo wengine hawataweza
kutimiza’’. Methali ya watu wa China inasema, “Maua ya kesho yako kwenye mbegu za leo’’.
Kesho yako haiwezi kuongelewa bila leo yako.
Leo ni akiba ya kesho. Kesho ni mavuno ya leo. Unachopanda leo ndicho utakachovuna kesho.
Izungumzie kesho yako kwa kuangalia leo yako. Pd. Dkt. Faustin Kamugisha anasema,
“Tusiiogope kesho kwa vile matunda ya kesho yamo kwenye mbegu za leo. Leo tuishi vizuri ili
kesho iwe ya maana”.
Abraham Lincoln naye anateta kwa maneno haya, “Huwezi kukwepa kuwajibika kesho kwa
kukwepa kuwajibika leo”. Kesho hujaiona na hujui itakuaje lakini maamuzi yako yanaweza
kuiharibu kesho yako au yanaweza kuijenga kesho yako. James Allen anasema hivi, “Leo uko
pale ambapo mawazo yako yamekuleta, kesho utakuwa pale ambapo mawazo yako
yamekupeleka’’.
Jenga leo yako vizuri ili uifurahie kesho yako. Mwanahabari mkongwe Jenerali Ulimwengu
anashauri kwamba, “Leo lazima iwe bora kuliko jana, na kesho kuliko leo, la sivyo kuna tatizo’’.
Kila mara kuna watu ambao wanataka kuishi kesho, lakini wanashindwa kuifurahia leo.

Please follow and like us:
Pin Share